Ni ziara ya kitaifa itakayokaribisha na kuvuta maofisa, wataalamu na waandishi wa magazeti na vyombo vyote vya habari vikubwa wanaotembea na msafara wa Harris, watakaoshuhudia Watanzania wakimkaribisha mgeni wao kwa bashasha za kila aina kuanzia mavazi, ngoma, nyimbo, michezo , vyakula na vinywaji kwenye dhifa ya kitaifa na popote Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, atakapotembea na mgeni wake.
Kesho mchana Makamu wa Rais Harris anaondoka Accra Ghana kwenye safari ya saa sita na kuifikia Dar es Salaam, akilitembelea taifa ambalo ni miongoni mwa nchi tatu za Afrika zinazowekeza katika demokrasia, haki za binadamu na maridhiano na hasa wakati huu ambao dunia inakabiliwa na mdororo wa kidemokrasia.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari kutoka mtandao wa Ikulu ya Marekani.
Inasema nchi hiyo inaiona Afrika kuwa muhimu katika kushughulikia changamoto za kimataifa kwa hiyo, ziara ya Mama Harris ni fursa nyingine ya kushauriana na kushirikiana na washirika kuhusu malengo ya pamoja.
Ujio wa kiongozi huyo ni mwendelezo kwa kuwa hapo awali Makamu wa Rais alikutana na viongozi wote watatu wa Afrika ambao anazuru nchi zao huko Washington nazo ni Ghana, Tanzania na Zambia na anatazamia kuimarisha ushirikiano wa Marekani na uhusiano wake na kila mmoja wa viongozi hawa katika safari hiyo.
AKIWA TANZANIA
Keshokutwa Alhamisi, anatarajiwa kukutana na Rais Samia, pia anaelezwa kuwa ataweka shada la maua kukumbuka shambulio la bomu katika Ubalozi wa Marekani mwaka 1998.
Baada ya jukumu hilo anakutana na wajasiriamali kwenye viatamizi ‘incubators’ vya sayansi na teknolojia’ kuzungumza nao kuhusu uwekezaji kwenye eneo hilo.
Makamu Harris kutembelea viatamizi ni kipengele kingine muhimu cha safari ambacho kinagusa eneo linalowekwa pembeni la ubunifu na ugunduzi unaofanyika Afrika .
Kuna ubunifu mkubwa lakini kutokana na kukosa fedha hakuna utafiti wala uendelezaji wa sekta hiyo wala sayansi na teknolojia kwa Afrika kwa ujumla.
Ubunifu wa kizawa au ‘indegenous’ ni muhimu na ndiyo ufunguo wa kutatua kero za jamii kubwa ya bara hilo inayoishi zaidi vijijini kwenye shida ya maji, kilimo cha jembe la mkono, wadudu waharibifu wa mazao, matumizi ya kuni na makazi duni.
Sayansi na ubunifu wa Afrika ukiendelezwa utaleta majibu ya changamoto hizo, badala ya kupachika teknolojia za magharibi.
Ugunduzi wa Afrika unathaminiwa endapo unafanywa kwa kushirikiana na wadau wa nchi zilizoendelea au mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Huu ndiyo wakati wa kufunguka na kuliweka suala la kuendeleza wataalamu wa ndani kwenye ikulu ya Marekani, wakati wa ziara ya Mama Harris.
Taarifa inayoelezea ziara yake, inasema mara nyingi teknolojia za kisayansi na ubunifu unaotokea Afrika hazizingatiwi na watafiti wa kimataifa au wa nje na kwamba safari yake inaweza kusaidia mabadiliko na kuongeza nguvu mpya kwenye sekta hiyo.
Ujio wa kiongozi wa Marekani kwa Tanzania ambayo ni moja ya nchi bora na ya kipekee kuanzia watu, uchumi, rasilimali nyingi, utalii, siasa na juhudi za kufikia maendeleo endelevu Kusini mwa Jangwa la Sahara, unafaa kuiangalia nchi hii kama kiungo cha mataifa sita yasiyo na usafiri wala huduma ya bahari.
Tanzania ni mlango unaoziunganisha nchi za DRC, Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia na Uganda na Bahari ya Hindi ikifungua na kuendeleza uchumi wa nchi hizo kila siku.
Kuimarisha miundombinu, utafiti wa pamoja ili kufikia ubunifu na teknolojia za kisasa za ndani ya mataifa hayo ni suala linalohitaji pia kuishirikisha Marekani.
Kwenye ukanda huo kuna changamoto kama magugu maji ndani ya maziwa, taka za plastiki na za kielektroniki kama vifaa vya kompyuta, simu, rimoti na runinga vilivyosheheni ndani ya maji na ardhini ni suala la utafiti, ubunifu na urejelezaji kuzungumzwa ili kwa pamoja nchi zijinusuru na athari za taka hizo.
Kuna taka za plastiki ambazo zinajaa baharini, ziwani na kwenye mito. Taifa linahitaji kutumia ubunifu na ugunduzi wa ndani wa kufanikisha kuziongezea thamani ikiwa ni pamoja na kuzalisha bidhaa bora zaidi kuanzia mbolea, vifaa vya nyumbani, mapambo na nishati.
Ziara ya Makamu Hariss izungumzie pia jinsi ya kutumia utaalamu wa ndani na kuendeleza juhudi za kupata teknolojia nafuu na ya kifanisi ya kutumia hifadhi ya gesi asilia , upepo, jua na taka ngumu kupunguza uharibifu wa mazingira hasa misitu.
Si vibaya kukumbushia ujio wa Rais Barack Obama, ulioleta pia miradi ya umeme na nishati ukipewa jina la Power Africa.
Power Africa imeshirikiana na Tanzania kupata nishati za jua, upepo na kusaidia kutatua shida ya umeme kwenye gridi ya taifa, lakini pia ukileta mwanga mpya kwenye uhifadhi wa mazingira na kupunguza uzalishwaji wa hewa ukaa.
Kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani Tanzania inaendelea kufaidika na mkakati wa kukidhi mahitaji ya umeme kwenye gridi ya taifa kwa sababu uzalishaji nishati ulitegemea maji ambao kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa si wa kutegemea tena.
Katika miaka ya hivi karibuni, vyanzo vikuu vya umeme nchini ni gesi asilia na Marekani amekuwa mshirika mkuu mfano, Kinyerezi II inayozalisha megawati 240.
Uzinduzi ukifanyika Aprili 2018 na miongoni mwa wataalamu ni wa washauri wa Power Africa waliofanya mapitio ya kina ya kiufundi ya upembuzi yakinifu wa mradi na kutoa msaada kwa TANESCO kwenye hatua na michakato ya uwekezaji.
Mradi wa Kigoma Solar Power wa megawati 5, ambao ni mtambo wa kuzalisha umeme wa jua huko Kigoma, taifa kwa msaada wa the U.S. Trade and Development Agency USTDA na OPIC na sasa unasambaza umeme kwenye gridi ya taifa.
Kinyerezi I mtambo wa gesi asilia unaozalisha MW 150, kituo kidogo cha kilovolti 132kV na njia za kusambaza umeme za msongo wa 220/kilovolti 132kV ili kuunganisha mtambo mpya wa umeme kwenye mtandao uliopo wa usafirishaji, usingejivunia mafanikio bila msaada wa USAID na kampuni ya Jacobsen Elektro ya Norway.










