KIMBUNGA KINATIKISA MSUMBIJI…

16Mar 2023
Beatrice Philemon
MSUMBIJI
Nipashe
KIMBUNGA KINATIKISA MSUMBIJI…
  • Wataalamu watoa elimu madhara tabianchi; maradhi, utapiamlo…

INAPOZUNGUMZIWA dhana mabadiliko ya tabianchi, si watu wote wanaoifahamu vyema. Kwa miaka ya  karibuni, imebainika mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa majanga duniani, yanayoashiria uwezekano wa madhara makubwa kwa afya ya binadamu na ustawi wa jamii.

Hapo kunatajwa kugusa mifumo ya kijamii, kiuchumi,  mazingira na maliasili, kama vile hewa safi, majisafi ya kunywa, usalama wa chakula na malazi.

Mfano ni hivi sasa inajionyesha hali ya kusambaa Kimbunga Fredy nchini Msumbiji na Malawi, ikiendelea  kusambaza madhara hayo kwa wananchi kwa hali na mali zao.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linataja kati ya mwaka 2030 na 2050, kuna mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha takribani vifo 250,000 kila mwaka, kutokana na utapiamlo, malaria, kuhara na changamoto za joto kali.

Hivyo WHO inataja gharama za uharibifu wa moja kwa moja kwa afya, yaani pasipo kujumuisha gharama za sekta zinazohusiana na afya kama vile kilimo, maji na mazingira, kukikadiriwa thamani  kuanzia Dola za Marekani bilioni mbili hadi nne kwa mwaka, ifikapo mwaka 2030.

Aidha, maeneo yenye miundombinu dhaifu ya afya hasa katika nchi zinazoendelea, yatakuwa na uwezo mdogo kuhimili mabadiliko ya tabianchi, ikiwa hakutakuwapo msaada wa kujiandaa na kukabiliana na changamoto hizo kwa wakati.

Kuhusu jitihada na mikakati inayotakiwa kufanyika, kuifanya sekta na mfumo wa afya nchini kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi, Mratibu wa Mradi kutoka Jukwaa la Mabadiliko ya Tabianchi (FORUMCC), Msololo Onditi, anasema Tanzania kama yalivyo mataifa mengine duniani, imeshuhudia athari za mabadiliko ya tabianchi kwa afya ya binadamu na jamii kwa ujumla.

Anasema, dalili zinaonyesha kuwa madhara yanaweza kuongezeka siku zijazo, akitumia kauli:“ Uhusiano uliopo kati ya usalama wa raia, afya ya jamii na mipango kazi ya pamoja, vinaonyesha kuna haja ya kukabiliana na madhara yanayoibuka kiafya, yakisababishwa au kuchangiwa na mabadiliko ya tabianchi, hususani upotevu na uharibifu.”

Onditi anaendelea: “Mabadiliko ya tabianchi huathiri mfumo wa uzalishaji chakula, hewa tunayotumia kupumua, maji tunayokunywa na mazingira, kwa maliasili hupatikana na kutupatia mahitaji muhimu.”

Kwa Watanzania wengi, anataja mabadiliko ya tabianchi huathiri ustawi na afya zao, ama kubadilika au kuongezeka ukali na kujirudia kwa madhara ya kiafya ambayo tayari jamii imekuwa ikikumbana nayo.

Pia, anasema huja na madhara ya kiafya yasiyotarajiwa kwa watu, kwa kiwango  kisochowahi  kutokea huko nyuma

NINI KIFANYIKE?

Mtaalamu Onditi anaendelea: “Tukiwa wadau muhimu katika jitihada za kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi nchini, tunapendekeza wadau kama vile vyuo vikuu na taasisi nyingine za utafiti kufanya utafiti kuhusu athari za kiafya zitokanazo na matukio yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.”

Hapa ana ushauri kwamba, ni vyema kukafanyika utafiti kwa sababu kunapotokea ukame, wajawazito huathirika zaidi, hata kupata watoto wenye mapungufu kiafya, hata wanaokosa lishe kwa ukosefu wa vyakula.

Ni utafiti unaoelezwa utasaidia kujua ukubwa wa tatizo, maeneo, sekta au makundi ya watu katika jamii yaliyoathiriwa zaidi, au yaliyopo hatarini kuathiriwa na mabadiliko tabianchi.

Eneo lingine analitaja ni aina ya jitihada zinazotakiwa kuchukuliwa kukabili athari hizo na kutoa mwanga kwa watunga sera, wafanya maamuzi, wabia wa maendeleo na wadau wengine, kufahamu maeneo yanayohitaji ushirikiano zaidi, sambamba na asasi za kiraia.

 Tunaomba kulindwa, kuhifadhi na kurejesha mifumo ikolojia iliyoathirika au kuharibiwa ili kuimarisha hifadhi za kaboni na kupunguza hatari za mafuriko, joto kali na dhoruba ikiwemo kuunda na kutekeleza mfumo wa tahadhari ya mapema inayozingatia athari na hatari za mabadiliko ya tabianchi,” anasema.

ATHARI ZA MAFURIKO

Ofisa Mradi wa Jukwaa la Mabadiliko ya Tabianchi, Gladness Lauwo, anashauri ni muhimu kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kwa sababu mafuriko yanapotokea, husababisha kusambaa maji machafu na majitaka, maji ya kunywa kilimo, kusambaziwa kemikali, viambato vya dawa na vimelea vya magonjwa.

Lauwo anafafanua:“Mafuriko huzorotesha jitihada na hali ya usafi na kuharibu vituo vya afya. Makazi, miundo mbinu ya uhifadhi na usambazaji wa maji, mvua kubwa na mafuriko yanapopungua hutengeneza mazingira wezeshi ya kuzaliana vimelea vya magonjwa katika maeneo ambayo maji yanatuama kwa muda mrefu.”

Pia, anataja afya ya uzazi na watoto kama vile kuzaliwa kabla ya wakati, vifo vya mama na mtoto na kuharibika kwa utendaji wa kijamii.

Ofisa huyo anaeleza, iwe mafuriko, ukame au kiangazi cha muda mrefu, daima huongeza uwezekano wa mtoto kupata utapiamlo na matokeo yake ya muda mrefu ni kudumaa, inayoleta athari kubwa kiafya kuanzia akili na ukuaji kimwili watoto.

Pia anataja kukithiri athari hizo kunaweza kuongezea jamii mikasa ya mfadhaiko, wasiwasi, msongo wa mawazo, matatizo ya kitabia na kiakili.

Inaelezwa, mabadiliko ya tabianchi yanaathiri makundi ya kijamii kwa viwango tofauti, kulingana na uwezo wao kuhimili hali ya kiuchumi, jamii, ufahamu na maarifa na tofauti za kijiografia.

 

TANZANIA IKOJE?

Lauwo anaelezea: “Tukiangalia uwezekano wa kuathiriwa kuna watu au makundi ya watu katika jamii ambao wanaathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi kuliko watu wengine kulingana na hali za kiafya na umri.

“Kwa mantiki hii makundi ya watu wenye magonjwa sugu na wenye kinga dhaifu ya mwili, watoto, wazee na wanawake wajawazito ni miongoni mwa makundi katika jamii ambayo yapo hatarini zaidi kuathiriwa kiafya na mabadiliko ya tabianchi.”

 

Top of Form

Bottom of Form

Top of Form

Bottom of Form