Utoro unapotishia kidato cha kwanza, wadau wataja mbinu kuukomesha

17Jan 2023
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
Utoro unapotishia kidato cha kwanza, wadau wataja mbinu kuukomesha

MATUKIO ya baadhi ya wanafunzi wanaochaguliwa kuingia kidato cha kwanza kutoripoti shuleni kwa wakati, yanaelekea kuwa jambo la kawaida.

Shule zimefunguliwa Januari 9, wanafunzi wahamasishwe kwenda shuleni na kujifunza badala ya utoro. PICHA: MTANDAO

Ni kwa sababu yamekuwa yakijirudia kila mwaka katika mikoa mbalimbali, huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni utoro.

Kwa mfano, wanafunzi 4,060 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 mkoani Ruvuma, wanaripotiwa kuwa hawajafika shuleni kuanza masomo, sababu mojawapo ikiwa ni utoro, anaeleza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas.

Utoro huo unasababisha baadhi ya watu kutoa ushauri mbalimbali ambao wanaamini unaweza kusaidia kumaliza tatizo hilo, ambalo kama litaendelea, linaweza kukwamisha maendeleo ya elimu huku serikali ikiigharamiwa kuanzia msingi hadi kidato cha sita.

 

Miongoni mwa wadau hao ni Sadick Chiguma ambaye katika mazungumzo yake na gazeti hili, anasema ipo haja kwa serikali kufanya utafiti kwa nini baadhi ya wanafunzi hawapendi shule na kutafuta ufumbuzi.

"Inawezekana kuna sehemu haiko sawa ambayo inasababisha baadhi ya wanafunzi wanaochaguliwa kuingia kidato cha kwanza wasiripoti shuleni kwa wakati ndio maana ninashauri serikali ifanye utafiti," anasema.

Anataja taarifa ya Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali, kwamba wanafunzi 716, 664 waliotakiwa kuanza kidato cha kwanza, kufikia Januari 15 walikuwa hawajaripoti shuleni akisema inatakiwa kufanyiwa kazi.

"Mimi si mtaalamu wa elimu, lakini kama mzazi, pia mdau wa elimu, hivyo wito wangu ni huo kwamba kwa kuwa matukio ya utoro yanaendelea kujirudia, ni vyema utafiti ufanyike kubaini chanzo cha tatizo na kulikabili," anasema.

HAKUNA HAMASAMdau wa elimu Suzan Lyimo, anasema kinachosababisha baadhi ya wanafunzi kutoripoti shule ni kukosekana kwa hamasa katika elimu, kwa kuwa wapo wanaohitimu bila kujua kusoma na kuandika.

Anasema kwa mazingira kama hayo, wanafunzi wengine wanaona ni bora wakae nyumbani waendelee na shughuli nyingine, badala ya kukazania elimu ambayo wanaona haiwezi kuwaletea maendeleo.

 

"Hata wazazi na walezi wanakata tamaa, hivyo ni muhimu serikali iboreshe elimu ili kivutia watoto pia. Uboreshaji huo ingeanzia kwenye ujenzi wa mabweni katika sekondari zote za kata," anasema Suzan.

Suzan ambaye kitaaluma ni mwalimu na mwanasiasa, mbunge viti maalum CHADEMA kwa kipindi kirefu, anasema kuwa baadhi ya wanafunzi wa sekondari za kata hutembea umbali mrefu hata kilomita 10 kwenda na kurudi nyumbani, kitendo ambacho kinasababisha wachoke na kuona elimu kama ni mateso kwao.

"Lakini ni muhimu kuboresha mtaala ili kusaidia wanafunzi kuwa na kitu au namna ya kuwawezesha kuendesha maisha yao wanapohitimu, kwani baadhi yao hukata tamaa wanapoona waliohitimu darasa la saba wanafanya shughuli zao wanakuwa na mafanikio lakini wa kidato cha nne hawana mbele wala nyuma," anasema.

