Masharti na kukosa mbinu utafutaji kunavyowakwamisha wenye ulemavu

23May 2023
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Masharti na kukosa mbinu utafutaji kunavyowakwamisha wenye ulemavu

ELIMU ya mbinu za utafutaji miongoni mwa wajasiriamali wanaoishi na ulemavu ni tatizo. Aidha, mwamko wa kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na serikali  ni mdogo, ikilinganishwa na wasio na ulemavu kutokana na vikwazo mbalimbali  kama masharti ya mikopo hiyo.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Watu Wenye ulemavu, Ussi Khamis Debe. PICHA: RAHMA SULEIMAN

Kutokana na vikwazo, idadi ya waliopata mkopo ni ndogo na kati ya vikundi 90 vya wajasiriamali wenye ulemavu vilivyosajiliwa Zanzibar ni 12 pekee vilivyopata fedha za mkopo wa UVIKO-19.

Ikumbukwe wakati wa janga la corona, serikali ilipata mkopo wa Shilingi bilioni 230 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kukabiliana na athari za maradhi hayo.

Wizara ya Masuala ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar, ilitengewa Shilingi bilioni 31 kwa ajili ya wajasiriamli visiwani Zanzibar.

                                   

Fatma Mgwali Khamis, katibu wa kikundi cha watu wenye ulemavu mkoa wa Kaskazini Unguja cha Safinia yako, ambaye haoni anasema upatikanaji wa mikopo hiyo umekuwa na changamoto kubwa hasa kwa wenye ulemavu.

Anasema kikundi chao chenye wanachama 20 ambao wanajishughulisha na kazi za mikono za ufumaji ni mwaka pili sasa tangu kuomba mkopo huo hawajapata kitu.

“Tumeshakamilisha taratibu zote za kuomba mkopo huu mwaka wa pili hatujaingiziwa fedha na shughuli zetu za uzalishaji zimesita. Tumejaribu kufuatilia benki lakini wanasema hawajaona fomu ya maombi yetu,”anasema.

Anasema miradi yao imesimama kutokana na kukosa fedha za kununua malighafi inayotumiwa kufuma.

Fatma anataja malighafi wanazotumia kuwa ni kamba za usumba (makkumbi ya nazi) kwa ajili ya kufuma mazulia na mikoba ambayo soko lao kuu ni watalii.Walipoomba mkopo walitarajia fedha hizo kuwaongezea mtaji ili kuzalisha bidhaa nyingi na kuwa na soko la uhakika.

“Hivi sasa tunapata tenda ya kuuza bidhaa zetu lakini hatuna kitu kwa  sababu ya kukosa zana na nyenzo za kufanyia kazi kama tungepata mkopotungeendeleza uzalishaji,” anasema Fatma.

Fatma ambaye ni diwani viti maalum mkoa wa Kaskazini Unguja anaiomba serikali fedha hizo kupelekwa katika mabaraza ya miji ili kusaidia katika utaratibu uliowekwa.

Fatma anaungwa mkono na Njuma Ali kutoka kikundi cha watu wenye ulemavu  wa kukindi hicho kinachojishughulisha na  ufinyanzi.Njuma, anasema siku zinayoyoma, fedha za mkopo hawajapata licha ya kukamilisha taratibu zote zinazohitajika ikiwamo kuwa na akaunti namba yakikundi na kujaza fomu ya mkopo, ambayo  wameyakamilisha  na muda umepita tena takribani mwaka sasa hakuna fedha walizopata.

Anasema waliomba mkopo baada ya Rais Dk. Hussein Mwinyi kusisitiza kuitumia fursa ya fedha za UVIKO-19 kujikwamua kiuchumi baada ya kuathiriwa na janga la maradhi hayo.

Mjasiriamali Nasra Hamad, mwenye ulemavu wa viungo ni mama lishe, anasema kuna usumbufu mkubwa wa kuomba mkopo huo na alikatatamaa mapema kuomba mkopo kutokana na vikwazo.

Anashauri serikali  kukutana na  wenye ulemavu na kuwapa elimu jinsi ya kuomba mkopo huo ili kuondokana na usumbufu wanaokumbana nao.“Kila siku tumekua tukirejeshwa kuwa maombi yetu hayajakamilika mara nenda huku mara kule hali ambayo imenikatisha tama,” anasema.

Anasema watu wenye ulemavu wanahitaji mikopo nafuu kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini lakini pia kuondosha wimbi la ombaomba mitaani ambako wenye ulemavu wanaongoza kwa idadi.

 

WAJUTIA MIKOPO

Katibu wa kikundi cha Yajayo Yanafurahisha huko Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja, Muhammed Abdallah, anasema nia ya mkopo huo ni nzuri lakini haujawanufaisha wenye ulemavu.Anasema waliomba mkopo wa milioni 15 na kupatiwa 8,000,000 Machi mwaka jana, akikiri uwepo wa changamoto katika kuomba mkopo huo hadi kuupata akitaja  harakati nyingi za kuanza usajili hadi kupata fedha.

