Sasa anaona mabadiliko makubwa.Huyo ni mwanamke wa jamii ya wafugaji Wamasai, ambao ilikuwa ni mwiko kwao kumiliki mfugo, hata kutoa uamuzi juu ya maslahi binafsi, licha ya kazi ya kuihudumia aliyofanya, ikiwamo kupelekea mifugo malisho, kusafisha zizi na kukamua maziwa asubuhi na jioni.Mali yake kubwa ilikuwa maziwa yanayokamuliwa asubuhi tu, tena yaliyobaki baada ya kutenga ya matumizi ya nyumbani. Maziwa ya jioni pamoja na faida ya kuuza ng’ombe ni mali ya baba, jambo ambalo ni kinyume na Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya Mwaka 2000, inamyotaka mwanamke kushiriki katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii vizuri zaidi .
“Kama hiyo siku maziwa ya asubuhi hayakupatikana mengi sipati ya kupeleka mnadani kuuza, yakipatikana mengi ndio napata kama lita mbili naenda kuuza, pesa inatumika kununulia watoto mafuta na sabuni ya kutumia hapa nyumbani, kuna wakati nilikuwa nahisi unyonge lakini sasa umekwisha,” anasema Happy.
Unyonge wa mama huyo mwenye mume na watoto watatu, ukakoma mwaka jana baada ya kikundi chao cha vikoba kinachoitwa Galilaya, kutembelewa na taasisi binafsi ya Ujamaa Community Resource Team (UCRT), hata wakapewa elimu ya kujitambua, sasa imewanyanyua, wakiitegemea kiuchumi.
Kupitia taasisi hiyo Happy na wana kikundi wenzake 30 wamepata elimu ya kufuga kisasa, wakinenepesha mifugo, biashara na pesa za kutunisha mfuko wa kikundi hicho, ndipo akachukua mkopo Sh. 500,000 akanunua ngombe wawili sasa jike limezaa mapacha na linatoa lita nne ya maziwa kila siku, anamiliki bila kupimiwa na mumewe.Kupitia biashara ya kuuza maziwa hayo, Happy ana uhakika wa kupata si chini ya Sh. 5000 kwa siku anazotumia kuhudumia watoto na kulipa marejesho ya mkopo kila wiki.
Pia, ameeshaongeza mifugo ya kuku ambao mara anapouza, inamsaidia kulipa deni, jambo analosema limemuongezea heshima kwa mumewe.
Upande wa pili, anakumbusha akiwa kama mama wa nyumbani akiwa na jukumu la kuingia msituni kukata miti kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, sehemu ya mkopo alinunua gesi kuondokana na uharibifu wa mazingira na kuchochea ongezeko la mabadiliko ya tabianchi, sasa anatumikia elimu aliyoipata kupitia UCRT.
Happy ni kati ya wanawake 90 walionufaika na mikopo, elimu ya kufuga kisasa, biashara na madhara ya kutumia kuni kiafya na kimazingira.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mawakini Violet Elias, ni jambo lililobadilisha maisha yao kiuchumi na kuwaondoa kwenye utumwa wa waume zao, sasa wanahamasisha mabadiliko katika jamii zao.
Mwingine ni Yasinta Tango, aliyenufaika na mkopo Sh. 700,000 akanunua mbuzi watatu, kuku sita na sehemu ya pesa akanunua gesi ya kupikia, baada ya kuona faida zake kiafya na kiuchumi, ikiwamo kutumia muda mdogo kupika, anapata muda zaidi wa biashara zake.
“Nilipouza kuku mwezi uliopita kiasi cha fedha nikaanzisha biashara ya kuuza maandazi jioni na faida yake zinanisaidia kuongezea fedha za kulipia deni ninalodaiwa vikoba,” anasema.
Mama huyo anasimulia alikotoka, ilikuwa vigumu kumhamisha mume wake kutoka kwenye dhana ya kutumia kuni, kuelekea kwenye gesi, akimhamisha kutoka imani kuwa gesi zinalipuka kila mara na kuwasababishia vifo.
Happy anataja pesa za mkopo zilimuwezesha kununua gesi na kuipeleka nyumbani na baada ya kutumia muda mrefu bila madhara mume wake akaridhika.
“ Baada ya kuipeleka ile gesi nyumbani kwa nguvu, mume wangu alikasirika na kuniambia watoto wake wakilipuka nitawalipa, lakini kwa kuwa tulielekezwa njia salama za kutumia gesi na ninazifuatilia vizuri, sasa ni miezi sita hakuna madhara yoyote yametokea hata mume wangu sasa anasaidia kubadilisha mtungi” anasimulia.
