Matatizo yasitumike kama fursa ya utajiri

19May 2023
Joseph Kulangwa
DAR ES SALAAM
Nipashe
Matatizo yasitumike kama fursa ya utajiri

HURUMA ni hali impatayo mtu mwenye roho nzuri, pale aonapo mwenzake anapitia kipindi kigumu cha maisha na hatimaye kutamani amsaidie kuondokana na hali hiyo na hatimaye aishi kama wengine.

Ni kweli, kuwa binadamu hatufanani wala kulingana kimaisha, kutokana na hali ya kipato, lakini pia afya aliyonayo kila mmoja. Ndiyo sababu tofauti ya matajiri na masikini ni jambo lisiloepukika.

Kuna watu duniani ambao wameona watu wakiteseka kimaisha na kuamua kuwasaidia wao moja kwa moja au kupitia watu au taasisi zingine, huku wao wakiweka mazingira ya kukaribisha usaidizi huo.

Vituo vya habari hususan redio na televisheni, vimekuwa mstari wa mbele nchini kutengeneza mazingira ambamo watu wenye matatizo ambao mara zote ni wa hali ya chini kiuchumi husaidiwa.

Kuna vituo kadhaa vya redio ambavyo vimekuwa vikijikita katika hilo na kupata wasikilizaji wengi ambao hujitokeza kusaidia wenye matatizo kama hivyo, ingawa si rahisi kuyamaliza.

Upo mtindo wa vituo hivyo kuigana, pengine ni kutokana na kuwa vingi na kukosa umahiri wa kuandaa vipindi tofauti, hivyo kimoja kusubiri kingine kuja na wazo na mara moja nacho kuiga.

Ni sawa na mtaani, ambako mtu ataanzisha biashara ya vitumbua na mwingine akiona mwenziwe anapata wateja, naye atafungua biashara hiyo hiyo na kujikuta wakigombea wateja hao hao wachache.

Matokeo yake ni biashara kufa kwa kukosa wateja, au wafanyabiashara wenyewe kuoneana inda na wivu na kufanyiana hiyana na kusambaratishana. Hayo ndiyo huwa maisha ya mitaani.

Nimekuwa miongoni mwa wasikilizaji wa vipindi vya kusaidia wenye matatizo, ambapo waandaaji hualika kila mwenye tatizo kufika studio na kuhojiwa chanzo cha matatizo na nini anataka na kisha hutoa namba za simu ili kuomba msaada.

Kweli, kuna wasikilizaji ambao hupiga simu na kuahidi kutoa kitu kwa ajili ya mwombaji, na hatimaye hupewa lakini mara nyingi matatizo huwa hayamaliziki, kwani mengi huwa yanahusiana karibu sana na matatizo ya kiafya.

Kama ijulikanavyo, matatizo ya kiafya ni aghali kuyamaliza, kwa kuwa yanahitaji mchakato wa kuonana na daktari, vipimo na hatimaye tiba ambayo yawezekana isipatikane nchini, na mgonjwa kulazimika kupelekwa nje.

Ni wazo jema sana kusaidia wenye matatizo kwa njia hiyo ya kuwaalika, kuwahoji na hatimaye kuwaunganisha na wasikilizaji ambao miongoni mwao, wenye roho nzuri husaidia kuyatatua.

Ukipata fursa ya kusikiliza baadhi ya wenye matatizo, utatambua jinsi wanavyoishi maisha magumu sana kulingana na wanavyojieleza. Baadhi yao utawasikia wakilalamika kuwa na watoto na kuishi nao mitaani au kwenye mapagala.

Sababu za hali hiyo, utaambiwa ni ama kifo cha mzazi mmoja hususan wa kiume au kutelekezwa na mzazi huyo huyo na kumwacha mama na wanawe wakiishi katika mazingira hayo hatarishi.

Mwingine utamsikia akilalamika kuwa anapoishi ambako ni kwenye pagala, hana kitu chochote cha kula wala kulalia na wanawe wawili au watatu na hata nguo alizovaa ni hizo hizo hana zingine.

Atakuwapo atakayesema chakula anapewa na majirani achilia mbali sasa mgonjwa, ambaye alishazunguka kwa waganga na kuwamaliza, lakini bila nafuu yoyote na kukata tamaa huku akimwachia Mungu maisha yake.

Lakini, jambo ambalo mimi pengine na wengine wanaofuatilia matatizo haya hushangaa, ni pale mwenye matatizo anapoombwa kutaja namba ya simu ili atumiwe msaada, anataja tena namba mbili au zaidi za simu akimaanisha ana simu zaidi ya moja.

Na huyo anakwambia analala kwenye pagala (jumba ambalo halijakamilika ujenzi). Unajiuliza katika pagala hilo, mtu huyu anachaji wapi simu yake/zake! Au mtu huyu ambaye hana pa kula, hana mavazi, hana pa kulala anawezaje kumiliki simu?

Wengine hutumia simu za watu wengine, je, unajiuliza, kuna uhakika gani wa usalama wa fedha hizo zinazotumwa kwa ajili ya msaada huo, hata kama atatumia simu ya kituo cha redio, kuna uhakika wa usalama wa mchango? Je, si mradi wa watu?

Maswali yanakuwa mengi na hasa tukirejea kwenye amri ya Serikali wakati fulani, dhidi ya ombaomba mitaani wakitumia watoto kuwasukuma kwenye vitimwendo na wengine kukaa kando mwa barabara na kutanguliza watoto!

Kama kuna ulazima huo wa kusaidia wanaoishi katika  mazingira magumu, basi Serikali kupitia Wizara yenye dhamana, ijenge vituo vingi vitakavyolea watu wenye matatizo kama hayo wakiwamo watoto, na wananchi wenye uwezo wa kuchangia wakazipeleka huko.

Vinginevyo, matatizo ya watu yataendelea kutumika kama fursa kwa wengine, ili mradi tu wana miundominu ya kuwavuta na kuwatambulisha kwa jamii yenye wasamaria wema walio tayari kujitoa kusaidia. Alamsiki!