“Kuna vipengele vingi kuanzia usajili nenda rudi ni nyingi lakini mkataba wao wa kurejesha malipo unatisha na sio rafiki kwa wenyeulemavu kama sisi,” anaongeza Abdallah.Anasema muda wa kurejesha ni kikwazo... “Tunaojishughulisha na kazi ya ushonaji tunatakiwa tukamilishe marejesho ya fedha tulizokopa ndani ya mwaka mmoja na nusu,” anasema.

Muda  ni mdogo hasa ikizingatiwa kuwa mauzo wanayouza si ya kiwango kikubwa na lazima wanatakiwa kurejesha fedha hizo za mkopo benkikila mwezi ni Shilingi 440,000, anaeleza Katibu.

 

“Fedha tuliyopatiwa yote tumenunulia vifaa vya kazi pamoja na mali ghafi….huu mkopo kwa kweli umetuweka roho juu maana hatunafaida tunayoipata, tunapouza bidhaa inatulazimu tuchangishane wanachama ili turejeshe benki kwa sababu mauzo yetu hayafiki 400,000 kwamwezi.”

Anasema hawataendelea tena kukopa baada ya kumaliza deni kwa sababu wanapitia wakati mgumu.Katibu Mtendaji wa Baraza la Watu Wenye ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe, anasema mikopo ya fedha za UVIKO-19 hasa kwa  wenye ulemavu nitatizo  licha ya Rais  Mwinyi kuagiza wapewe.

“Sisi baraza tumechukua jitihada za kutengeneza vikundi vya watu wenyeulemavu maana vilikuwa vichache na hadi sasa viko  90 Unguja na Pemba, tulivyovisajili ili kutimiza masharti na tukaviunganisha na wakala wa uwezeshaji, kazi ipo katika utoaji wa mikopo kuna nenda, urudi nyingi mno,”anasema Debe.

Analeza kwa mshangao kuwa vikundi 90  vilivyoomba mkopo huo  12 ndivyo vilivyopata na baadhi ya vingine vinakataa kukopakwa kuogopa kufilisiwa au kushtakiwa kwa kushindwa kulipa.

Anasema juhudi zinahitajika, kubadilisha mitazamo hasi ya vikundi hivyo ili kuitumia fursa ya kupata mikopo itakayowasaidia kujiendesha kiuchumi na kuachana na ombaomba.Asha Aboud mwanaharakati wa kutetea haki za watu wenye ulemavu, anasema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha juhudi zao za kupata maendeleo.

Anazitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni ukosefu mitaji kwa sababu  wengi hawakopesheki kutokana na uwezo mdogo.

Anasema zipo taasisi za fedha ambazo zinatoa fedha za mikopo kwa makundi mbalimbali kuendesha shughuli za ujasiriamali lakini kwa wenye ulemavu hayajafikiwa kikamilifu.

Mratibu wa jumuiya ya watu wasioona Zanzibar, Adil Muhammed, anasema wameitumia fursa hiyo ya mikopo lakini wengi wao hawakuzipata licha ya kufuata taratibu hivyo wamekata tamaa.

 

“Sekta nyingi zinapuuza kuwashirikisha wenye ulemavu hali inayosababisha kuwepo  athari kubwa kwao lazima tushirikishwe katika utoaji waruzuku,” anasema Muhammed ambaye haoni.

“Unapofatilia jambo lolote sisi tusiona huwa na changamoto kubwa sababu ina tulazimu tuongozane na atakayetuongoza kwa kila jambo ambaye inabidi umgharamie kila kitu. Unapofuatilia fursa kama hizi ukaambiwa njoo kesho, njoo kesho inatuvunja moyo na kutugharimu,” anasema Muhammed.

Kassim Haji Mrisho Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mitaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, anasema wajasiriamali na watu mbalimbali wamehamasika kuomba mikopo ya fedha za UVIKO-19 lakini kundi la wenye ulemavu ni wachache.Anasema awamu ya kwanza imetoa mkopo wa Shilingi bilioni 15 kwa vikundi mbalimbali vya wajasiriamali ikiwamo ya watu wenye ulemavu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harusi Suleiman anasema serikali inasimamia kuona sheria ya watu wenye ulemavu inatekelezwa kikamilifu, lengo ni kuona haki za makundi hayo zinapatikana zikiwamo fursa za kiuchumi.

Harusi, anasema, sheria ya watu wenyeulemavu ya mwaka 2022 lengo lake ni kwenda na wakati na mabadiliko yaliopo sasa duniani ikiwamo mikataba ya kimataifa na kikanda kulinda haki za makundi hayo.