Maumivu haya yatavumilika Yanga, Azam FC?

04Apr 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Maumivu haya yatavumilika Yanga, Azam FC?

YANGA na Azam FC wamewasilisha barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakipinga marekebisho ya ratiba ya mechi za viporo vya Ligi Kuu Bara kwa timu hizo.

Msemaji wa Yanga Jery Muro.

Hata hivyo, hakuna uwezekano wowote wa Bodi ya Ligi kufumua tena ratiba hiyo kwa matakwa ya klabu hizo zinazoshiriki michuano ya soka Afrika.

Yanga inashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Azam FC wanashiriki Kombe la Shirikisho.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi TFF, Boniface Wambura alisema wamepokea barua kutoka klabu hizo zikitaka ratiba ya mechi za viporo kuangaliwa upya kwa vile inabana maandalizi yao ya mechi za kimataifa.

Wambura alisema siyo rahisi kwa bodi hiyo kupangua tena ratiba hiyo kutokana na ukweli kwamba muda ni mdogo.
Ni maumivu! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na marekebisho ya ratiba ya Ligi Kuu Bara na kuwalazimu wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Afrika mwaka huu, Yanga na Azam FC kucheza mechi nne ndani ya siku 10.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), ilitangaza kuipangua tena ratiba ya ligi hiyo kwa kuzingatia mechi za viporo za timu hizo zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Ratiba mpya inaonyesha kuwa timu hizo zitacheza mechi nne ndani ya siku 10 kuanzia Aprili 3-13 baada ya kuzikabili Ndanda FC na Prisons jijini kwenye Kombe la FA.

Huku wakihitaji muda mzuri wa maandalizi wa mechi yao mbili ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Esperance itakayochezwa Chamazi Aprili 10, Wanalambalamba watacheza mechi tatu ndani ya siku saba dhidi ya Prisons, Toto na Ndanda kabla ya kuikabili timu hiyo ya Ligi Kuu ya Tunisia.

Yanga nao wanakabiliwa na mtihani uleule, wakati wakijiandaa kuchuana na Al Ahly Aprili 9 katika hatua ya 16-Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Wanajangwani wanatakiwa kucheza mechi tatu -- moja ya Kombe la FA dhidi ya Ndanda FC na mbili za viporo vya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar na Mtibwa Mtibwa -- kabla ya kuwavaa wababe hao wa Misri.

SIMBA WACHEKELEA
Wakati maumivu yanaonekana dhahiri kuzinyemelea Yanga na Azam FC, wapinzani wao katika mbio za ubingwa, Simba wameeleza kufurahishwa na uamuzi wa TFF kupangua tatiba ya Ligi Kuu.

Zacharia Hanspoppe, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Simba, alikaririwa jana na moja ya mitandao ya kimataifa ya michezo akisema: "Azam na Yanga watakula jeuri yao".

"Hatukatai Azam na Yanga kupewa muda wa maandalizi wa mashindano yao ya Afrika, lakini huko nyuma walikwishakosea kwa kwenda kucheza bonanza na kuacha ligi.

"Matokeo yake sasa wanazidi kulundikiwa mechi za viporo na kupoteza ladha ya ligi. Kwa kuwa walikaidi mawazo ya timu nyingine, sasa wacheze mechi za Ligi Kuu."

Simba, mabingwa mara 18 wa Tanzania Bara, ndiyo wanaongoza msimamo wa ligi hiyo kwa sasa wakiwa na pointi 57 baada ya mechi 24, pointi saba mbele ya Yanga na Azam waliocheza mechi 21.

MECHI ZIJAZO ZA YANGA, AZAM
Yanga vs Ndanda Machi 31
Yanga vs Kagera Aprili 3
Yanga vs Mtibwa Aprili 6
Yanga vs Al Alhy Aprili 9
Yanga vs Mwadui Aprili 13
--------------
Azam FC vs Prisons Machi 31
Toto vs Azam FC Aprili 3
Azam FC vs Ndanda Aprili 6
Azam FC vs Esperance Aprili 10
Mtibwa vs Azam FC Aprili 13