Mwenyeji Samia adokeza Tanzania iko pazuri, mzizi kwenye afya umma

25May 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mwenyeji Samia adokeza Tanzania iko pazuri, mzizi kwenye afya umma

NI siku chache zimepita, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amezindua maandalizi ya mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika, kuhusu uwekezaji rasilimali watu na kujibu hitaji la nguvu kazi hiyo utakaoanza leo, ukidumu kwa siku mbili.

 

Taarifa ya Benki ya Dunia iliyosambazwa juzi, ikamnukuu Rais Dk. Samia kuhusu nafasi ya viongozi wa Afrika, waunda sera na wadau wa maendeleo kwa ujumla, kufuatilia afya na stadi za watu walioko kazini.

Hilo linafanyika, huku Makamu Rais wa Benki ya Dunia, Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika, Victoria Kwakwa akitaja matarajio ifikapo mwaka 2050, idadi ya watu itaongezeka mara mbili kufika bilioni 2.2, ilhali imeingia katika karne iliyoko na pengo la nguvukazi inayojimudu.

Kimsingi, Rais Dk. Samia anapozungumzia maendeleo ya nguvukazi, kwa sura ya awali ina maana ya mtaji kiuchumi, lakini nyuma ya pazia kunakobeba picha pana na kuu inaangukia uchumi.

Mzizi wa taasisi rasilimali watu (human resource), inasimamia sura ya ubunifu au kujiongeza, ikiwa ndiye mkuu katika yote ya uzalishaji na uotaji huduma, ikihama kutoka kwenye mtendaji (personell).

Ni dhana iliyoibuliwa kitafiti kuanzia mizizi ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na wadau wa kimataifa, zikiamini rasilimali watu ndio wanaozalisha na kuendesha nyenzo zingine za uzalishaji, kama mtaji fedha na miundombinu.

Ili rasilimali watu kuwa na tija, inapaswa kuwapo uwekezaji ndani yake ikiisimamia zaidi afya, ndio vingine vinafuata kama vile elimu, huduma na sera. Hapo ndipo hoja na nafasi ya Rais Dk. Samia anatoa tangu anaingia madarakani.

Kwenye msingi wa afya, kuzalisha tija ya kutoka kwa binadamu inaanzia kwenye siku 100 za kiumbe kinapozaliwa, kupata malezi na huduma sahihi za kiafya.

Tanzania ikiwa katika nafasi ya utendaji wake kiuongozi, kumekuwapo staili ya kupokezana vijiti kwenye kivuli cha chama kinachotawala hadi sasa na kwa maana hiyo, wanasimama katika sera inayofanana, tofuati ni katika falsafa ya mkuu wa nchi aliyepo, maono, kadhalika mahitaji ya wakati.

Tangu kuingia kwake madarakani zaidi ya miaka miwili iliyopita, Rais Dk. Samia akiwa mkuu wa nchi na kabla ya hapo zaidi ya miaka mitano, makamu mkuu wa nchi ana mengi katika kufanikisha kuandaa nguvu kazi.

Ushuhuda unaanza katika namna akitumikia awamu ya tano makamu rais na rekodi ya sasa, kisha mkuu wa nchi, sasa ikiwa ni miaka mitano na ushee akipiga hatua kubwa kuneemesha rasilimali watu wa sasa na wajao.

DK.SAMIA NA MMAM

Mzizi wake unaanzia, Rais Dk. Samia katika uongozi wa awamu ya sita kwenye ‘kijiti’ cha Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) ulioasisiwa katika awamu ya nne, chini ya Rais Jakaya Kikwete umekuwa na mtazamo mpana.

Tangu wakati huo kumetengwa kila kijiji au kitongoji kuwa na zahanati, kituo cha afya kwa kata na ngazi zote za juu ni kuwa na hospitali, kuanzia mkoa na zaidi kuwapo hospitali za rufani.

