Wadau hasa wabunge wa upinzani, watetezi wa haki za binadamu walishaona na kukosoa upungufu ambao ulitakiwa kurekibishwa kabla ya kuipitisha kwa hati ya dharura.
Wiki hii, asasi ya kimataifa ya Internews inayojihusisha na kuviwezesha vyombo vya habari na wanahabari wananchi kupata taarifa, iliandaa mjadala na wadau ambao ulilenga kujadili sheria hiyo pamoja na jinsi ya kutumia mitandao ya kijamii kwa usahihi kuwafikishia wananchi habari.
Katika mjadala huo, washiriki wakiwamo Baraza la Habari (MCT) na Mfuko wa Taasisi za Habari (TMF) walisisitiza kuwa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 ina upungufu mkubwa na kama ikiendelea kutumiwa inaweza kuifanya nchi kuwa adui wa matumizi ya mtandao wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) duniani.
Licha ya jitihada za kujenga mkongo wa taifa sheria hii ni adui wa uhuru wa kujieleza na inakiuka pia haki za binadamu, ilielezwa.
Watanzania wengi hawafahamu kuwa inawahusu lakini itamuathiri yeyote anayetumia mtandao wa intaneti, kifaa chochote cha mawasiliano iwe kompyuta kubwa au ndogo, vifaa vinavyofanya kazi kama kompyuta, simu za mikononi na televisheni, wajumbe wengi walionya.
Licha ya kwamba malengo ya sheria hii ni pamoja na kuainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta, utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kielektroniki na masuala yanayohusiana na hayo, matumizi ya mitandao kama Twitter, Instagram, JamiiForums, Facebook, tovuti, barua pepe, WhatsApp, blogu na data zote zilizo katika kifaa chochote cha kielektroniki yanaathiriwa na sheria hii.
IBARA TATA
IBARA YA 32-35
Ibara hizi zinamlazimisha mtoa huduma kutoa data za wateja wake kwa mkuu wa kituo cha polisi bila kibali cha Mahakama. Wakuu wa vituo vya polisi wamepewa nguvu nyingi na sheria hii!
Imependekezwa Mahakama ipewe mamlaka haya na si polisi, na ifanyike hivi baada ya kujiridhisha kuwa mwananchi anatakiwa kufanyiwa upekuzi, kuchukuliwa data zake au za wateja wake.
IBARA YA 39-45
Watoa huduma na wahifadhi tovuti wanalindwa na ibara hizi lakini kwa masharti. Katika ibara ya 39, Waziri anapewa mamlaka ya kuamua kipi ni kosa na kipi si kosa. Pia ana mamlaka ya kusimamisha na kusitisha huduma, kuondoa taarifa juu ya kitendo husika mfano, kulazimisha kuondoa mijadala yote ya ufisadi kama yeye ataona kwa mamlaka yake kuwa mjadala huo haufai kuendelea.
Ibara za 31-38 na ibara za 39-46 zinakinzana kwani kwa wakati mmoja mtoa huduma anaweza akawa ameona jambo, akalitoa na kujiandaa kuitaarifu mamlaka husika huku mamlaka hiyo hasa polisi ikiwa na uwezo wa kwenda kuchukua vifaa na data za mtoa huduma huyo.
Polisi imepewa kinga kubwa ambayo haiingiliani na sheria yoyote ile, ni hatari.
IBARA YA 7
Huu ni mkuki unaowajeruhi watumiaji vifaa vya mawasiliano vya kielektroniki. Kuanzia kifungu cha 1 hadi 3 cha ibara hii. Sheria haibainishi ni aina gani za data ambazo haziruhusiwi kuguswa ama kufutwa au zikiguswa au kufutwa ni kosa la jinai.
Katika ibara hiyo ya 7(1g), kipengele hiki kinarudiwa mara kadhaa katika bara za 32-35. Badala ya ibara za mbele kurejea ibara hii, watunga sheria wameiacha ibara hii ikiwa haieleweki hadi mtu asome ibara za mbele.
Wajumbe walihoji ni nani aliyeidhinishwa katika ibara na kipengele hiki?
IBARA YA 8
Muswada huu haujasema bayana iwapo nyaraka za siri zinaweza kuwekwa wazi katika mtandao kama zina maslahi ya nchi au wananchi. Kwa mfano, kuweka taarifa za matumizi mabovu ya pesa za umma kwenye mtandao. Ibara hii inanyima uhuru hata kama ni kwa maslahi ya nchi.
IBARA YA 14
Neno pornografia halijapewa maana na hivyo jambo lolote lenye mwonekano wa kiasherati (sexually vulgar) linaweza kutafsiriwa kama pornografia na kumuingiza muhusika mikononi mwa sheria.
Ponografia zote ni chafu lakini siyo kila kichafu ni ponografia. Hivyo kutokana na kuwa sheria hii inasema ponografia zote ni chafu hii itasababisha kila mtu ahukumiwe chini ya kifungu B.
Wana mjadala wanataka marekebisho yafanyike ili Uchafu na Ponografia viwe vipengele viwili tofauti.
FUNGU LA 15
Suala la kujifanya mtu mwingine kwenye mtandao (kuficha utambulisho), linaweza kuleta utata kwani kuna baadhi ya mitandao ambayo watumiaji hutumia majina bandia.
