Wapo ambao wanalazimika kuishia njiani na kufanya michezo na ikifika muda wa kurudi nyumbani wanarejea na wazazi au walezi wanaamini walikuwa masomoni.
Kwa wazazi na walezi wenye majukumu mengi au wagonjwa wasioweza kufuatilia na kukagua za wanafunzi wanaamini watoto wao walikuwa shuleni jambo ambalo ni tofauti hata baadaye akipewa taarifa kutoka shule na wanajamii wengine wanakuwa wagumu kuamini kwa kuwa kila siku watoto hao wanaaga wakielekea shuleni.
Shule kuwa mbali na makazi pia imekuwa ikiathiri wanafunzi wa kike ambao baadhi yao wamekuwa wakijiingiza kwenye zawadi za lifti za pikipiki na magari zinazozalisha mimba na kuwakatishia masomo.
Hali hiyo kwa sasa ni tofauti katika baadhi ya maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ambayo imeanza kutatua kero hizo kwa kujenga shule maeneo yaliyokuwa na kero kama hizo.
Kibaha ni moja kati ya halmashauri tisa zinazounda mkoa wa Pwani ikiwa na kata 14, vijiji 26, vitongoji 102 na kaya 33,352 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka mwaka 2022.
Katika kata 14 ni sita pekee zilikuwa na shule za sekondari hivyo kufanya baadhi ya maeneo watoto kutembea umbali mrefu kufuata elimu kwa majirani.
Akizungumza na Nipashe Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Butamo Ndalahwa, anasema wapo wanafunzi ambao ufaulu wao ulikuwa unashuka kutokana na umbali wa shule na wakifika wanakuwa wamechoka huku wengine wakikatisha masomo.
Yote, yalirudisha nyuma kiwango cha ufaulu kwa halmashauri hiyo lakini pia kudumaza maendeleo kwa kuwa na vijana wachache wanaofikia na kuhitimu masomo.
“Kutokana na baadhi ya watoto kuwa na umri mdogo walishindwa kutembea umbali mrefu na kuchoka waliacha shule na kwenda kuchunga ng’ombe…” anaeleza.
Kwa mujibu wa Ndalahwa halmashauri ilipeleka fedha zilizotokana na mapato ya ndani kujenga vyumba vya madarasa, akitaja Sekondari ya Kawawa ambayo ipo pembezoni, iliyoanza kupokea wanafunzi.
Kadhalika, anataja juhudi za wananchi za kuanzisha ujenzi wa Sekondari ya Kawawa, ili kuwaondolea wanafunzi adha ya umbali mrefu kufuata shule ziliungwa mkono na serikali kuu iliyotoa fedha za kujenga vyumba vitano vya madarasa na matundu matano ya vyoo.
Mkurugenzi huyo anaendelea kueleza kuwa mbali ya umbali wa shule pia zipo ambazo zilikabiliwa na msongamano wa wanafunzi hali ambayo ilisababisha kushuka kwa ufaulu.
Anaeleza kuwa Shule ya Sekondari Disunyala ni kati ya mpya zilizoanzishwa kuondoa tatizo la msongamano kwenye shule nyingine na kwamba Shilingi milioni 112.5 zilitolewa kujenga vyumba vya madarasa vitano na matundu ya vyoo.
Awali shule hiyo ilipokea Shilingi milioni 100 fedha za UVIKO- 19, kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa matano na kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023.
Shule hiyo ambayo iliyoanzishwa katika kata ya Kilangalanga ilikuwa na lengo la kupunguza msongamano tayari imepokea vyumba 10 vya madarasa na matundu ya vyoo ndani ya miaka miwili yanayohitajika na wanafunzi.
Katika hatua nyingine, Ofisa Elimu Sekondari, Fatuma Kisalazo anabainisha kuwa halmashauri hiyo ilipokea Shilingi milioni 940 kwa ajili ya ujenzi wa sekondari mpya mbili kupitia mradi wa kuinua Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
Anasema ujenzi huo umetekelezwa katika kata mbili za Gwata na Kikongo kwa kujenga vyumba nane vya madarasa, matundu 20 ya vyoo, maabara ya kemia, biolojia na fizikia, jengo la utawala, maktaba, tangi la maji la chini.
Fatuma anasema katika utekelezaji wa mradi huo kwa shule zote mbili, yapo majengo ambayo yamekamilika kwa asilimia 100, ikiwamo vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na mengine yapo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.
Halmashauri hiyo imetoa Shilingi milioni 172.9 zinazotokana na mapato ya ndani kwa ajili ya kuendeleza ujenzi na utengenezaji wa madawati na kwamba kila shule imepokea milioni 86.4.
“Sekondari hizi zimepokea wanafunzi 210 wa kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2023 na wanaendelea na masomo ujenzi wa shule hizi umepunguza vikwazo walivyokuwa wanakabiliana navyo vya kutembea umbali mrefu,” anaeleza.
Aidha katika Kata ya Boko Mnemela ambayo haikuwa na sekondari na kusababisha wanafunzi wa maeneo hayo kutembea umbali mrefu hadi katika kata ya Soga wananchi walishirikiana na kuanzisha shule mpya ya Boko Mnemela kwa kuanza kujenga vyumba vya madarasa vitatu.
Fatuma anasema baada ya jitihada za wananchi serikali imetenga milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne katika shule hiyo na Januari 2023 ilipokea wanafunzi 125.
Anasema shule shikizi zimeanzishwa kwenye kata ambazo wanafunzi wanatembea umbali mrefu ikiwamo Shule ya Msingi Masaki ambayo ipo kata ya Magindu, ambapo wanafunzi walikuwa wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa 10 huku wengine wakikwama kutokana na umri kuwa mdogo.
Anasema serikali ilipeleka fedha zitokanazo na mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na sasa shule hiyo ambayo ipo pembezoni mwa halmashauri inapokea wanafunzi.
Anabainishwa kuwa shule nyingine shikizi zilizoanzishwa kwa ajili ya umbali ni Mkombozi iliyopo kata ya Kawawa ambayo ilijengwa kwa Shilingi milioni 100 fedha za UVIKO -19 zikijenga vyumba vitano vya madarasa na kwa miaka miwili tangu kuanzishwa wanafunzi 51 wameandikishwa.
Pamoja na ujenzi wa shule kwenye maeneo mbalimbali katika halmashauri hiyo pia suala la chakula shuleni limeendelea kuzingatiwa kwa utaratibu unaofanywa kati ya shule, walezi na wazazi lengo likiwa ni kuwapa chakula ili wasikwamishwe na njaa.
Mmoja wa wazazi wa Kata ya Kawawa Athumani Issa, anaeleza kuwa kuboreshwa kwa mazingira kutaleta hamasa kwa wanafunzi akisema wapo wanafunzi waliokuwa wakisuasua kutokana na kuchoka kutembea umbali mrefu huku wengine wakifeli kwa kukosa muda wa ziada wa kujisomea baada ya muda wa kawaida wa masomo.
Omari Hassan anayeishi Mlandizi anasema serikali kuimarisha miundombinu ya shule ni kuinua kiwango cha elimu na ufaulu kwani hakuna mzazi au mlezi atakayekubali mtoto asiende shule ambayo ipo karibu na mazingira ya nyumbani na pia ni bora.










