Baada ya kipenga cha mwamuzi kupulizwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Machi 19, mwaka huu, ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya US Monastir ya Tunisia, iliashiria kuwa klabu hiyo kongwe imeweka rekodi ya kutinga hatua hiyo kwenye kombe hilo tangu lianzishwe miaka 19 iliyopita.
Ikumbukwe kombe hilo lilianzishwa kwa mfumo huu wa sasa ambao unaanzia mtoano hadi makundi, baada ya ule wa mwanzo ambao ni mtoano hadi mwisho.
Kombe la Shirikisho barani Afrika lilianzishwa mwaka 2004, likichukua nafasi ya Kombe la CAF lililoanzishwa mwaka 1992 ambalo Simba iliingia fainali mwaka 1993 na kufungwa na Stella Abdijan mabao 2-0, likibadilishwa mfumo na kuuweka huu ambao leo tunaouona, tofauti na ule wa awali ambao ni washindi wa pili tu wa ligi ya nchi wanachama husika ambao walikuwa wakishiriki.
Kombe la CAF, ambalo lilijulikana sana kama Kombe la Abiola, likipewa jina la mfanyabiashara tajiri na mwanasiasa wa nchini Nigeria, Mashood Abiola.
Kabla la kuitwa hivyo lilijulikana kama Kombe la Washindi barani Afrika, ambapo pia washiriki wake ni timu zile zile zilizokuwa zikikamata nafasi ya pili kwenye nchi wanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (CAF), lilichezwa na mtindo ule ule wa mtoano mwanzo mwisho.
Kombe la Washindi lilianzishwa miaka 1975 na ndilo asili ya Kombe la Shirikisho tunaloliona leo, CAF wakilibadisha majina na mifumo kwenda Kombe la CAF na baadaye Shirikisho kutokana na mahitaji na mazingira.
Historia inaonesha kuwa Yanga imeshawahi kutinga robo fainali ya Kombe la Washindi mwaka 1995, na imesotea hatua hii kwa miaka 28 sasa.
Lakini haijawahi kutinga hatua ya robo fainali tangu lilipoanza kuitwa Kombe la CAF hadi Kombe la Shirikisho takriban miaka 30 iliyopita hadi mwaka huu ilipofanya hivyo.
Ilifanya majaribio kadhaa na kufanikiwa kutinga hatua za makundi, ilishindwa kutinga hatua ya robo fainali mara mbili 2016 na 2018 ilipofanikiwa kucheza hatua ya makundi, lakini ikiishia kukamata mkia.
Ilivyotinga robo fainali Kombe la Washindi
Miaka 30 iliyopita, Yanga ilicheza robo fainali ya Kombe la Washindi, ilipoanza raundi ya kwanza kwa kuifunga Vaal Professional ya Afika Kusini jumla la mabao 4-3, ikitoa sare ya mabao 2-2 ugenini na kushinda nyumbani 2-1 na mechi ya raundi ya pili ilicheza dhidi ya Cadets Club ya Mauritius, ikafanikiwa kushinda kwa jumla ya mabao 4-2, ikishinda nyumbani 3-1 na kulazimisha sare ya bao 1-1 ugenini na kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali mwaka 1995.
Hata hivyo, ilitolewa kwenye hatua hiyo kwa kuchapwa jumla ya mabao 4-2 dhidi ya Blackpool FC ya Zimbabwe, ikifungwa mabao 2-1 mechi zote mbili, nyumbani na ugenini.
Jaribio lililoshindikana mwaka 2016
Yanga ilitinga hatua ya makundi mwaka 2016, ikiitafuta robo fainali yake ya kwanza tangu kuanza kwa mfumo mpya wa Kombe la Shirikisho. Ilikuwa kwenye Kundi A, pamoja na timu za TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mo Bejaia ya Algeria na Medeama ya Ghana.
Haikufanikiwa, kwani ikiishia kukamata mkia kwenye kundi ikimaliza na pointi nne, ilizozipata kwa kuifunga Mo Bejaia bao 1-0 nyumbani na sare ya bao 1-1 dhidi ya Medeama Dar es Salaam, huku ikipoteza mechi nne, mabao 3-1 ugenini dhidi ya TP Mazembe na Medeama, bao 1-0 dhidi ya Mo Bejaia ugenini na idadi kama hiyo dhidi ya TP Mazembe nyumbani.
Ikashindwa tena mwaka 2018
Ilishindwa kwa mara ya pili kutinga hatua hiyo mwaka 2018, ilipotingia hatua ya makundi. Ikiwa kwenye Kundi D, safari hii ilikuwa pamoja na USMA Alger ya Algeria, Rayon Sports ya Rwanda, na Gor Mahia ya Kenya.
Kama mwaka 2016, ilimaliza ikiburuza mkia kwenye kundi hilo, ikiwa pia na pointi nne ilizozipata kwa kuifunga USMA Alger mabao 2-1 nyumbani, na suluhu dhidi ya Rayon Sports, huku ikipoteza mechi nne, ikichapwa nyumbani mabao 3-2 dhidi ya Gor Mahia, ugenini mabao 4-0, na idadi kama hiyo ya mabao dhidi ya USMA Alger, bao 1-0 dhidi ya Rayon Sports.
Historia imeandikwa 2023
Hatimaye mwaka huu, Yanga ikafanikiwa kutimiza azima yake ya kucheza robo fainali baada ya kushindikana miaka yote hiyo.
Kama ilivyokuwa mwaka 2018, ilipangwa Kundi D, pamoja na mechi ya kwanza kuchapwa mabao 2-0 dhidi ya US Monastir ugenini, ilirekebisha makosa, ikaifumua TP Mazembe 3-1 nyumbani, ikaenda kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Real Bamako ugenini kabla ya kuifunga nyumbani mabao 2-0 na kisha kupata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya US Monastir.










