MVUA ZINAPOKOLEA

17Jan 2023
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
MVUA ZINAPOKOLEA
  • Zitumike kilimo na ufugaji, kupanda miti ya kutosha

NI vyema kushukuru Mungu, anayetupatia mvua karibu mikoa yote ya Tanzania sasa, ambayo ni muhimu kwa mustakabali wa maisha ya watu na viumbe hai kuanzia mifugo na wanyamapori.

Kupanda miti kulenge matokeo chanya kwa wakulima, wanyama na makazi salama yenye miti na mvua. PICHA: MTANDAO

 

Kwa miezi kadhaa maisha yaligubikwa na tishio la ukame takriban nchi nzima isipokuwa mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria, ambako msimu wa mvua za vuli haukutetereka.

Mikoa mingine ilikuwa na ukame kwa muda mrefu, uliokwamisha upatikanaji wa maji, mito ya Ruaha Mkuu na Ruvu, ikawa haina maji ya kutosheleza kuzalisha umeme kwenye vituo vya Mtera na Kidatu (Ruaha Mkuu) huku maji yakipungua kwa wateja karibu wote.

Kadhalika, ndani ya kipindi hicho gharama za maisha mijini na vijijini zikapanda kutokana na ongezeko la bei za vyakula iliyotokana na mafuta na kusababisha gharama za usafiri na usafirishaji kupaa.

Hata hivyo maeneo yaliyokuwa makavu yanapata mvua na baadhi yakiathiriwa na mafuriko, kuharibika miundombinu ya barabara, madaraja, kuzoa makalvati na kubomoa matuta ya barabara hivyo kusababisha wananchi wakose huduma za usafiri na usafirishaji wa uhakika.

Pamoja na changamoto hizo, Watanzania wanasonga mbele wanaishi na kujitahidi bila kukata tamaa, ili kumudu maisha yao.

Sasa mvua inanyesha watu waituimie na ardhi pia kwa maarifa ili wasisumbuliwe na adui njaa wakati nguvu wanazo, ardhi ipo tena ya kutosha na maji ya mvua hupatikana karibu nchi nzima.

Uzoefu wa miaka mingi, unaonyesha kuwa wengi wanaitumia ardhi kwa kilimo, ufugaji na shughuli nyingine za uzalishaji tena kimazoea bila kuzingatia thamani yake halisi.

Tangu Uhuru 1961 ni kuogelea kwenye kilimo na ufugaji bila kujali athari zake hasi kwa mazingira, matokeo yamesababisha maeneo kadhaa kugeuka jangwa hali ambayo siyo salama kwa mustakabali wa Watanzania.

Kulingana na takwimu za mwaka 2015 za Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa mwaka, Tanzania Bara ilikuwa inapoteza hekta takribani 372,000 za misitu ya asili.

Mwaka 2017 kituo cha kufuatilia masuala ya ‘gesiukaa’ (CO2) na athari zake kwa mfumo wa hali ya hewa nchini na duniani cha Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), kilitoa taarifa iliyoonyesha ongezeko la kutoweka misitu Bara kwa kiwango cha hekta 469,000 kwa mwaka.

Hili ni tofauti ya hekta 92,000 zinazoongezeka kila mwaka tangu 2015 na kuashiria uharibifu mkubwa wa mazingira nchini na upotevu wa misitu ya asili.

Kwa kuwa mvua inanyesha katika maeneo mengi nchini, ni vizuri hatua za makusudi na nia njema, zichukuliwe ili rasilimali ardhi itumike vizuri kwa shughuli za kilimo; ufugaji na kuotesha miti ya kutosha.

Katika kutimiza adhma hii ipasavyo, nichukue fursa hii kutahadharisha wakulima walio wengi vijijini; kuachana na ‘kilimo cha mazoea’. Kauli hii inamaanisha kuwa: wakulima wamezoea, kwa muda mrefu, wamekuwa na mtazamo kwamba maeneo yenye misitu ya asili ndiyo yanayofaa kwa kilimo. Hivyo, wamekuwa wakifyeka misitu na hatimaye kuchoma moto, kama njia rahisi ya kusafisha shamba au mashamba na kupanda mbegu hususani ni za mazao ya chakula kama mahindi, mtama, ulezi na ngano.

Vilevile, wakulima huotesha mbegu za mazao ya biashara kama pamba, tumbaku, ufuta, kadhalika wafugaji kwa mazoea yao ni ‘kuchunga’ badala ya ‘kufuga’.

