Tangulia Joni Woka, hii ni safari ya wote

18Feb 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Tangulia Joni Woka, hii ni safari ya wote

WIKI hii imekuwa ni ya majanzi kwa muziki wa kizazi kipya baada ya kupata pigo la kuondokewa na mmoja wa wasanii waliowahi kutamba na kwa nyimbo mbalimbali akiwa na kundi la WA2KU2.

JOHN WOKA

Msanii huyo ni Denis Michael Mhina ama 'Joni Woka' kwa jina la kisanii ambaye alijipatia umaarufu mkubwa kwa staili yake ya kurapu kwa staili kama ya mtu mlevi ingawa hakuwa mnywaji pombe.

‘John Woka’ alifariki dunia alfajiri ya Jumanne wiki hii katika hospitali ya taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa baada ya kulipukiwa na gesi mwakati akitengeneza gari lake, maeneo ya Sinza, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa kaka yake aliyejitambulisha kwa jina la Omari Millay, mwili wa marehemu ulisafirishwa jana kwenda nyumbani kwao jijini Tanga kwa ajili ya mazishi ambayo yanatarajiwa kufanyika leo.

Millay alisema kuwa Joni Woka alizaliwa mwaka 1981 jijini Dar es Salaam Tanga akiwa ni mtoto wa tatu, lakini akiwa ni mtoto wa kwanza kwa mke wa sasa wa mzee Denis Mhina.

Alihitimu kidato cha nne mwaka 2000 katika Sekondari ya Tanga Technical na kisha akaanza kujishughulisha na shughuli mbalimbali zikiwamo za ufundi wa umeme wa magari kabla ya kuibukia kwenye muziki wa kizazi kipya uliomfanya ajulikane kwa watu wengi.

Kwa mujibu wa kaka yake huyo, marehemu Joni Woka ameacha mke na mtoto wa kike wa miaka minne lakini akiashindwa kuwataja kwa majina, kwa madai kwamba alikuwa hajayajua vizuri.

Joni Woka aliibuliwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 na kundi la Wagosi wa Kaya baada ya kumshirikisha katika nyimbo za 'Lidandasi za Majungu' na 'Walimu', ambazo zote kama kawaida yake alikuwa akirapu kwa staili kama mtu mlevi.

Wakati huo kundi hilo liliwika kwa nyimbo mbalimbali kutokana na mtindo ambao lilikuwa likitumia wa kuimba kwa lafudhi ya makabila ya mkoani Tanga, huku Woka akichombeza kama mlevi.

Mbali na nyimbo hizo, kundi lilifyatua nyimbo za 'Kunani Kule Tanga', 'Wauguzi', ‘Wakulima’ na nyingine nyingi, ambazo zilikuwa katika albamu yao ya kwanza waliyoipa jina la ‘Tanga Kunani’ walioitoa mwaka 2001.

Makundi yaliyoasisi muziki wa kizazi kipya nchini, Wagosi wa Kaya ambalo tangu lilipojikits katika medani hiyo lilikues likitosa nyimbo zilizogusa jamii kwa namna moja ama nyingine.

Baada ya kuvutiwa na uimbaji wa Joni Woka aliyeibuliwa na kundi hilo, wasanii mbalimbali walianza kumshirikisha katika nyimbo zao akiwamo Ras Lion ambaye baadaye alikuwa mtu wake wa karibu wakaungana na kuanzisha kundi la WA2KU2.

Baadhi ya nyimbo walizotamba nazo katika kundi lao hilo ni 'Hii Kitu', 'Sophia', 'Baby Gal', 'Yalaah', 'Nikikupata', 'Hodi Mganga', 'Sumu ya Panya', 'Mkora' na nyingine nyingi zilizolifanya kundi hilo kuendelea kuvuma.

Hata hivyo, baadaye mwenzake Ras Lion aliamua kuachana na muziki na kujishughulisha na biashara ambazo hakuziweka wazi akidai kwamba soko la muziki wa kizazi kipya limekuwa gumu.

Msanii huyo alitimkia mkoani Arusha ambako aliamua kuweka maskani yake huku na kumwacha Joni Woka ambaye naye mbali na muziki alikuwa akijishughulisha na ufundi wa umeme wa magari hadi mauti yanamkuta.

Akimzungumzia marehemu, Ras Lion amesema kuwa amepoteza rafiki wa kweli ambaye walifanya naye kazi za muziki kwa uelewano mkubwa na pia kuishi pamoja kama ndugu ingawa wanatoka mikoa tofauti.

"Mimi ninatoka mkoa wa Mwanza, yeye alikuwa ni mwenyeji wa mkoa wa Tanga, lakini tuliishi vizuri sana na kufanya kazi pamoja bila kukwaruzana kama ilivyo kwa abaadhi ya wasanii...nimepoteza rafiki wa kweli," amesema Ras Lion kwa masikitiko. Kwa upande wake mmoja wa wasanii wa kundi la Wagosi wa Kaya, Fredrick Maliki 'Mkoloni' amesema kuwa mwanzoni watu walidhani kwamba Joni Woka ni mlevi kutokana na staili yake ya kurapu. Amesema kuwa baada ya kugundua kuwa sio mlevi, walimpenda na kumshabikia kila wanapomuona hata kama sio jukwaani na kumfanya awe maarufu zaidi kwenye muziki wa kizazi kipya. "Sisi kama Wagosi wa Kaya tuliona kipaji chake na kuamua kukiweka wazi kumshirikisha katika nyimbo zetu na alipoonekana katika video ndipo umaarufu wake ukaongezeka hasa staili aliokuwa akitumia," amesema Mkoloni. Amesema kuwa Joni Woka aliibuka na ubunifu wa kuimba kama mtu mlevi na kupata umaarufu na ameondoka nao na kwamba hakuna msanii aliyewahi kuuiga. "Kundi letu likuwa linataka ubunifu wa aina hiyo ndio maana kwa muda mfupi tuliibuka kwa kishindo na kupata umaarufu mkubwa mashabiki na tulimshirikisha Joni Woka kwa sababu alikuwa mbunifu kama sisi," amesema na kuongeza: "Ukisikiliza nyimbo zetu ‘Ripoti Kamili’, ‘Trafiki’ ‘Soka la Bongo’, ‘Safari Zetu’, ‘Nyeti’ ‘Kiinua Mgongo’, ‘Ushauri wa Bure, ‘Tizauye Kaya’, ‘Kibaka’, ‘Hotuba’, ‘Hamna Shida’, utagundua ubunifu wetu, ambao pia Joni Woka alikuwa nao." Amesema kuwa Joni Woka ameondoka na ubunifu wake ambao umemfanya apate umaarufu kwenye muziki wa kizazi kipya kama alivyokuwa msanii Mr Ebbo ambaye naye aliondoka na ubunifu kwa lafudhi ya kabila la Kimasai.