KUONDOKA KIFUNGONI

18Jan 2023
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
KUONDOKA KIFUNGONI
  • Vyama vya siasa sasa ni mguu sawa, vyaanza kujadili kipengele cha masharti

BAADA ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kuruhusiwa, baadhi vimeshaianza, vingine vikiwa vinajiandaa kuanza wiki ijayo na vipo pia ambavyo vinajipanga kukutana kujadili jinsi ya kuendesha harakati za kisiasa.

Magdalena Sakaya Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara. PICHA:CUF

 

CUF, imefungua pazia, ikizindua mikutano ya hadhara, Jumamosi iliyopita katika viwanja vya Bakhresa Manzese Dar es Salaam. 

 Uzinduzi huo unafuatiwa na kila mkoa kuandaa mikutano hiyo, huku viongozi wake wakitarajiwa kujichimbia kwa siku tatu kwenye vikao maalum kujadili mikakati ya kufanikisha mikutano hiyo.

Magdalena Sakaya Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, anasema, vikao vitaanza kesho, makao makuu ya chama Buguruni Dar es Salaam na kwamba vitajadili masharti ya serikali mikutano hiyo.

"Pamoja na kuzindua mikutano yetu, lakini tumeona kuna haja ya kukutana kwanza kujadili mambo mbalimbali yakiwamo masharti ya serikali ya kutaka mikutano isiwe na matusi na kashfa," anasema Magdalena.

WATAKA UHURUNaibu Katibu Mkuu anaitaka serikali iache waseme ukweli katika mikutano ya hadhara, kwa kuwa wamejipanga kujenga hoja zenye maslahi kwa umma na kukosoa kwa hekima.

"Tutakosoa kwa hekima na tunaiomba serikali isitufunge midomo, ituache tuseme ukweli na ukweli usije ukaonekana kama matusi, hivyo ni muhimu kukubali ukweli na kuufanyia kazi."

 

Anasema chama hicho kimezindua mikutano yake Jumamosi na kwamba kila mkoa unaendelea na ratiba ya mikutano ya hadhara.

Magdalena anafafanua kuwa kuanzia kesho, vigogo wa chama hicho, watajichimbia katika vikao kwa siku tatu, kwa ajili ya kujadili mikakati mbalimbali ya kufanikisha mikutano ya hadhara.

"Tuna hoja nyingi za kupeleka kwa wananchi, kuanzia mfumuko wa bei ya vitu mbambali kikiwamo chakula, utendaji mbovu wa baadhi ya viongozi wa serikali, rushwa kukithiri, huduma mbovu za afya hospitalini na maisha magumu," anasema.

Mwanasiasa huyo anasema hakuna mpinzani ambaye anaweza kuongea kwa kupamba, bali atasema ukweli, ambao anaamini serikali ikiuchukua na kuufanyia kazi utachangia maendeleo ya nchi.

"Taifa linaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu, hivyo wale ambao watakwenda kinyume, wachukuliwe hatua, lakini angalizo letu ni kwamba, ukweli usigeuzwe kuwa kashfa au matusi," anasisitiza.

ACT KUJADILIANAWakati mikutano ya hadhara imeruhusiwa, Kamati Kuu cha Chama cha ACT-Wazalendo, inatarajia kukutana jijini Dar es Salaam wiki ijayo Januari 21, kujadili ajenda tatu ikiwamo programu ya ujenzi wa chama 2023.

Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Janeth Rithe, anasema watazungumzia pia hali ya kisiasa nchini pamoja na mambo mengine kuhusu ruhusa ya mikutano ya hadhara.

"Kamati Kuu itajadili pia hatua iliyofikiwa kwenye ajenda ya mageuzi ya kisiasa na kuidhinisha ratiba ya uzinduzi wa mikutano ya hadhara ya chama chetu itakayofanyika nchi nzima," anasema Janeth.

Anafafanua kuwa masuala yote yakiwamo ya jinsi ya kuendesha siasa za kistaarabu na zenye manufaa kwa umma, yatajadiliwa kwa kina na wajumbe wa kamati hiyo na kuiongeza kuwa chama chao ni chenye hoja, si vurugu.

NI HOJA SI MATUSIMkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, anasema mikutano yao itakuwa na hoja zaidi ya 10 na si matusi.

 

"Tuna hoja, sera na ajenda zetu, si matusi, viongozi wasiwe na hofu. Mtu anapotoa lugha za kashfa na matusi, kuna sheria, zinaelekeza cha kufanya, viongozi wasitabiri kitakachozungumzwa katika mikutano," anaonya Mrema.

Kwa mujibu wa Mrema, ratiba ya mikutano ya chama hicho itaanza wiki ijayo, Januari 21 Mwanza, kisha Musoma mkoani Mara na kuendelea katika maeneo mengine ya Tanzania Bara na Visiwani.

"Tutarejea katika hotuba za viongozi wetu mbalimbali walizowahi kutoa kwenye mikutano ya hadhara, kwa kuzingatia kuwa mikutano ilizuiliwa si kwa sababu ya matusi bali kwa sababu ya kutaka watu wachape kazi," anasema.

Anafafanua kuwa CHADEMA si chama cha matusi bali cha hoja zenye mashiko kwa taifa na kwamba hoja zao huwa ni chungu kwa baadhi ya viongozi wa serikali ambao huzichukulia kama matusi.

Kiongozi huyo anaongeza kuwa wamechagua 21 Januari kuwa siku ya uzinduzi wa mikutano ya hadhara, kwa kuwa ni tarehe ambayo kilipata usajili wa kudumu mwaka 1993 na kitakuwa kinatimiza miaka 30.

Rais Samia Suluhu Hassan, ameanza mwaka 2023 kwa kukutana na viongozi wa vyama vya siasa, na kuridhia mambo makuu matatu katika medani za siasa, ambayo yalikuwa kilio kikubwa cha wanasiasa.

Katika mkutano huo, anaruhusu rasmi mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, lakini akisisitiza zaidi siasa za kistaarabu na kuwataka wanasiasa kuepuka kejeli na matusi.

Akizungumza katika mkutano huo anafafanua kuwa aliitisha mikutano hiyo kwa kuwa kulikuwa na masuala yaliyozungumzwa na bado hayajatolewa maamuzi, hivyo akasema ipo haja ya kufanya taifa kuwa kitu kimoja na kuwapo kwa maridhiano.

Tanzania ina vyama 19 vyenye usajili wa kudumu vinavyotarajiwa kufanya mikutano ya hadhara ambavyo ni UPDP, NRA, TADEA, TPL, CHADEMA, CUF, NCCR, UDP, UMD, CCM, Demokrasia Makini, DP, SAU, AFP, CCK, ADC, CHAUMMA na ACT- Wazelendo.