Bingwa aichambua kwikwi, tiba yake

19Jan 2023
Pilly Kigome
DAR ES SALAAM
Nipashe
Bingwa aichambua kwikwi, tiba yake

KWA maisha ya binadamu suala la kupata kwikwi si geni, inafahamika kuvitokea viumbe vingi vinavyoishi duniani. Ila swali je, huo ni ugonjwa?

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto kutoka Hospitali ya Rufani Mkoa wa Temeke, Salha Ally, anakana kwikwi kuwa ugonjwa, bali anaitafsiri ni dalili kuna ugonjwa unataka kujitokeza kwenye mwili huo.

Anaitafsiri kwikwi inatajwa ni kitendo kisichozuilika, kitokanacho na kusinyaa kwa kuta za kiwambo cha moyo au ‘diagram’ kitendo kinachojirudia mara nyingi kwa mwanadamu, huku kikitoa sauti.

Dk. Ally anasema, husababishwa na kidaka tonge cha kiumbe kama binadamu (epiglottis) ambacho hufunga haraka wakati hewa inapoingia kwenye koo.

“Kwikwi pia tunaweza tukasema, ni kitendo cha kutetema au kurukaruka kwa mwili mara kadhaa, kinachotokana na hali ya mfumo wa hewa unapoingia kwenye koo hufanya hali hiyo ya kurukaruka kwa mwili,” anasema.

Dk. Ally anasema, kwikwi hutokea pale upumuaji wa mtu unapositishwa kwa kipindi kifupi. Pia inaweza ikatokea bila sababu na mara nyingi huwa ya ghafla, lakini ikiendelea kwa muda mrefu ni ishara ya tatizo la kiafya.

Kwa mujibu wa daktari huyo, watu wengi hupata kwikwi na kisha inaondoka yenyewe. Pia kuna mazingira kwikwi huondoka kwa tiba za awali. Vilevile anataja, kuna kwikwi zinazochukua muda mrefu inayoendelea zaidi ya saa 48, anaitaja ni ya hatari na inahitaji msaada wa kitaalamu kutoka kwa madaktari, kwa kuwa inaendana na tatizo kubwa la kiafya.

Dk. Ally anaielezea Nipashe kuwapo kwikwi kwa mtu kila mara, maana yake ni kwamba, ana dalili ya kupungukiwa madini kama vile sodium, potassium na wengine kuangukia magonjwa ya kisukari, figo na maambukizi ya bakteria.

WATOT0 WACHANGA

Anasema, kwa upande wa watoto wachanga, hali hiyo hujitokeza kutokana na ukosefu wa maji mwilini na ikiwa mtoto hapati maziwa ya kutosha kutoka kwa mama, kuna uwezekano wa kukutana na hali hiyo ya kwikwi.

Katika hilo, anawashauri kinamama kuwanyonyesha watoto kitaalamu na kwa maelekezo maalum kutoka kwa mtaalamu wa afya, kwani kadri siku zinavyoenda, kunaonekana ukiukwaji kwa kanuni stahiki za kiafya katika kuwanyonyesha watoto wachanga, miili yao ipate mahitaji muhimu kiafya.

 

INAVYOJITOKEZA, INAVYOTIBIWA

Inatajwa pale inapotokea mtenganisho wa misuli inayoweka mipaka ya kifua na tumbo, ina mchango mkubwa katika mwendo wa mtu kupumua.

Kuna hali ya kujikunyata ghafla, sehemu ya mwanzo ya koromeo inayohusika na kutoa sauti, kwamba inajibana na kusababisha kufunguika kabisa koo. Hapo, kunachangia hewa kuingia ghafla kwenye mapafu na kutokea kwa sauti iliyozoeleka kwa jina la kitaalamu ‘hic’.

Ni eneo linalohusika na sauti; kwikwi moja inaweza ikatokea au zikaja mfululizo kwa mpangilio maalum, wastani wa kwikwi mbili.

Kuna mambo yanayotajwa kuchangia ni; kula haraka haraka bila kituo, kumeza hewa pamoja na chakula, kula chakula kingi cha mafuta au chenye viungo vingi, matumizi ya vinywaji vyenye kaboni.

Mengine kwa mujibu wa Daktari Ally, kunywa pombe nyingi kwa mpigo, tumbo kujaa gesi au vidonda vya tumbo.

Anataja zingine ni mabadiliko ya ghafla ya hali ya hewa, kiharusi au uvimbe kwenye ubongo, hofu au msisimko na hata baadhi ya matumizi ya dawa zinaweza kusababisha shida kwikwi, zikiwamo zile za acid reflix, nicotine, benzodiazepines.

UNAONDOAJE KWIKWI

Mtaalamu wa tiba asili kutoka jijini Dar es Salaam, Hamis Kaibu, anaeleza tiba za kuidhibiti kwikwi, zinajumuisha kuweka sukari chini ya ulimi kiasi cha nusu kijiko na wakati wa kumeza, mtu abane pua kwa vidole; pili anataja kunywa maji haraka, mtu akivuta hewa taratibu kwa ndani.

Tatu, anataja kitunguuu maji nacho kinasaidia kutoweka tatizo hilo, kwa kusaga kitunguu kuchanganya na chumvi, majisafi kupatikana juisi ambayo mtu akinywa mara mbili inasaidia kukabili tatizo hilo.

Pia anataja hiliki iliyotwangwa ikichanganywa na maziwa fresh kinywaji hicho kinasaidia kuondoa tatizo hilo.

Mkazi wa Kigogo Mkwajuni, Dar es Salaam,  anayejitambulisha kwa jina Saidi Selemani (57), anafafanua kuwa njia nyingine za asili zinazosaidia tatizo hilo, ni mtu kufikicha macho, kunywa maji haraka, huku akiwapo mtu kando amwita jina lake.

Kulala usingizi kifudifudi, nako kunatajwa tiba ya tatizo hilo kwa haraka, kwa mtoto anayeweza kuwekwa begani huku akiwa anampigwa mgongoni, naye husaidiwa kwa kiwango kikubwa, kwani kunamshtukiza mgonjwa na kuondoa mwenendo wa kwikwi.

Dawa zitumikazo ni za aina nyingi na hakuna dawa maalum kwa ajili ya kutibu kwikwi. Tiba huenda zaidi kwenye visababishi.

 

 

Top of Form

Bottom of Form

Top of Form

Bottom of Form