Dk. Mpango na Waziri Mwigulu walivyotoa ushuhuda kikaoni Doha makubwa

17Mar 2023
Jenifer Gilla
DAR ES SALAAM
Nipashe
Dk. Mpango na Waziri Mwigulu walivyotoa ushuhuda kikaoni Doha makubwa

NI keshokutwa Dk. Samia Suluhu Hassan, anatimiza miaka miwili ya urais. Ikiangaliwa, je katimiza yapi na ana mwelekeo upi katika kuongoza Watanzania?

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, akiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, walipokuwa kikaoni, jijini Doha Qatar, siku chache zilizopita. PICHA: MPIGAPICHA WETU.

Nyuma yake ana safu kamili  ya kuchapa kazi, msaidizi mkuu wa kwanza, ni Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango, ambaye hadi wiki moja iliyopita, alikuwa jijini Doha, nchini Quatar, akimwakilisha rais katika Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi zinaoendelea za Kipato cha Chini (UNLDC5). 

Hiyo ilikuwa kati ya tarehe nne na tisa mwezi huu, nchi 46 duniani zilikutana kujadili watavyokomboa nchi zao na janga hilo, mjadala kuzama katika Mpango wa Utendaji wa Doha (DPoA).

Kimsingi, unaowekewa mkazo mambo matano, ikiwamo elimu ya chuo kikuu kutolewa kwa mtandao, ili kukuza ubora wake na kujengewa uwezo wa kuboresha usalama wa chakula na ushirikiano na nchi zinazoendelea katika kuleta maendeleo.

Mengine, ni kuwapo kituo cha msaada wa kuongeza uwezo wa kustahimili athari za mabadiliko ya hali ya hewa, kupitia kurekebisha na kuboresha mfumo wa tahadhari kama vile kujengwa madaraja, kuta za kuzuia maji ya bahari na kuvamia makazi na kuboresha miundombinu ya barabara.Ni mpango unaotarajiwa utazisaidia nchi kukabiliana na vikwazo vinavyorudisha nyuma maendeleo yao, ikiwamo kukosa kutoa elimu bora na usaidizi wa kuhitimu katika kundi la nchi zenye kipato cha chini, kukabiliana na usalama wa chakula na mfumuko wa bei za vyakula na msaada katika uwekezaji.

 

MIKAKATI YA TANZANIA

Tanzania nayo iliwasilisha mkutanoni hapo, mikakati yake kuboresha teknolojia, ili itumike kukuza uchumi wa nchi na taifa kujikwamua kutoka katika umasikini. 

Kimsingi, unalenga kuzishinikiza nchi zilizoendelea zitoe msaada wa hali na mali, hata kujiletea teknolojia ya kisasa itakayotumika kukuza uchumi kwa njia ya ushirikiano. 

Akiwasilisha mada mkutanoni, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema Tanzania inakaribisha ushirikiano wa kuhamisha teknolojia ili kujiongezea uwezo wa nyenzo za maeneo mbalimbali, ikiwamo upatikanaji wa chanjo.

Anasema ni teknolojia anayoitegemea kuiunganisha Tanzania na watu bilioni tano duniani kote mtandaoni, huku watu bilioni mbili wanaotumia biashara ya mtandaoni wakifikiwa na asilimia 60 ya Pato la Taifa, linalopitia njia za kidigitali. 

Hivyo, anaeleza nchi imedhamiria kupunguza umasikini na kukuza uchumi ambao mpaka mwaka jana umerekodiwa kukua kwa asilimia tano kwa mwaka, baada ya kusuasua hadi asilimia 4.8 mwaka 2020, ilhali  kabla ilikuwa asilimia 6.7 kabla ya janga la Uviko -19. 

Anataja maeneo wanayochangia kukua uchumi, inajumuisha nidhamu, sera rafiki ya fedha, mageuzi endelevu ya kitaasisi na udhibiti wake, pamoja na kuchukua hatua kukabili misukosuko ya kiuchumi, kwa kushirikisha wazawa. 

Mengine anaorodhesha ni kugatua mfumo wa afya, ushirikiano wa kimkakati, utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Usambazaji wa Chanjo ya COVID-19 na Mpango wa Majibu ya Kijamii, ikiendana na majadiliano ya kusamehewa au kusimamishwa kwa madeni.

Kwa kipekee, Waziri Dk. Nchemba, anataja kampeni ya filamu ‘Royal Tour’ imekuwa na nafasi yake katika mapinduzi ya sekta utalii.

Anasema Mpango wa Utendaji wa Doha (DpoA), unaonyesha matumaini kwa nchi kuondakana na umasikini,unaosababishwa na changamoto kama za mikopo mikubwa, mfumuko wa bei za chakula duniani na kuongezeka gharama kwenye miradi ya maendeleo. 

Akifafanua hoja hizo, Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango, anasema Tanzania imeweka kipaumbele kuwekeza  katika maeneo muhimu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwamo nishati ya jua na upepo, usimamizi bora wa taka na teknolojia rafiki kwa mazingira. 

Dk. Mpango anasema hadi sasa nchi inashuhudia athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, ikiwamo matukio makubwa kama ya ukame na mafuriko, mvua zisizotabirika, kupanda kina cha bahari na baadhi ya visiwa kuzama, vyote vikisababisha uhaba wa chakula, migogoro ya kijamii na kupanda gharama za maisha, hata kudororesha uchumi 

Anaongeza  kuwa, Tanzania inakadiriwa kuwa na hasara ya kiuchumi kufika Dola za Marekani milioni 33.7 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kutokana na mafuriko. 

Makamu wa Rais anasema, serikali inachukua hatua, zikiwamo  kuchimba mabwawa ya maji, kuhamasisha nishati safi ya kupikia, kupanda miti kila mkoa, kujenga kingo ufukweni mwa bahari kudhibiti mmomonyoko wa udongo, kuandaa mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na Mpango Kabambe wa Mazingira wa mwaka 2022 hadi 2032. 

Anasema pamoja ya kuwa katika kundi la nchi masikini zenye kipato cha chini, uchumi wa Tanzania unaendelea kukua licha ya kuptiwa na janga la UVIKO-19 na vita vya Ukraine na Russia, ikitumia mikakati wa kikanda, kiserikali na kimataifa na kuongeza ufadhili wa kiuchumi wa masharti nafuu inayoisaidia kupiga hatua za kimaendeleo.

“Tanzania imepiga hatua kubwa tangu mkutano wa Nne wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinaoendelea za Kipato cha Chini (LDC4, uliofanyika miaka 11 iliyopita. Uchumi wetu unasalia kuwa thabiti wenye mwelekeo mzuri…,” anatamka Dk. Mpango, ambaye kitaaluma, ni mchumi.