Ziara ya JPM Rwanda ije na tija kwa taifa

16Apr 2016
Adam Mwambapa
Dar
Nipashe
Ziara ya JPM Rwanda ije na tija kwa taifa

HATIMAYE Rais Dk. John Pombe Magufuli, ameamua kufanya ziara yake ya kwanza ya mwaliko nchini Rwanda, baada ya kupita miezi kadhaa tangu kuwapo kwake madarakani mara tu alipopokea kijiti cha uongozi, kutoka kwa Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete.

Tangu Dk. Magufuli, ashinde kiti cha urais na kutangazwa rasmi na Tume ya Uchaguzi Nchini (NEC), Oktoba 25 mwaka jana, kama mshindi aliyewashinda wagombea wengine wa vyama saba vya upinzani, kisha kuapishwa rasmi Novemba 5, mwaka jana, hajawahi kutoka nje ya nchi kwa ziara yoyote ya kikazi au kwa mwaliko wowote isipokuwa ziara hii.

Hatua hiyo imejitofautisha kwa asilimia kubwa na rais aliyemtangulia Dk. Kikwete, anayesadikika kusafiri mara nyingi zaidi kuliko rais yeyote wa Tanzania.

Inasadikiwa mpaka anaachia ngazi na kumpisha Rais Magufuli, alikuwa amesafiri safari 400, zote zikikadiriwa kugharimu Sh. trilioni 4.4.

Ukiachilia deni la taifa linalopanda kila mwaka, lakini pia wafanyabiashara mbalimbali hasa wale wakubwa hawakusimamiwa kikamilifu kulipa kodi zao. Zaidi walijifunza tabia za ukwepaji kodi, iwe kwa kujua au kutojua na kulitia hasara taifa na kuchangia kudidimia uchumi kwa kiasi kikubwa.

Ujio wa Rais Magufuli, kwa kushirikiana na safu yake ya uongozi hasa Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, umeonyesha jinsi wanavyofichua yale ambayo wananchi wengi hawakuyatambua.

Mambo yaliyowahi kupigiwa kelele na wadau mbalimbali vikiwamo vyombo vya habari, wakilalamika jinsi wafanyabiashara wakubwa wanavyokuwa si waumini safi wa ulipaji kodi, ingawaje kelele hizo hazikupewa umuhimu unaostahili.

Ikumbukwe kuwa, maendeleo ya nchi yoyote yanayoonekana kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na ulipaji kodi sahihi.
Hilo likiwa ni jambo kubwa pengine kuliko mengine, lakini pia, maendeleo huja kwa wananchi kuweka utaifa na uzalendo kwa nchi yao kwanza, kupiga vita vitendo vya kutoa na kupokea rushwa, kutumia kile kinachopatikana bila kuathiri kubomoa hazina nyingine isiyohusika.

Tena kutojilimbikizia mali kupita kiasi, na zaidi sana kila mmoja kujiona ana haki ya kuthaminiwa utaifa wake. Hapo maendeleo yaweza kupatika ‘ima fa ima’.

Nchi kama Rwanda, misingi yake ilishawekwa sawasawa na Rais Kagame, maendeleo yanayoonekana nchini humo ni kazi iliyofanywa kwa kudhamiriwa.

Ukiachana na marais wa Rwanda kama, Dominique Mbonyumutwa, aliyeiongoza Rwanda tangu Januari 28, 1961 mpaka Oktoba 26, 1961, Gregoire Kayibanda (Oktoba 26, 1961 – Julai 01,1962), kwa mara nyingine tena Gregoire Kayibanda (Julai 01, 1962-Julai 05,1973), Juvenal Habyarimana (Julai 05,1973-Aprili 06,1994), Theodore Sindikubwabo (Aprili 08,1994-Julai 19,1994), akiwa rais wa mpito, lakini Rais Pasteur Bizimungu (Julai 19,1994-Machi 23,2000).

Tangu mwaka 2000, amekuwapo Rais Kagame wa chama cha Rwanda Patriotic Front (RFP) mpaka leo.

Rais Kagame amekuwa akipendwa na wananchi wa Rwanda, hata kama kwa upande mwingine atazungumziwa vibaya kuwa ni katili, mbabe na mengineyo yenye sifa mbaya, lakini amechangia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo nchini humo na anapendwa sana.

Pia isisahaulike kuwa maendeleo iliyonayo leo nchi ya Rwanda, mwaka 1994 nchi hiyo iliingia kwenye historia ya kukumbukwa ya mauaji ya kimbari. Inakisiwa zaidi ya watu 500,000 walikufa.

Matokeo ya mauaji ya kimbari kama wanavyojua wengi, ndiyo yaliyoongeza kwa asilimia kubwa chuki zaidi kati ya Wahutu na Watutsi.

Rwanda isingetegemewa kuwapo na neno linaloitwa ‘amani’, lakini pia umoja na hatimaye wengi wangetegemea Rwanda ingesuasua na ingedidimia zaidi hasa kiuchumi.

Tofauti na fikra za wengi, Rwanda kuna maendeleo makubwa, ukilinganisha na Tanzania ambayo haijawa kwenye wakati mgumu kama ilivyo kwa Rwanda; zaidi Tanzania iliingia kwenye vita vya Uganda mwaka 1978 basi.
Maendeleo yanapatikanaje nchini humo? Pengine hili ndilo linekuwa ni swali la awali la kujiuliza.

