Yamoto Band kunogesha Kilimanjaro Lager Marathon

19Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Yamoto Band kunogesha Kilimanjaro Lager Marathon

MBIO za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zinakuja kwa staili ya aina yake mwaka huu baada ya kundi la Yamoto Band kuteuliwa kutumbuiza mashabiki na washiriki wa mbio hizo.

YAMOTO BENDI

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambao ndiyo wadhamini wakuu wa mbio hizo, Pamela Kikuli, alisema wameichagua bendi hiyo kwani ndiyo moja ya bendi zinazopendwa kwa sasa.

“Tuna uhakika kwa umati wa watu zaidi ya 10,000 ambao unatarajiwa pale, bendi hii itawapa burudani ya aina yake kwani ina waimbaji mahiri na pia wanacheza vizuri,” alisema meneja huyo.

Mbio za Kilimanjaro Premium lager zinatarajiwa kuwavutia washiriki zaidi ya 4,000 kutoka nchi zaidi ya 45, zitafanyika Jumapili Februari 28 katika viwanja vya Chuo Cha Ushirika Moshi (MoCU) ambako jukwaa la burudani litafungwa.

Kwa mujibu wa meneja huyo, wasanii wanaochipukia kutoka mkoa wa Kilimanjaro pia watapata fursa ya kutumbuiza katika jukwaa moja na Yamoto.