KUKITHIRI UVUVI MABOMU…

16Mar 2023
Jenifer Gilla
DAR ES SALAAM
Nipashe
KUKITHIRI UVUVI MABOMU…
  • Wavuvi Pwani watoa siri nyuma ya pazia hujuma zao baharani

MAJIRA ya saa mbili na robo usiku, Simbaeli Mudy (si jina lake kamili) mkazi wa Pemba Mnazi, Manispaa ya Kigamboni, Dar es Salaam, anasogea pembezoni mwa ukuta wa nyumba yake kuchungulia upande wa kulia kuangalia kama kuna mtu anayekuja, akijihakikishia usalama, kisha anaendelea na achokifanya.

Simbaeli anaingia stoo ya nyumba yake, anatoa chupa yenye mafuta ya petroli ujazo lita tano, yaliyochanganywa na unga kidogo wa mbolea ya urea, utambi na kibiriti, akiwa na wenzake tisa, wanaelekea ufukweni kupanda boti kwa safari ya uvuvi.

Alichokibeba Simbaeli, ni bomu ambalo yeye na wavuvi wenzake wamelitengeneza, ili kulitumia katika uvuvi, lengo ni kupata samaki wengi, jambo ambalo ni kinyume na sheria ya nchi.

Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003, inapiga marufuku uvuvi wa mabomu, ambayo adhabu zake ni faini isiyopungua Sh.200, 000 na isiyozidi Sh. milioni 15 au kwenda jela kati ya miaka miwili hadi 10.Nipashe inabaini uvuvi haramu katika mwalo wa Buyuni umekithiri na hufanyika katikati ya bahari majira ya usiku wa kuanzia saa saba hadi tisa, umma ukiwa usingizini.

Mvuvi Alphonce Joseph, anasema baada ya kulipuliwa mabomu katika miamba, wanapata samaki wengi, hata kuna wakati maboti hayatoshi kubeba samaki wote waliowapata, wanawaacha wengine wakielea majini.“Sasa inategemea na wingi wa samaki unaotaka kuupata, kama unataka samaki wengi unatumia dumu la maji la lita tano, kama ni kidogo tunatumia chupa za lita mbili au lita moja na ule unga wa baruti ndio unasaidia kuleta mlipuko mkubwa,” anasema. 

Mtaalamu wa viumbe bahari, Jerry Mang’ena, anasema watu wengi wanajikuta wanakula samaki aliyevuliwa kwa kutomjua. Anafafanua namna ya kumtambua, anapobonyezea, eneo lililobonyezwa huwa halirudi haraka.

Pia, macho yake yanakuwa yamevilia damu, sehemu ya haja inakuwa wazi, kwa sababu mishipa iko wazi choo chake kinatoka chenyewe.

HOJA ZA KITAALAMU

Mtafiti wa viumbe bahari kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Prof. Philip Bwathondi, anasema uzoefu wa muda mrefu, unambainishia uvuvi wa mabomu ndio unaoongoza nchini, ukifuatiwa na  nyavu za plastiki, sababu kuu ni umasikini na kukosa elimu ya madhara yake.

“Kutokana na shughuli zao wavuvi, hawatakiwi kuwa na maisha magumu, lakini takribani asilimia 85 ya wavuvi wana hali ngumu. Bidhaa wanazovuna, wanaziuza kwa bei nafuu sana, huku madalali wakitajirika. Hiyo nayo inawasukuma kuingia kwenye biashara hiyo, ili kupata faida ya haraka,” anasema Prof. Bwathondi.

Mvuvi Deus James, anasema wanakopata vifaa vya kutengeneza mabomu ya ama petroli au mafuta ya taa, huuziwa  na wauzaji mafuta, huku utambi na unga unaotumika kulipua, wananunua kwa wachimba madini wanaopasulia mawe makubwa.

Mchimbaji madini kutoka Shinyanga, Remsi Chonzi, anakiri kuwapo biashara hiyo, kati ya wachimba madini na wavuvi, ingawa ana hoja, kuhusu unga wa baruti.

“Unga wanaouziwa wavuvi ni ule unaoletwa na watu wa mataifa ya Ulaya wanaokuja migodini kununua madini. Wenyewe unafanana na mbolea ya ‘urea’ huwa tunawauzia kwa kupima kipimo kinaanzia Sh. 30, 000 hadi Sh. 40,000 pamoja na utambi wake wa kulipulia Sh. 10,000,” anafafanua.