MWENYEKITI NA HISTORIA
Mweyekiti wa kikundi hicho, Suzana Leonard, anasema kikundi hicho kilianza mwaka 2018 kama Baraza la Haki la Uongozi wa Wanawake, kikiwa na wanachama 30 wa kutetea haki za watoto wa kike wanaonyanyasika kijinsia.
Anasema, walichanga kila mmoja Sh.5000 wakanunua mbuzi 24 wa kufuga, kwa lengo la kugawana pale wanapozaa, lakini mwaka 2021 mifugo tisa ilikufa, kutokana kukosa malisho bora, baada ya kuibuka ugonjwa wa UVIKO-19 uliolazimisha familia kukaa ndani na kupunguza misongamano.
“Kipindi cha uviko-19 kikoba kiliyumba, mpaka mwaka jana tulipotembelewa na UCRT na kutupa elimu ya biashara na Sh. milioni saba ambazo tumenunua viti 100 kwa ajili ya kukodisha na nyingine tumekopeshana kwa ajili ya miradi ya mtu mmoja mmoja, ambayo ndio imetuwezesha kununua gesi na kuondokana na matumizi ya kuni kupikia,” anasema.
Mwenyekiti huyo anasema, malengo ya kikundi ni kuongeza viti idadi ifike 300, kununua turubai ya kukodisha na bajaji ya kupelekea viti kunakohitajika, ili kurahisisha huduma na kuwavutia wateja wengi, hata wapate faida nyingi.
Vilevile, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mawakini, Violet Elias, anasema tangu kutembelewa na UCRT wamehamasisha wanawake wengi kujiunga na vikoba ili kupata mikopo, kuachana na matumizi ya kuni kutoka kikundi kimoja na sasa vipo vitatu vyenye jumla ya wanachama 90, vipo chini ya Baraza la Haki la Wanawake na Uhifadhi Mazingira.Anasema, mikopo hiyo pia imewaondoa wanawake kutoka kuwa wategemezi wa chanzo kimoja cha biashara ambapo walikuwa wakitegemea kuuza maziwa na baada ya mifugo kufa na biashara zikafa lakini sasa wanafanya biashara nyingine ikiwamo kuuza maandazi, migahawa na kufuga kuku.
“Katika jamii ya kifugaji japo kuwa mwanamke anafanya kazi ngumu ya kulisha mifugo, lakini mali yake pale ni maziwa tu na anaruhusiwa kuuza yale yaliyobaki baada ya kutoa ya kutumia nyumbani.
“Ng’ombe ni mali ya baba yeye ndio anauza na hela ni ya kwake, kwa hiyo kadiri mifugo inavyopungua mama anaathirika zaidi, sasa tunashukuru tuna uwezo wa kununua mifugo yetu wenyewe na kufanya biashara nyingine,” anasema.
Meneja Mradi kutoka UCRT, Fred Loure, anasema mradi wa taasisi USAID - Tuhifadhi Mazingira, waliwafikia wanawake hao mwaka jana na kuwapa elimu biashara kupitia vikundi vya vikoba, lengo ni kuwashawishi kuachana na ukataji miti, wahamie kutunza maliasili, mazingira na wanyamapori.
“Moja ya elimu tuliyowapa ni ile ya kufunga maeneo ya malisho, tumewaelekeza kipindi kama cha sasa ambacho majani ya malisho yapo mengi, wafunge mapori yaliyotengwa kulisha mifugo ili yachipue, halafu watayafungua baada ya miezi mitatu kunakuwa na ukame, ili kuepukana na adha ya uhaba wa malisho, na hii imesaidia sana,” anasema.
Anasema mpaka sasa wamevifikia vijiji 127 katika wilaya 10 wakizilenga jamii za wafugaji, waokota matunda na warina asali, ikiwa na lengo la kumwezesha mwanamke kiuchumi kupitia vikoba, kuwajengea uwezo wanajamii wanufaike, wakitoa ufadhili kwa vijana kusoma vyuo na umiliki wa ardhi.
Kwa mujibu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), uwezo wa wanawake kumiliki fedha ni mdogo duniani, Kusini mwa Jangwa la Sahara, ni asilimia 37 tu ya wanawake wana akaunti za benki, ikilinganishwa na asilimia 48 ya wanaume, pengo likaongezeka katika miaka kadhaa iliyopita.
Ili kuondokana na adha hiyo na kukuza uchumi wa nchi, shirika hilo linaelekeza kubadilisha sera na kanuni ili ziwe rafiki kwa mwanamke.