Itakuwaje watu kwa madhumuni mabaya wakitafuta mtu mwenye jina kama hilo na kumshtaki mtumiaji wa mtandao?
Walihoji je, mtu kujitambulisha kama mtu mwingine inahusisha kutumia jina lisilo lake hata kama hajajifanya mtu mwingine?
Wadau hao wanataka suala hilo likafafanuliwa kisheria kwakuwa ni jambo muhimu lakini wachache wataelewa manaa yake.
IBARA YA 16:
Katika kipingele hiki wadau wanaona utata kwa vile haifahamiki ni nani ana mamlaka ya kubainisha kuwa jambo lililowekwa kwenye mtandao ni la ‘ukweli, ‘uongo’ au ‘upotoshaji’? Wanaonyesha wasiwasi kuwa mamlaka zinaweza tumia hili kama mtego kwa manufaa yao.
Kipengele hiki kama vingine kimeambatanisha muda usiopungua bila kusema muda usiozidi. Hivyo mtuhumiwa anaweza kufungwa hata kifungo cha maisha kutokana na mamlaka ya mahakama.
Watu binafsi wanaweza kutumia vibaya kifungu hiki kuzuia uhuru wa maoni kwa kuwaburuza watumiaji wa mtandao mahakamani kila kukicha na kuwapotezea muda wao wa kazi na ikiwa mbaya zaidi ikibainika baadaye sana kuwa walionewa.
IBARA YA 20
Wajumbe wanaona kuwa katika mawasililano ya mtandao kama ilivyo mawasiliano mengine kuna ujumbe ambao mtu hawezi kuacha kuupata.
Mfano kutembea barabarani na kuona bango la matangazo, au kuwa ndani ya daladala iliyowasha redio.
Vivyo hivyo katika mtandao sio kila ujumbe anaopokea mtu ameuomba na hivyo kifungu hiki kinafanya kila atakayepokea ujumbe kuingia kwenye jinai.
IBARA YA 21(1)
Eneo jingine linalopigiwa kelele ni tofauti baina ya tafsiri za Kiswahili na Kiingereza. Upande wa Kiswahili unamlenga mtoa huduma wakati Kingereza unamlenga yeyote anayetumia mtandao.
Kwa upande wa Kiswahili inamlazimu mtoa huduma kumtaja mhusika aliyeweka ujumbe na pia kumuadhibu mtoa huduma huku tafsiri ya Kiingereza ya Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 inazungumzia kuhusu tafiti kwa ujumla. Kwa ujumla tafsiri ya Kiingereza ni nzuri lakini ya Kiswahili imepotoshwa na inavunja uhuru wa mawasiliano.
MUHIMU
Hakuna kinga yoyote kwa mtoa taarifa hivyo hata (whistle blowers) wako hatarini kwa mujibu wa ibara hii.
IBARA YA 22
Wajumbe wanaichambua ibara na kuhoji ni nani ana mamlaka ya kuamua kuwa ujumbe kwenye mtandao unatolewa au kuboreshwa kwa kusudi au bila kusudi?
Itambulike kuwa ujumbe wa kwenye mtandao huboreshwa kueditiwa au kufutwa wakati wowote muhusika anapoona inafaa maana mtumiaji huamua mwenyewe.
IBARA YA 23
Hii inahusika na unyayasaji wa mtandao au cyber bullying, lakini haujapewa maana.
Sheria inatakiwa kuweka bayana maudhi ya kihisia ni nini. Kwani mtu yeyote atakayeudhiwa ‘kihisia’ au kudai kuwa hisia zake zimeudhiwa anaweza kushtaki. Sio kila linalosababisha maudhi ya kihisia ni unyanyasaji.
IBARA YA 27
Wajumbe wanahoji ni nani anaamua kitendo fulani ni kula njama? Mazungumzo ya kawaida na maamuzi ya kukubalika na upande mmoja yanaweza kutafsiriwa kama kula njama na watu wa upande mwingine.
IBARA YA 31 (3A):
Kadhalika sheria ya Kiingereza inasema ‘as soon as practicable’ lakini ya Kiswahili inasema wakati wa upekuzi na ukamataji wa mali. Hizi zina maana tofauti.
Ibara hii inawapa mamlaka wakuu wa vituo vya polisi kufanya upekuzi na kuchukua vifaa vya kielektroniki vya mawasiliano na taarifa binafsi za raia bila amri ya mahakama. Hii ni hatari kwa vile kuna uwezekano wa kuharibu ama kukaa na kifaa cha mhusika bila kujali kuwa anakihitaji kwa ajili ya kuendesha maisha yake.
MADHARA
Hivyo kila Mtanzania anatakiwa kuwa mwangalifu iwe ni mkaazi wa kijijini, mjini, mwanahabari ama mjasiriamali kwa sababu anabanwa na Sheria ya Makosa ya Mtandao.
Kwa vyombo vya habari inakuwa vigumu kutafuta na kutangaza taarifa za kufichua uovu za kiuchunguzi mitandaoni. Pia inawezekana kupokonywa vifaa vya kielektroniki vya Tehema kwa muda usiofahamika hatua inayokwamisha uzalishaji.










