Zijue ishara za nje panapo shida kwenye afya ya akili

19Jan 2023
Christina Mwakangale
DAR ES SALAAM
Nipashe
Zijue ishara za nje panapo shida kwenye afya ya akili

KWENYE jamii masuala ya afya ya akili hususan kwa nchi zinazoendelea mwamko bado upo chini, jambo linalosababisha ongezeko la matukio, ikiwamo watu kufanyiwa ukatili kama vile kudhalilishwa nafsi zao.

Mtaalamu bingwa wa afya ya akili kutoka Idara ya Afya ya Akili, Hospitali ya Rufani ya Kanda Mbeya (MZRH), Dk. Raymond Mgeni, anasema zipo dalili ambazo kitaalamu huchukuliwa kuwa chanzo cha magonjwa hayo na hazitakiwi kupuuzwa, ikiwamo hasira, kucheka bila kuchekeshwa, kuongea bila kuwa na wa kuongea naye.

“Kukasirika kusiko na sababu au kukasirika kwa kufoka foka, pia zinaweza kuwa ni dalili ya ugonjwa wa akili. Lazima unaposema huyu ana ugonjwa wa akili, kuna vigezo huzingatiwa kutokana na miongozo ya kuleta jina la ugonjwa wa akili aliyo nayo mgonjwa,” anasema bingwa.

Anaendelea: “Kupandwa na hasira ni jambo la kawaida. Hasira isiyo ya kawaida huweza kuashiria ugonjwa pia, hasa kwa ugonjwa ujulikano ‘baipola’...”

Anaeleza kuwa, pia wapo watu wenye utani uliopitiliza kwa wengine, jambo linalomfanya anayetendewa utani huo kuupokea kwa mtazamo hasi au chanya, huku akionya kwamba vitendo hivyo mara kadhaa hujitokeza maeneo ambayo wamezoeana hukutana mara kwa mara kama vile maofisini.

“Mtu anataniwa na pengine anachotaniwa ni jambo la kweli. Ukishasikia kutokana na utani huo, hauwi mgonjwa, sema ni vile watu hukasirika sana wanapoguswa katika ‘self-image’ (mtazamo binafsi). Jinsi wanavyojitazama, ni rahisi kuathirika na maoni kutoka nje,” anasema Dk. Kuganda.

Tabibu bingwa wa afya ya akili, Dk. Saidi Kuganda, anasema hata watu wanaofanya mambo mabaya, wanapoambiwa kwamba wao ndio wamefanya vitendo hivyo, hukasirika. Yote hayo, anaainisha kwamba ni muhimu jamii kuwa makini nayo.

“Watu wanaofanya mambo mabaya, wakiambiwa ukweli hukasirika. Mtu kweli ni muongo, halafu ukimwambia muongo anakasirika. ‘Why’? (kwanini). Si jambo jema kutaniana kunakopeleka ‘negative emotions’ (hisia hasi) za mwenzio.

“Akikukataza ukatazike, ndio mtaenda sawa. Vinginevyo ni kumnyima furaha na amani mwenzio, jambo ambalo ‘in a long run’ (ikichukua muda mrefu) linaweza kumsababishia mwenzio hasira (negative emotion) au msongo wa mawazo.

“Hii changamoto ikizidi inaleta madhara na maradhi,” anasema Dk. Kuganda, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Afya ya Akili Tanzania (MEHATA).

USHAURI WA MABINGWA

Dk. Mgeni, ambaye anatumikia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), anatamkia kwamba yapo mambo muhimu 10 yanayoweza kusaidia jamii kukuza uelewa kuhusu afya ya akili na magonjwa ya akili nchini.

Hapo anaorodhesha suala la kusikiliza vipindi maalumu kupitia vyombo vya habari kama radio, runinga na maandiko magazetini.

Pia anataja haja ya mafunzo na elimu kwa jamii kuhusu afya ya akili, yanayopaswa kupewa kipaumbele mitandaoni, kwa kushirikisha wataalamu kutoka idara za afya ya akili; madaktari, wanasaikolojia, watu wa tiba kwa kazi, maofisa ustawi wa jamii pamoja wauguzi, akisisitiza hasa wa idara za afya ya akili.

“Lengo la kufanya hivi, iwe katika kutoa elimu juu ya afya ya akili na magonjwa ya akili. Jamii bado ipo gizani, inapokuja suala la afya ya akili pamoja na magonjwa ya akili. Hili linawanyima watu kupata huduma hizi haraka pindi wapatapo changamoto za kuugua akili.

“Huduma za afya ya akili na saikolojia ziwapo katika hospitali zote za serikali na taasisi binafsi. Umuhimu huu ni kuhakikisha watu wanapopata changamoto zinazoweza kuwaathiri afya ya akili, kupata huduma za wataalamu wa tiba ya akili mapema na kufikika,” anasema bingwa huyo.

Hapo anafafanua nafasi ya mafunzo ya udhibiti wa msongo wa mawazo sehemu za kazi, iwe ni lazima katika taasisi za serikali na binafsi.

“Eneo la kazi limekuwa linachangia sana watu kukutana na msongo wa mawazo. Hivyo, mafunzo yanapokuwapo ya kuwajengea watu uwezo wa kukabiliana na hali za msongo wa mawazo itasaidia kupunguza changamoto za wafanyakazi wanaokuwa katika hatari ya kupata baadhi ya magonjwa ya akili mfano sonona.

“Pawe na masomo kuhusu afya ya akili na kuzifahamu dalili za makundi ya magonjwa ya akili yatakayojenga msingi kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi, sekondari na vyuoni, namna waweze kulinda afya ya akili na pindi mtu anapokuwa na dalili aweze kujua pa kupata msaada,” anashauri bingwa huyo.

Eneo lingine anataja ni haja ya kuwapo mijadala kupitia majukwaa ya mitandaoni, ikiwamo mfano ‘Clubhouse, Twitter’ inayogusa elimu ya afya ya akili na hatua za kuchukuliwa pindi mtu anapopata changamoto za afya akili, ajue wapi pa kwenda.

“Pawepo huduma za mawasiliano ya simu yanayopatikana wakati wote, kwa msaada wa dharura, huduma za afya ya akili pindi mtu anapofikiria kujidhuru au kutawaliwa na mawazo ya kutaka kujiua. Hili linaweza kufanikiwa kushirikiana na kampuni ya simu,” anashauri mtaalamu huyo.

Dk. Kuganda anasema, pia nyumba za Ibada, iwekanisani au misikitini, viongozi wa dini wawe na nafasi ya kuwajengea uwezo waumini wao katika kudhibiti hali za hasira, ili kuepusha watu kujichukulia sheria mkononi na kudhuru wengine.

Hapo, anashauri kutolewe fursa za ufadhili kwa wataalamu wa idara ya afya ya akili, kuongeza elimu ya kibingwa kusaidia zaidi katika utoaji wa elimu na hata matibabu ya magonjwa ya akili.

Mkurugenzi wa Afya ya Akili na Matumizi ya Dawa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Dévora Kestel, alihitimisha hoja ya kitaalamu, kwa kurejea Ripoti ya Afya ya Akili ya Mwaka 2022.

Kestel anasema wenye changamoto ya afya akili, hukumbana na unyanyapaa, kutengwa na jamii na mazingira duni na huduma za kusaidia afya ya akili nafuu na ubora, akisema kwamba kila mtu ana haki ya afya ya akili.

0000

Top of Form

Bottom of Form