Mang’ena, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Aquafarm, anasema uvuvi wa mabomu unachangia uhaba wa samaki, kwa sababu wanakimbilia kwenye kina kirefu cha maji.

Anautaja ni aina ya uvuvi unaoathiri sana mazalia ya samaki, yakiwamo matumbawe na mapango, ambayo samaki hupendelea kutaga na kuhifadhi mayai yao, kwa utulivu uliopo.

MIKASA NA MADHARA

Jumanne Shija (35), anasimulia mkasa wa uliompatia ulemavu mwaka 2015, baada ya kukatika kiganja cha mkono wake wa kulia, huku wenzake wanne wakifariki, alipokuwa anavua samaki akitumia bomu, hata akaacha kazi hiyo.

“Mabomu yanakuwa na utambi mfupi, kwa hiyo unapoliwasha tu unatakiwa ulitupe hapo hapo. Sasa mwenzangu alichelewa kulirusha, kwa hiyo alipoliachia likatuvuta na kututupa kwenye maji, mimi hapa nimekatika mkono na mwili wangu wote una makovu,” anasimulia. 

Mwenyekiti wa BMU, Pemba Mnazi, Rajabu Mkalapema, anasema kila baada ya miezi mitatu wanapokea taarifa za kifo wastani wavuvi wawili kutokana na uvuvi haramu, taarifa inayofika kutoka kwa ndugu, wahusika wakihofu kujulikana.

Magdalena Chalila, mvuvi wa Mwaloni Pemba Mnazi, anasema uvuvi haramu umewaathiri wanawake wavuvi, kwa sababu samaki wote wamekimbilia kwenye kina kirefu cha maji.“Wanawake wengi wanavua kwenye kina kifupi cha maji, kwa kuwa hawana utaalamu wa kuogelea kwenye kina kirefu…” anasimulia na kuendelea: “…kwa sababu jua limekuwa kali na nyumba zao zimebomolewa na mabomu.”

Bingwa kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk. Emmanuel Lugina, anaainisha mlaji samaki aliyepigwa na bomu, yupo hatarini kupatwa na saratani. 

“Sasa ukiangalia mabomu ya mlipuko yanayotumika kuvua samaki, utagundua dhahiri yametengenezwa kwa kemikali mbalimbali ambazo zimehusishwa na saratani (organic amines, hydrocarbons na inorganic chemicals).

“Binadamu pia anaweza kupata madhara kwa kunywa maji au kula chakula kilichokuwa na vimelea vya kemikali zilizoko kwenye mabomu hayo,” anafafanua Dk.LuginaShirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO) linatahadharisha uvuvi haramu usioripotiwa na usiodhibitiwa, husababisha kupotea tani milioni 11 hadi 26 za samaki kila mwaka.

VITA ILIVYO

Mwenyekiti wa Kambi ya Wavuvi Muruani Pemba Mnazi, Kigamboni, Amadi Ali, anasema wanakabiliana na shughuli hizo kwa kuweka doria na kutoa taarifa polisi, wanapobaini matendo hayo.

“Tunapobaini kuna wavuvi wanavua kinyume na utaratibu, tunatoa taarifa kwa maofisa uvuvi wanaoshirikiana na kikosi cha polisi maji na wanaweka doria kuwakamata,” anasema.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Wanamaji Tanzania Kamishna Msaidizi, Moshi Sokoro, anasema kuna vikwazo katika kudhibiti uvuvi haramu, ikiwamo kuvujishwa taarifa za doria, hali inayokwamisha utendaji wao, katika kukabili uvuvi haramu na vifaa vyake.

Ofisa Uvuvi Kata ya Pemba Mnazi, Rahimu Said, anakiri madhila katika fukwe anazozisimamia na wanaendelea kushirikiana na viongozi wa mazingira ya usafi wa fukwe (BMU), kukabiliana nayo kupunguza mikasa na kesi, kutoka 20 mwaka 2018 hadi kesi mbili mwaka jana.

Anataja njia wanazotumia, ni doria na utaratibu maalumu wa kumtambua mgeni anayeingia mahali hapo, kwa ajili ya shughuli za uvuvi.