Hiyo yote imebeba maana ya kusogezea tija ya kiafya Mtanzania kuanzia  anayezaliwa, aliye masomoni, kazini hadi mstaafu, mfano hai unaoendelea wa kampeni za kuwapo chakula kwa wanafunzi shuleni, ili kupatikana tija darasani. Hao ndio nguvu kazi kwa kipindi kijacho, ambao wana historia ya tija kwa siku zao 100 za uhai.

Hapo inapoongezewa na elimu bora, hali kadhalika sera na huduma sahihi, inatoa majibu kwa tija ya rasilimaliwatu kitaifa, ikishuhudiwa fursa zake zikipanuliwa kwa namna endelevu, mfano maboresho yanayofanyikia katika mrejesho wa mikopo elimu ya juu.

Kwa namna ya upekee, Rais Dk. Samia, ndani yake akaingiza juhudi ambazo zinapanua fursa ya kijinsia katika uongozi kitaifa, nafasi za wanawake zikipanuka kwa kasi.

Ni wiki hii Rais Dk. Samia, akaweka wazi namna anavyopanua idadi ya majaji katika ngazi ya mahakama kuu, ikiwa inakaribia uwiano kufikia asilimia 50.

Katika juhudi hizo za rais wa awamu ya sita, mtangulizi wake wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete akavunja ukimya, akitoa rai kwa Watanzania kumuombea Rais Dk. Samia, ili aendelee kuwa na afya njema na kuwatumikia wananchi kwa kutatua changamoto zinazowakabili.

Kikwete akiwa mjini Kibaha mnamo katikati ya mwezi uliopita, iliyoandaliwa na Rais Dk, Samia kwa ajili ya wananchi wa mkoa wa Pwani, akitamka:"Kazi aliyo nayo Rais (Dk. Samia) ni kubwa. Inahitaji hekima na juhudi nyingi, hivyo ili kufikia malengo anapaswa kuongozwa na Mungu, sisi sote ni vyema tukamuombea,”

ANAVYOTETEA AFYA

Rais Dk. Samia akafafanua, chapicho la kitabu ‘Tanzania Nutritional Survey’ la mwaka 2019, udumavu kwa watoto wenye chini ya umri miaka mitano ulikuwa asilimia 31.8; wenye uzito pungufu asilimia 15; ukondefu asilimia 3.5.

Vivyo hivyo akarejea, hali ya lishe kwa wajawazito katika ngazi ya kujifungua inaonesha upungufu wa damu asilimia 28; huku utapiamlo uliokithiri unaendelea kuongezeka kufikia asilimia 31.8, wote wakiangukia zao la nguvu kazi kwa wakati tofauti.

Hapo ana nena katika zama za uongozi wake kuwa: “Nafurahi kueleza kwamba juhudi zinazofanywa na serikali kwenye suala la lishe, ikiwamo kutoa elimu kuhusu masuala ya lishe, kutenga mafungu maalum kwa halmashauri, kuongeza virutubishi kwenye chakula na kuwapa dhamana wakuu wa mikoa kusimamia masuala ya lishe kwenye maeneo yao, kumeboresha hali ya lishe ingawa jitihada zaidi zinahitajika.”

Katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Rais Dk. Samia anafafanua vijana ni nguvu kazi muhimu kuweka nguvu za pamoja, serikali ikiendelea kutoa elimu, sambamba na kukabili ugonjwa Ukimwi na Virusi vya Ukimwi.

Akiwa ziarani mkoani Geita, Rais Dk. Samia, akatilia mkazo hoja ya maboresho ya rasilimali watu nchini, kwa kuwataka Watanzania kujiunga na bima ya afya kwa wote pindi itakapoanza ili wanufaike nayo, huku serikali ikiboresha huduma za afya nchini.

Ni hatua inayogusa pia kinamama na hali ya kijinsia, pale raslimaliwatu yao shuleni inapopata mimba, amewaandalia utaratibu unaowapa fursa kurejea masomoni.

Mkutano wa uwekezaji rasilimali watu unawaleta pamoja wakuu wa nchi na serikali za Afrika kubadilishana uzoefu na kutoka na azimio la pamoja juu ya namna ya kuboresha uwekezaji huo barani Afrika.