Mdau huyo wa elimu, anasema ni muhimu serikali iwekeze kwenye zaidi isaiadie wanafunzi kupiga hatua moja kwenda nyingine badala ya kuhitimu na kujikuta wakiwa mzigo kwa wazazi na walezi."Ninaposema kuwekeza kwenye elimu, nina maana kwamba serikali iongeze idadi ya walimu kwani ni wachache lakini idadi ya wanafunzi inazidi kuwa kubwa, hivyo ufundishaji unakuwa mgumu na kusabababisha baadhi ya wanafunzi kutoona umuhimu walimu," anasema.

Anasema baadhi ya watu wanaweza kuchukulia kuwa wiki ya kwanza wanafunzi huwa wanaripoti wachache, baadaye wataongezeka na kwamba hali ya sasa imebadilika, inawezekana wasionekane tena.

 

ZIFANYIKE KAMPENI

Godwin Gonde ni Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia Kurasini Dar es Salaam, anasema ili kumaliza tatizo hilo, ni vyema kampeni kubwa ya muda mrefu ifanyike kuhamasisha umuhimu wa elimu.

"Hatua hiyo inaweza kuwafanya wanafunzi, wazazi, walezi na walimu kujali elimu hasa kama mfumo wake utakuwa na manufaa, kwani baadhi yao wamekataa tamaa na mfumo uliopo, kutokana na kwamba wapo waliotimu sekondari na vyuo, lakini hawajaleta mabadiliko chanya kwenye jamii," anasema Gonde.

Anafafanua kuwa jamii haina kitu cha kujifunza kutoka wale waliohitimu, hasa wa wakati huu, na kuongezea kuwa miaka ya zamani aliyesoma alikuwa tofauti na ambaye hajasoma na kwamba ajira zilikuwapo za kutosha na maisha yalibadilika.

 

“Kwa sasa mtu aliyesoma, hana tofauti na yule ambaye hajasoma, ambaye hajasoma anaweza kufanya mambo makubwa kuliko mwenye elimu ya darasani, hivyo ipo haja ya kuhamasisha umuhimu wa elimu na pia kubadiliko mfumo wa elimu uliopo ambao hamsaidii mwanafunzi kujiajiri," anasema.

 

Aidha, serikali isitumie nguvu kukamata wazazi au walezi ambao watoto wao hawajaripoti shuleni, badala yake ianzishwe kampeni maalum ya kuhamasisha umuhimu wa elimu, huku mfumo ukibadilishwa, anasema mhadhiri huyo."Wadau wa elimu wahusishwe katika kampeni hii ya kuhamasisha jamii kujua umuhimu wa elimu, lakini kikubwa zaidi iwe ni serikali kuangalia mfumo wa elimu uliopo na kuuboresha, ili usisababisha wanafunzi na jamii kwa ujumla kutoona umuhimu wa elimu," anasema.

HALI ILIVYO 2023

Katika taarifa yake ya Januari 15, mwaka huu kwa vyombo vya habari, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, anasema wanafunzi 716,664 sawa na asilimia 67, wanaotakiwa kuanza kidato cha kwanza mwaka 2023, walikuwa hawajaripoiti shuleni.

Msemaji huyo wa serikali anafafanua kuwa wanafunzi 354,277 kati ya 1,070,941 waliotarajia kuingia kidato cha kwanza sawa na asilimia 33 ya matarajio wakiwamo wenye ulemavu 697, ndio ambao walikuwa wamejiandikisha.

Kutokana na hali hiyo, anatoa wito kwa wazazi na walezi kuhimiza watoto wao waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza waripoti shuleni haraka iwezekanavyo ili waendelee na masomo.

Msigwa akafafanua kuwa serikali inagharimia elimu ya msingi na sekondari kwa kutoa Sh. bilioni 29 kila mwezi na kutoa maelekezo ya kuhusu michango ya wanafunzi wanaoanza shule, ili visiwepo vikwazo vinavyoweza kusababisha wasijiunge na shule.

Aidha, anasema wanafunzi 14,581, wameandikishwa katika Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Waliokosa (MEMKWA), huku 334 kati yao wakiwa ni wale wenye mahitaji maalum.