Kadhalika, kumekuwapo na mazoea ya kuanzisha makazi mapya vitongoji, katika vijiji vinavyopakana na misitu bila kufuata matumizi bora ya ardhi. Masuala haya yamesababisha kasi kubwa ya kutoweka misitu ya asili.

Ni vyema kuchukua hatua mahususi, kudhibiti matumizi yasiyolenga kuhifadhi mazingira, badala yake kusababisha uharibifu wa ardhi.

Kwanza, halmashauri wilayani ziweke kanuni au sheria ya kuhakikisha kila kijiji kina mpango, uliopitishwa na mamlaka wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji. Kilimo kiwe cha kumwinua mkulima kwa kutumia ardhi ndogo na kuvuna mazao mengi. Kiwe ni kijani kwa misingi ya kuhifadhi udongo lakini kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Maji ya mvua yavunwe na kuhifadhiwa kwa lengo la kufanikisha kilimo endelevu mathalani, wakati wa kiangazi uzalishaji mazao uendelee kupitia fursa za umwagiliaji taifa lineemeke pia kuhifadhi mazingira ipasavyo.

Wataalamu wa kilimo na wengine waliomo katika tarafa au kata mbalimbali; washirikiane na kuhakikisha rasilimali ardhi na maji vinatumika ipasavyo kuwaletea maendeleo endelevu wanavjijiji kwa kutumia rasilimali ardhi vizuri.

Ufugaji pia uwe endelevu na tabia ya kuchunga mifigo kutoka eneo moja kwenda eneo lingine idhibitiwe. Mfugaji awe na sehemu maalumu ya kufugia mifugo yake na kuhakikisha eneo husika analitunza na kuliendeleza ipasavyo.

Isiwe ni kuharibu mazingira ya sehemu fulani halafu kuhamia eneo lingine wakidhani kuwa wao wafugaji wanayo hati-miliki ya maeneo yote Tanzania. Wataalamu wa mifugo wakishirikiana na wenzao katika Tarafa na Kata husika wahakikishe wenye mifugo wanafanya kazi kwa kanuni za tija halisi siyo kuwa chimbuko la migogoro na kuharibu mazingira kwa faida zao binafsi.

Upandaji miti upewe kipaumbele kijamii na kitaifa kwa lengo la kuinusuru Tanzania isigeuke jangwa tukajikuta ‘tunaangamizwa kwa kukosa maarifa’ wakati maarifa Watanzania tunayo.

Kwa miaka mingi halmashauri nchini zimekuwa na lengo la kupanda na kutunza miti milioni moja na laki tano kwa mwaka.

Hata hivyo hali halisi inaonyesha kuwa lengo hilo halijafanikiwa ipasavyo; kutokana na maeneo mengi nchini kuwa wazi. Sasa ni wakati muafaka kwa Watanzania wote, pamoja na mambo mengine, ni kujikita kwenye kupanda na kuitunza miti.

Kwa bahati nzuri watafiti wa Taasisi ya Kufanya Tafiti za Miti (TAFORI) wameainisha maeneo yote na kuonyesha ni aina gani za miti zinazoweza kustawi vizuri katika kila sehemu nchini.

Wataalamu wa misitu, kilimo na mifugo hata wale wa maendeleo ya jamii na mazingira watumie mwongozo huo wa kitaaluma ili matokeo ya zoezi la kupanda miti liwe lenye tija na Tanzania iwe ya kijani.

Kila aliye na uwezo wa kupanda miti apande angalu miti mitatu katika maskani yake. Miwili ya matunda na mwingine wa kivuli mahali pa kupumzikia wakati wa jua kali.

Kama unalo eneo la kutosha tenga sehemu kama eka mbili panda miti inayostawi vizuri katika mazingira hayo kwa faida za baadaye. Licha ya kuboresha hali ya hewa, lakini utavuna miti hiyo itakapokomaa na kupata mbao, nguzo, kuni au mkaa kwa matumizi ya familia au kuuza kupata fedha. Misitu au miti ni rasilimali yenye faida nyingi kwa binadamu:

Ni vyema kupanda miti kwa wingi ili kufaidika siku zijazo. Vilevile, tuhifadhi misitu ya asili iliyobaki kwa manufaa ya leo na vizazi vitakavyofuata.

Wazazi na mababu waliotangulia walihifadhi misitu leo jamii inafaidika kwa kiasi kikubwa; hivyo ni wajibu wa Watanzania wa leo kuhifadhi rasilimali misitu kwa manufaa ya wajukuu wao na vizazi vya baadaye.