Ndani ya tafsiri hiyo, serikali ya awamu ya sita iliyoko madarakani imeipa kipaumbele, ikiiongezea mgao wa bajeti sekta hiyo, kutoka Sh. bilioni 294 za mwaka mmoja kabla, hadi Sh. bilioni 751 iliyoidhinishwa siku chache zilizopita katika mwaka wa fedha 2022/23, sawa na ongezeko la asilimia 158.
Takwimu zinaonyesha umuhimu wa sekta ya kilimo ikiajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania, pia inachangia asilimia 27 kwenye Pato la Taifa (GDP), asilimia 60 ya malighafi na asilimia 25 ya fedha za kigeni.
Hata hivyo, inapiga hatua za maendeleo ya uwezeshwaji kuneemesha uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula, sekta hiyo nchini bado inakabiliwa na vikwazo vinavyodhoofisha maendeleo yake.
Katika orodha hiyo, inatajwa kuwapo ufinyu wa fedha za kuwezesha taasisi na wataalamu wa kilimo kufanya
utafiti wa kina, hivyo serikali imekuwa ikifanya mikakati ya kuongeza ufanisi wa sekta hiyo nchini.
Vilevile ndani ya kilimo kunatajwa kuwapo bajeti rafiki, inayoshuhudia fedha za kibajeti za utafiti, zikiongezeka kutoka Sh bilioni 11.63 hadi Sh. bilioni 40.73, hatua inayotajwa kuiwezesha, ndai ya miaka hiyo miwili ya awamu ya sita, chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Hatua hiyo inatajwa ni muhimu, hata Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk. Geoffrey Mkamilo, anafafanua akisema
imeiwezesha taasisi yake kufanya kazi yenye tija, akitaja mapinduzi ya tafiti za mbegu za mazao, ndani ya miaka miwili hadi sasa.
Dk. Geoffrey Mkamilo, anafafanua: “Dhima ya TARI ni kugundua na kuhimiza matumizi ya teknolojia mbalimbali za kilimo, ili kuongeza tija, uhakika wa chakula na lishe, kuwa na kilimo endelevu na chenye mchango chanya katika ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kushirikiana na wadau wa kilimo wa kitaifa na kimataifa kwa ujumla”.
Kwa mujibu wa Dk. Mkamilo, katika miaka miwili hadi sasa,TARI imeshatafiti na kugundua aina 25 ya mbegu bora za mazao, zilizoidhinishwa kutumiwa na wakulima, akizitaja kuwa mbegu bora zilizoidhinishwa na Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI).
Anaorodhesha kwa ufafanuzi wa idadi na aina zake kwenye mabano ifuatavyo: Mtama (mbili), migomba (nne), viazi vitamu (mbili), miwa (sita),maharagwe (sita), ngano (mbili), choroko (mbili) na aina moja ya mpunga.
Dk. Mkamilo anaeleza kuwa aina hizo ni zinazostahimili ukame na magonjwa, zikiwa na uwezo mkubwa wa kutoa mazao mengi, na anamshukuru Rais kuweka mkazo katika kuisaidia taasisi yao kupanua wigo wa kufanya tafiti za mbegu nchini.
"Kwa mfano, mbegu za ngano tulizozivumbua, zina asilimia 38.9 ya gruneti, protini inayohitajika sana katika viwanda vya uzalishaji, zina uwezo wa kuzalisha kati ya tani nne hadi 4.6 kwa hekta," anaeleza.
Pia, anaongeza kwa mara ya kwanza, TARI imefanikiwa kugundua na kuzalisha mbegu za miwa zenye uwezo wa kuendana na hali ya mvua, hatua muhimu inayotarajiwa kuwasaidia wakulima wadogo kupunguza gharama za uzalishaji, ikilinganishwa na mbegu za awali zinazotegemea ardhi ya maji na umwagiliaji kwa asilimia 100.
"Tafiti zetu zimefanikiwa kugundua nafasi mpya ya kupanda pamba ambayo ni sentimita 60 kwa sentimita 30, hatua muhimu ambayo imechochea ongezeko la mavuno kutoka wastani wa kilo 710 hadi 1,422 kwa ekari," anasema Dk Mkamilo.
Bosi huyo mkuu wa TARI, anasema katika juhudi za kuongeza tija ya uzalishaji pamba nchini, wametafiti na kugundua zana rahisi ya kupanda pamba, yenye uwezo wa kupanda ekari moja kwa saa moja hadi saa tatu,badala ya saa 11 kwa kutumia jembe la mkono.
"Ugunduzi wa mashine hii kwa kiasi kikubwa umepunguza upoteaji wa mbegu kutoka asilimia 15 hadi tano," anafafanua, ikiwa ni zao la mageuzi ya taasisi anayotumikia katika miaka miwili iliyoko ya uongozi kitaifa ulioko madarakani, chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
TEKNOLOJIA MPYA
Vilevile anataja TARI imegundua teknolojia rahisi na rafiki za kuhifadhi nyanya na juisi za miwa kwa zaidi ya miezi miwili, pasipo kupoteza ubora wake, kwa kutumia
viambata asilia tofauti na njia za kawaida, zenye uwezo wa kuhifadhi kwa siku mbili pekee.
