Wakati serikali ya DRC, ikisema hivyo, kundi la Islamic State (IS), limekiri kuhusika katika shambulio hilo la bomu kwenye Kanisa la Pentekoste lililoko Kasindi, mashariki mwa nchi hiyo.
Watu takribani 10 wanauawa katika tukio ambalo lilitokea waamini wakienda kwenye ibada ya Jumapili iliyopita Januari 15, kwa mujibu wa maofisa nchini humo.
Pia taarifa zinasema takriban watu 39 wamejeruhiwa na Jeshi la Congo lilieleza kwamba kitendo hicho ni cha kigaidi cha ADF.
Kundi la ADF ni mojawapo ya vikundi vya waasi vinavyojulikana hasa eneo la mashariki la DRC, ukanda ambao unatajwa kuwa wa hatari zaidi nchini humo.
Jumuiya ya kimataifa imelaani hatua ya kundi hilo na mauaji ya mamia ya raia wa DRC pamoja na kushambulia huku rambirambi zikitumwa kwa familia zilizofiwa.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini DRC, umelaani shambulio hilo wakati Msemaji wa Jeshi la DRC, Antony Mualushayi, akisema: "Ni wazi kwamba ni kitendo cha kigaidi kinachofanywa na magaidi wa ADF ambao wamepata hasara ya vita na kipigo kutoka kwa vikosi vya Jeshi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo".
Kasindi iko takriban kilomita nane kutoka mji wa Beni ambako ADF ina ngome, mwishoni mwa mwaka jana, mwakilishi mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, analiambia Baraza la Usalama kwamba, usalama ni moja ya changamoto kubwa inayokabili DRC.
WAASI DRC
Kundi la Waasi wa ADF, ni la wanamgambo wa Kiislamu, lilianzishwa katika miaka ya 1990 na kimsingi linahusika na malalamiko ya ndani ya Uganda.
Tangu lilipoibuka tena DRC, kwa mfululizo wa mashambulizi dhidi ya raia wa Congo na mwelekeo wa kimataifa wa kijihadi, ADF limezidi kudai mashambulizi yanayofanyika ikiyahusisha na IS.
Siku moja baada ya shambulio hilo, mshukiwa ambaye ni raia wa Kenya, amekamatwa akihusishwa na shambulio la bomu kwenye kanisa huko Kasindi katika Jimbo la Kivu Kaskazini Mashariki mwa DRC.
Msemaji wa Jeshi la Congo, Kapteni Mualushayi, anathibitisha kwamba mshukiwa huyo alikamatwa katika kituo cha mpakani cha Kasindi muda mfupi baada ya shambulio hilo.
Rais wa Congo, Felix Tshisekedi, amelaani vikali shambulio hilo na kuahidi kuwafikisha wahalifu mbele ya sheria.
HATARI MASHARIKI
Eneo la mashariki mwa DRC, limekuwa kitovu cha mapigano ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwasambaratisha wengine wengi kwa miongo takriban miwili.
Waasi wa ADF wanaendelea kuwa tishio kwa usalama wa raia wanaoishi mashariki mwa DRC. Shambulio hilo ambalo tangu wakati huo limedaiwa ni la IS inayojiita Jimbo la Afrika ya Kati (ISCAP).
Mashirika ya kiraia mashariki mwa DRC, yamesema watu zaidi ya 60 wameuawa katika kipindi cha wiki moja kutokana na mashambulio ya makundi ya waasi.
Hivi sasa, wakuu wa majeshi wa nchi za Afrika Mashariki wanakutana tena katika mji wa Mashariki wa Goma, kubuni tena kikosi cha kikanda cha kumaliza makundi hayo ya wanamgambo.
Wanatarajia kuweka sheria, vifaa na muda wa mwisho wa operesheni za kikosi hicho, licha ya kwamba hadi sasa bado haijafahamika ni lini kikosi hicho kitaanza rasmi operesheni zake dhidi ya wanamgambo watakaokiuka maagizo ya kusitisha uasi.
Kwa nchi hizo kukutana na kijadili, si awamu ya kwanza, kwani mkutano wa aina hiyo hufanyika na hata kuundwa kwa kikosi maalum cha kikanda cha kukabiliana na makundi ya wanamgambo huko Congo.
Umoja wa Mataifa, umeweka juhudi kadhaa, kupitia ujumbe wake wa walinda amani nchini humo MONUSCO na vikosi vya kikanda vya kupambana na makundi vya wanamgambo hao, bado ghasia za mauaji ya kikatili dhidi ya raia wasio na hatia zimekuwa zikiendelea kuripotiwa mashariki mwa DRC.
Mashariki mwa DRC kuna makundi zaidi ya 100 ya wapiganaji wa misituni ambao wanasababisha kukosekana usalama, mauaji na kupora mali katika eneo hilo.
Wadadisi wa kisiasa wanasema ni vigumu kwa mashambulio makubwa ya kijeshi kuwamaliza wapiganaji wa msituni, kwa kuwa wajumbe wa makundi hayo wamekuwa na mtindo wa kujificha uraiani wanapokabiliwa na mashambulio makali.
Na kwamba mashambulizi makubwa yaliyolenga kumaliza uasi wa wanamgambo wa FDLR wanaoshukiwa kufanya mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 mwishoni mwa mwaka 2019, yaliwaua baadhi ya wapiganaji wakuu wa kundi hilo, akiwamo Sylvestre Mudacumura.
Baadhi ya maofisa wakuu wa jeshi la Rwanda walisema FDLR sio tatizo, lakini sasa kundi hilo limeanza kusikika likishutumiwa kufanya mashambulizi na sasa Rwanda ikisema linashirikiana na jeshi la Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
Kwa mujibu wa mashirika hayo, mapigano pia yalizuka Jumapili iliyopita kwenye mji wa Ituri, baada ya kuuawa kwa mwalimu wa jamii ya Lendu na kuwachochea wapiganaji wa CODECO wanaodai wanatetea kabila la Wahema kulipiza kisasi.
Wahema na Walendu, wamekuwa na mgogoro wa muda mrefu ambao hadi sasa umesababisha vifo vya mamia ya watu kati ya mwaka 1999 na 2003 kabla ya kutumwa kwa vikosi vya kimataifa kudhibiti mauaji yaliyokuwa yanatokea.
Jumatano iliyopita kuliripotiwa mashambulizi mengine kusini mwa mji wa Ituri, ambako watu kadhaa waliuawa na waasi wanaodaiwa kuwa ni wa ADF.
Shambulio jingine la waasi wa ADF liliripotiwa Alhamisi, huku miili ya watu 21 ikipatikana kaskazini mwa Ituri, kwa mujibu wa ripoti za UN zaidi ya makundi ya waasi 120 yanafanya shughuli zao mashariki mwa DRC, mengi yakipigania kuchukua maeneo yenye utajiri wa rasilimali ikiwamo madini.









