Ilifanya hivyo kwa mara ya kwanza Machi Mosi, 2014 ilipoichapa Al Ahly ya Misri bao 1-0, mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwenye mechi ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Lilikuwa ni bao la Nadir Haroub 'Cannavaro' dakika ya 85. Katika mechi hiyo, Yanga ilitawala soka kwa kipindi kirefu, ikiishambulia mfululizo.
Katika mechi hiyo, kwa kiasi kikubwa mshambuliaji Emmanuel Okwi ndiye aliyekuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Al Ahly kiasi kwamba ili ilibidi akabwe na mabeki zaidi ya mmoja, tena kwa tahadhari kubwa.
Hata kwenye mechi ya marudiano Yanga ilipotolewa kwa mikwaju 4-3, ilipofungwa bao 1-0 nchini Misri, Okwi bado aliendelea kuwanyanyasa Waarabu hao.
Jumamosi ijayo Yanga inakwenda kucheza tena na timu hiyo hiyo ya Al Ahly Uwanja wa Taifa kwenye mechi ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, Yanga inakwenda kucheza bila ya baadhi ya wachezaji waliocheza mechi ya mwaka 2014, akiwemo Okwi ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa nchini Denmark.
Ingawa itakuwa na baadhi ya wachezaji kama Amissi Tambwe, ambaye ana kipaji cha ufungaji, na Donald Ngoma mshambuliaji mwenye kutumia nguvu na kusumbua mabeki, lakini kukosekana na mchezaji mwenye kipaji kama Okwi aliyeng'ara kwenye mechi zote na kuifanya Yanga kutolewa kwa tabu na vigogo hao, ni pengo.
Je, Yanga itaweza tena kuifunga Al Ahly Jumamosi kama ilivyofanya 2014 bila Okwi? Tusubiri tuone.
Wachezaji wengine watakaokosekana
Mbali na Okwi, wachezaji waliocheza kwenye mechi iliyochezwa Machi Mosi 2014 Uwanja wa Taifa na kutoa kichapo cha bao 1-0 kwa Al Ahly ambao hawapo tena na timu hiyo ni Frank Domayo ambaye kwa sasa anaichezea Azam FC, Mrisho Ngasa anayecheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini klabu ya Free State, Hamisi Kiiza ambaye kwa sasa yupo kwa mahasimu wao wa jadi Simba, Said Bahanuzi anayeichezea Mtibwa Sugar kwa sasa na Didier Kavumbagu ambaye anakipiga na Azam FC.
Wachezaji aliocheza mechi iliyopita baina ya timu hizo Uwanja wa Taifa na wakitarajia pia kucheza mechi ijayo ni pamoja na mfungaji wa bao 'Cannavaro', ambaye amerejea tena kwenye kikosi baada ya kuwa mejeruhi, Diogratius Munishi 'Dida', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Simon Msuva, na Haruna Niyonzima.
Wachezaji wapya watakaokumbana na Al Ahly
Baadhi ya wachezaji ambao hawakuwepo kwenye mechi ya 2014 na wanatarajia kucheza kwenye mechi ya Jumamosi ni pamoja na Tambwe, Ngoma, Thabani Kamusoko, Deus Kaseke, Geofrey Mwashiuya, Pato Ngonyani, Malimi Busungu, Paul Nonga, Haji Mwinyi na wengineo.
Rekodi za Yanga dhidi ya Al Ahly
Rekodi za Yanga dhidi ya timu za Waarabu hususan kutoka nchini Misri, inaanzia mwaka 1982 ilipopata kipigo cha mabao 5-0 mjini Cairo kutoka kwa Al Ahly katika raundi ya pili ya Klabu bingwa Afrika na mechi ya marudiano ikaambulia sare ya bao 1-1 jijini Dar es Salaam.
Mwaka 1988, Yanga ilikutana na Al Ahly tena katika Ligi ya Mabingwa na kutoka sare ya 0-0 mjini Mwanza, lakini ilikung’utwa mabao 4-0 katika mechi ya marudiano Cairo.
Mwaka 2009, Yanga ilijikuta ikipata tena kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Al Ahly.
Katika mchezo wa kwanza jijini Cairo Yanga ilifungwa mabao 3-0 na mashabiki wakapata matumaini kwamba Yanga ingeing’oa meno Al Ahly,i Dar es Salaam kwenye Ligi ya Mabingwa lakini ikachapwa bao 1-0.
Mwaka 2014, Yanga ikishinda kwa mara ya kwanza dhidi ya timu za Kiarabu kwenye Uwanja wa Taifa, lakini ikafa bao 1-0 nchini Misri na kutolewa kwa mikwaju 4-3 ya penalty.
Bahanuzi akikosa penalti ambayo ingewapeleka hatua ya makundi.
Kama Simba iliweza kuwavua ubingwa mabingwa watetezi Zamalek mwaka 2002 na kutinga hatua ya makundi, basi nina hakika hata Yanga wakija na mipango mizuri wanaweza kuing’oa Al Ahly.










