Hayo ni madini yanayotumika kutengeneza penseli, huku kielektroniki inaelezwa inasaidia kupitisha joto na umeme, mfano kwenye betri na paneli ya sola, hivyo inachangia kuunda nyenzo za kielektroniki.
Mkurugenzi Mkazi wa kampuni Magnis Energy Tanzania, Peter Tsegas, anaiambia Nipashe kwamba ushirikiano wao na kampuni tanzu, Uranex, zote za Australia zimeshakamilisha kulipa fidia wananchi 1,140, watakaoupisha mradi huo, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Mkurugenzi Peter, ambaye pia ni Mwendeshaji Mkuu wa mradi, anasema kampuni kwa sasa inamiliki eneo la kilomita za mraba 30 zenye kiasi kikubwa cha madini bora, baada ya utafiti uliokuwapo tangu mwaka 2013.
Kwa mujibu wa bosi huyo wa mradi ulioko Nachu, inakadiriwa kuzalisha kwa miaka 16, lakini tafiti zaidi zinaonyesha uwezekano kufika miaka 40, kila mwaka kuzalishwa tani 230,000 za grafaiti.
FIDIA ZILIVYOENDA
Anafafanua kwamba wananchi watakaolipwa fidia ni walioathiriwa na mradi kabla mshauri huru alipotumika kuhakiki madai, kwa kuzingatia viwango vya kimataifa (IFCPS) kama vilivyoainishwa na Benki ya Dunia (WB).
Peter anaeleza, Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali ilishirikishwa kuhakikisha haki ya fidia ya ardhi na hatua ya kwanza walitakiwa kuhamisha makazi yao.
“Jumla ya nyumba 59 zimejengwa ndani ya viwanja 56 ambavyo vilinunuliwa na Uranex, zilikabidhiwa kwa ajili ya kuwahamishia wananchi, kutokana na kwamba eneo lilikuwa pori wenye makazi ya kudumu walikuwa wachache,” anabainisha.
Vilevile anasema, eneo la mradi lilikuwa na nyumba 59, akidokeza hatua inayofuata ni kujengea wakazi huduma za kijamii kama za afya na soko.
MANUFAA YA MRADI
Kwenye manufaa ya kiuchumi, mkuu huyo wa mradi anasema utakuwa na manufaa kutokana na kwamba, ni malighafi muhimu yanayogusa utengenezaji bidhaa kama betri za magari na umeme.
“Dunia ya sasa iko kwenye magari ya umeme katika kuhakikisha matumizi ya teknolojia safi ambayo haiharibu mazingira,” anasisitiza.
Pia, anafafanua utekelezaji wa mradi huo una sura ya manufaa kiuchumi, kwa kushuka chini kwa jamii zinazozunguka mradi na nchi kwa ujumla, kupitia mahitaji ya bidhaa na huduma zinazotolewa na kampuni za ki-Tanzania na wazalishaji wengine wa Ruangwa.
Mkurugenzi huyo anasema, ni takriban miaka 10 tangu mradi huo wa madini uanze na kuna maendeleo kwa wakazi tangu zama za utafiti, mara baada ya kupatikana leseni.
“Sasa tuko kwenye hatua ya ujenzi wa awali ambao umeshaanza,” anasema.
HALI YA AJIRA
Mkurugenzi Peter anafafanua, anasema kipaumbele kilichopo ni kwa wananchi, kupata mafunzo ya kilimo, ufundi vyuma, magari, lengo ni kuwainua kiuchumi.
Anasema, umeelekezwa kuboresha huduma za jamii kwa maendeleo endelevu ya mradi na wanauona ustawi wa wilaya hiyo, akitoa mfano mradi ulipoanza walilazimika kuagiza bidhaa kama nyama, kuku, matunda na mboga kutoka Dar es Salaam, lakini sasa zinazalishwa na wananchi, jambo wanalojivunia.
ATHARI MAZINGIRA
Mkurugenzi huyo anasema, wamejipanga kuhakikisha wanatumia nishati safi, ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na wako katika mazungumzo na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika hatua pana zaidi.
Anataja eneo la kufungwa bomba lenye urefu kilomita 90, kusafirisha gesi asilia kutoka Mingoyo kwa ajili ya uzalishaji na kupunguza matumizi ya nishati chafu kama mafuta ya dizeli.
Anasema, pia magari yao yanatumia injini ya gesi asilia kupunguza gesi ukaa kwenye mazingira yao, akinena kuwa uchakataji madini ya grafaiti hauhitaji kemikali zenye sumu kama zilivyo aina nyingine za madini.
“Tujitahidi kadri ya uwezo wetu kupunguza kusambaa kwa vumbi katika eneo la mradi tuna kifungu cha kufunga uzalishaji madini, ambacho kinatutaka kurejesha mazingira ya eneo la mradi katika hali yake ya awali, mara shughuli za mradi zitakapofikia mwisho wake,” anasema.
KUISAIDIA JAMII
Peter anasema mradi haujaanza rasmi, ila ukianza wana matarajio wenyeji watanufaika sana na huduma za elimu na afya kwa watoto wao, ikijumuisha kukarabatiwa shule na zahanati.
Pia anasema, hadi sasa wameshagawa vitabu vya sayansi kwa shule za sekondari na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali, ikiwamo maadhimisho ya Siku ya Wanawake wilayani humo.
Ni aina ya mjumuiko na ushiriki wakutumia bajeti Sh.milioni 250 kwa shughuli za kijamii, lengo ni kuhakikisha wenyeji wananufaika na shule tajwa.
CHANGAMOTO IKOJE?
Mkurugenzi huyo anasema, changamoto zilizopo ni upatikanaji mtaji wa kuendeleza stahiki kutokana na sababu mbalimbali, huku miradi ya bidhaa za grafaiti duniani, zikiwa kwenye ushindani mkubwa wa soko.
Anataja shida nyingine ni ubovu wa miundombinu, ambayo utatuzi wake uko kwenye kushirikiana na serikali kufikia maboresho yake.