"Taasisi imeendelea kutunza vinasaba vipatavyo 33,332 vya mazao mbalimbali ikiwamo mpunga (729), mtama (416), uwele (105), ulezi (3), alizeti (39), zabibu (26), migomba (128), maharagwe (10), muhogo (20), korosho (30,000), pamba (328), mahindi (250), viazi vitamu (6), miwa (107), minazi (7), michikichi (3), mkonge (60), na kakao 17, kwa lengo la kuzuia upotevu wa vizazi hivyo na kuwa na utafiti endelevu," anaeleza.
Pia, katika kipindi hicho cha miaka miwili, Dk. Mkamilo anasema TARI imeongeza uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 481,23 mwaka wa fedha 2020/21, hadi kufikia tani 1,225.872 mwaka 2021/2022.
Hapo anaainisha mkakati wa kuzalisha miche, vikonyo na pingili ulioongezeka kutoka 7,998, 784 kwa mwaka 2021/22 hadi 19,822,349 kwa mwaka 2023, yakihusisha mazao ya parachichi,michikichi, mihogo, miwa, viazi mviringo, korosho, matunda na viungo.
" Kwa upande wa usambazaji wa teknolojia bora za kilimo, tumefanikiwa kuzindua vituo mahiri vinne vya kusambaza teknolojia kwa wakulima, ikijumuisha kituo cha Nyakabindi (Simiyu), Nzuguni (Dodoma), Fatma
Mwasa ( Tabora) pamoja na kituo cha Mwalimu Julius Nyerere Morogoro," anaeleza.
UHAKIKI MABADILIKO
Katika kuhakikisha matokeo ya utafiti yanaleta mabadiliko chanya kwenye sekta kilimo nchini, Dk. Mkamilo anasema, taasisi yao imepeleka matokeo ya utafiti mbalimbali kwa wadau 5,497,547 wakiwamo wakulima na maofisa ugani.
"Njia zilizotumika kusambaza teknolojia hizo ni pamoja na maonyesho ya wakulima, siku za wakulima, maonyesho ya kilimo biashara, mafunzo wezeshi, majukwaa bunifu na mashamba darasa," anaeleza.
Pia, moja na njia hizo, amesema pia wamekuwa wakitumia vyombo mbalimbali vya habari, ikiwemo redio, magazeti, televisheni na mitandao ya kijamii katika kuwaelimisha wakulima juu ya matumizi sahihi ya teknolojia hizo zinazolenga kuongeza uzalishaji na tija katika uzalishaji mazao ya kilimo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa TARI, taasisi inaendelea kuongeza uzalishaji na upatikanaji mbegu bora nchini, wakiboresha mahitaji ya utafiti na uzalishaji na kwa miaka miwili hadi sasa, ameshaandaa ujenzi wa miundombinu ya kumwagilia hekta 854 zinazopatikana kwenye vituo 16 vya utafiti nchini.
Kwa mujibu wa Dk. Mkamilo, kukamilika ujenzi wa miundombinu hiyo utawezesha uzalishaji wa mbegu na majaribio ya utafiti kufanyika mwaka mzima.
"Tupo pia katika hatua nzuri ya ujenzi wa maghala matano ya kuhifadhi mbegu yenye vyumba vya ubaridi katika vituo vya TARI Naliendele, TARI Tumbi, TARI Hombolo, TARI Selian na TARI Dakawa, mradi ambao
utekelezaji wake umefikia asilimia 10," Dk. Mkamilo anaeleza.
Pia, anasema TARI imeanza kukamilisha taratibu za kuwezesha upatikanaji wa ithibati ya maabara ya udongo iliyopo katika kituo chake cha Mlingano Tanga, akifafanua:
"Kwa sasa hatua iliyofikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa na vitendanishi vya maabara na kufanya tathmini ya uwezo na ubora wa maabara hiyo, mchakato ambao umefikia asilimia 40,"
Anasema kuna ukarabati wa maabara nyinginezo katika vituo vya Tengeru, Mikocheni na Mlinganom, mahsusi kwa uzalishaji wa miche kwa njia ya chupa, utambuzi wa magonjwa na wadudu, kupima mbegu na kutathmini afya ya udongo.
TARI ILIKOTOKA
TARI, iliyoanzishwa kisheria mwaka 2016, inatekeleza majukumu yake kupitia mtandao wa vituo 17 vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Vituo hivyo vya TARI ni Naliendele (Mtwara), Uyole (Mbeya), Ukiligulu (Mwanza), Kihinga (Kigoma), Mlingano (Tanga), Kibaha (Pwani), Mikocheni (Dar es Salaam), Maruku (Kagera), Kifyulilo (Iringa), Ilonga (Ifakara), Dakawa (Morogoro), Selian (Tengeru), Tumbi (Tabora) pia Makutupora na Hombolo (Dodoma).