Lakini watu wengi wamekuwa wakidharau msemo huo kila wakati mpaka tatizo linapotokea na kusababisha athiri hata wakati mwingine kupoteza maisha, kama tunavyoona milipuko ya kipindupindu katika Visiwa vya Unguja na Pemba.
Ugonjwa huo umekuwa sugu Zanzibar tangu ulipoibuka Septemba 19 mwaka jana, katika maeneo ya Mjini Unguja na Pemba na kuenea hadi vijijini, tatizo hilo limejikita kikamilifu na sasa ni kam jipu lisilo na dawa.
Takwimu zinaonyesha watu 2,703 wameungua ugonjwa wa kipindupindu katika Visiwa vya Unguja na Pemba na kati ya hao 34 wamefariki sawa na aslimia 1.3 tangu kuibuka ugonjwa huo mwaka jana.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Wizara ya Afya Zanzibar asilimia 48 ya wagonjwa wanaofikishwa katika kambi za wagonjwa wa kipindupindu zinazoendelea kuongezeka walikuwa na hali mbaya na kusababisha matibabu kuwa magumu.
Wataalamu katika sekta ya afya akiwamo Mkurugenzi waKinga Dk Mohamed Dahoma, anasema wagonjwa wanaofikishwa katika kambi hizo ni watu wenye umri wa kati ya miaka ziro ambao ni watoto wachanga hadi wenye miaka 50 jambo ambalo limeleta wasiwasi mkubwa kwa wazazi kutokana na watoto kuwa miongoni mwa waathirika.
Takwimu zinaonyesha idadi ya wagonjwa walioripotiwa wanaume ni asilimia 52 wanawake asilimia 47 wakiwamo watoto walio chini ya umri wa miezi mitatu ambao ni asilimia 20 ya wagonjwa hao.
Idadi ya wagonjwa katika kambi ya Chumbuni kwa kipindi cha miezi mitano tangu kuibuka kwa maradhi hayo imeongezeka kutoka 10 mpaka 20 kwa wagonjwa wanaoripotiwa kwa siku katika kambi hiyo.
Wataalamu wa afya wanasema chanzo kikubwa cha uogonjwa huo ni kula kinyesi cha mgonjwa mwenye vimelea vya kipindupindu pamoja na jamii kuiishi katika mazingira machafu yenye taka maji na ngumu ambazo hukaribisha nzi.
Ugonjwa huo umepiga hodi katika vijiji vya Muungoni, Kitogani na Jozani katika mkoa wa Kusini Unguja na kuathiri wananchi katika maeneo hayo.
Bahati mbaya wakati kipindupindu kinaendelea kuenea kwa kasi katika maeneo mbali mbali kikitoka mjini na sasa vijijini, juhudi za usafi zinazochukuliwa na wananchi mitaani pamoja na vyombo vya kusimamia usafi haziridhishi, mathalani Baraza la Manispaa limeshindwa kusafisha masoko na kusababisha sehemu hizo kunuka.
Pamoja na kuwapo kwa viongozi kuanzia ngazi ya shehia, Wilaya, Mkoa na Maafisa Afya wa Mabaraza ya Miji hadi kwenye Halmashari, vyakula vimendelea kuuzwa katika mazingira machafu mitaani ikiwamo mishikaki na urojo huku wadudu kama nzi wakizagaa na kutua ovyo kwenye vyakula.
Tatizo la kuziba mitaro ya maji taka pamoja na kuibwa kwa mifuniko yake ya chuma na kuuzwa kama chuma chakavu na watumia dawa za kulevya, imechangia kwa kiwango kikubwa maji machafu yaliyochaganyikana na kinyesi kuzagaa mitaani.
Kukosekana uwajibikaji kwa viongozi na watendaji wakuu ni chanzo kingine cha kuenea ugonjwa wa kipindupindu na kupiga kambi Zanzibar na kusababisha watu wazima pia watoto kupoteza maisha.
Haiwezekani biashara za vyakula zifanyike mitaani katika mazingira machafu bila ya kuzingatiwa kanuni za afya huku serikali ikiendelea kulipa mishahara viongozi na watendaji wanaosimamia usafi katika maeneo ya biashara.
Hatua ya Wizara ya Afya kusambaza dawa za kinga za kipindupindu kwa wananchi badala ya kuchukua hatua za kuimarisha usafi wa mazingira pamoja na kusimamia kanuni za afya, ni kama kubeba maji kwa kwenye pakacha.
Ugonjwa wa kipindupindu Zanzibar ni jipu linalohitaji kutumbuliwa haraka na viongozi wakuu wa serikali ili kuepusha watu kuendelea kupoteza maisha kwa sababu za kukosa uwajibikaji wa viongozi na watendaji wachache.
Wakati umefika kwa watendaji wakuu kusimamia kwa vitendo kanuni za afya kwa sababu haiwezekani mtu kuishi katika nyumba bila kuwa na karo la maji machafu, au sehemu maalum ya kutupa taka bila ya kuchukuliwa hatua wakati anaumiza watu wengine.
Hatua za haraka za kuondoa ugonjwa wa kipindupindu zinahitaji hasa baada ya ugonjwa huo kuanza kujitokeza katika ukanda wa mashariki wakati eneo hilo muhimu kwa biashara ya utalii ambalo ndiyo nguzo ya uchumi wa Zanzibar.
Pamoja na juhudi zinazochukuliwa pia uwekaji wa dawa kinga katika visima vijijini unahitaji kufanyika kila mara baada ya kuwepo wasiwasi maji wanayotumia kuwa wananchi kuwa chanzo pamoja na kutoa elimu ya kuchemsha maji kabla ya kutumiwa.