Wafanyakazi nchini Rwanda ni wajibu wao, si kusukumwa kufanya kazi na huanza kazi saa moja asubuhi. Kazi hizo zikiwa ni kama vile ujenzi wa nyumba, barabara na kazi zingine zinazohusiana na maendeleo ya taifa.

Wanyarwanda, wamethubutu katika mambo mengi kama vile usafi na utii wa sheria bila shurti, hii ikiwa ni baina ya mtu na mtu, kaya hadi kaya na kuyajali mazingira kwa kutoharibu miundombinu wala kutotupa taka ovyo.

Hata hivyo, dhana ya uongozi bora anayoitumia Rais Kagame, imechangia kwa kiasi kikubwa kuifikisha Rwanda ilipo.
Taarifa za Rwanda kutajwa kwenye ripoti ya Benki ya Dunia, kama ni nchi iliyoboresha zaidi mazingira ya uwekezaji, ni jambo la kujivunia na kuonesha kuna kazi inayofanyika, na jitihada za kazi hizo zimeakisi duniani.

Kinachoonekana nchini Rwanda wafanyakazi wa serikali hawana nafasi ya kujiachia na ‘kutanua’ kwa kiwango cha juu, kama kutembelea magari ya kifahari.

Kwa Tanzania mameneja, wabunge na viongozi mbalimbali wa sekta tofauti tofauti, hujali kutumia magari ya kifahari kwa kile kinachodaiwa kuendana na hadhi yao.

Jambo lingine linayoifanya nchi ya Rwanda ikimbie kimaendeleo ni suala la usimamiaji mzuri wa vitendo vya rushwa. Rwanda haina mchezo kwenye suala la rushwa, kwa maana nzuri ni kwamba wana maanisha kutoka moyoni.

Katika suala la rushwa halina msamaha hata kidogo. Ukikamatwa unatoa au unapokea rushwa, hawasubiri mahakama itoe hukumu hutumika sheria ya papo kwa hapo.

Pamoja na kwamba Wanyarwanda huzungumza lugha yao kwa kiwango kikubwa, lakini sasa hivi mabadiliko yanaonesha kuwa Wanyarwanda huzungumza Kiingereza na Kiswahili vizuri.

Mbali na yote hayo, bado Rwanda ina waza mambo makubwa na ya mbele zaidi, kwa sasa Kichina hufundishwa Chuo Kikuu Cha Kigali, wakijua wazi kuwa Kichina ni lugha ambayo itaiteka dunia muda si mrefu, kwa jinsi uchumi wa nchi ya China unavyokimbia na kuleta ushindani mkubwa kwenye Umoja wa Nchi Tajiri Duniani (G8).

Tayari wanafunzi wengi wanasoma na wanaongea Kichina kiufasaha, hii ni ishara tosha ya uthubutu wa Wanyarwanda, wanatambua umuhimu wa kujifunza lugha nyingine muhimu.

Jambo kuu zaidi walilolifanya na linalotakiwa kuigwa na nchi zingine, ni pale Wanyarwanda walipoamua kuyapa kisogo yaliyotokea na kuangalia mbele.

Kitambulisho kikuu uingiapo nchini Rwanda ni usafi wa hali ya juu wa Jiji la Kigali.

Kama nilivyoongea hapo awali, ni marufuku kutupa takataka ovyo bali sehemu maalum zilizotengwa. Wao kila ifikapo Jumamosi ya mwisho ya mwezi, ni siku ya usafi na kila mtu anashiriki katika kufanya kazi za usafi, hili pamoja na sheria zimefanya tabia ya usafi ijengeke.

Sheria za usalama barabarani ni msumeno, kila anayeendesha pikipiki (bodaboda) imewekwa sheria kwamba ni lazima avae kofia ngumu, yeye pamoja na abiria.

Kinachofurahisha Rwanda, waendesha pikipiki wote hasa za kukodi wana namba na mavazi maalum kwa ajili ya kazi zao, hii inawafanya kutambulika kirahisi hata kwa mgeni hapati shida.

Usalama wa Rwanda ni jambo lingine ambalo linawashangaza wengi, wakati hapa nchini hali ya usalama ni tete, kiasi cha mtu kuhofia hata kuwa na kiasi cha fedha japo Shilingi milioni moja.

Rwanda hali haiko hivyo, suala la usalama linapewa kipaumbele cha hali ya juu. Iweje Rwanda iliyotoka kwenye vita na hali ya machafuko, iwe salama kiasi cha benki kufungwa saa nne usiku!

Kwa haya na mengine mengi. Ipo haja kubwa sana ziara ya Rais Magufuli, ilete tija na mabadiliko kwa kile alichojifunza kutokana huko.

Sidhani kama Rwanda ina kipaumbele cha kujenga mahakama na jela za mafisadi, kama kipaumbele kimojawapo na ahadi ya Rais Magufuli.

Nje na hapa nchi itaendelea kutoa mifano ya nchi zingine zilizoendelea, bila kuanza kuchukua hatua au kuiga mbinu na mafanikio ya nchi husika.

Rais Magufuli aanze sasa kuyatumia yale aliyojifunza nchini Rwanda, aachane na mahabusu, mahakama za mafisadi na kuanza kuangalia kinachowafanya watu wawe mafisadi, wezi, wala rushwa, wabadhilifu na madudu mengine mengi.

Mungu Iponye Tanzania!
0713/0765 937 378.
amwambapa7@gmail.com