Kikosi cha kwanza cha Yanga kinavaana na Al Ahly kikiwa na beki Kelvin Yondani pekee mwenye uelewa wa presha na ugumu wa mechi hiyo dhidi ya mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Yondani amebaki kuwa mchezaji pekee aliyedumu kwenye kikosi cha Yanga tangu aliposajiliwa akitokea Simba mwaka 2013.
Yondani hajawahi kusugua benchi au kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha hivyo ni wazi kuwa yeye na kocha Hans Van Der Pluijm ndiyo wenye uelewa mkubwa wa jinsi ya kucheza dhidi ya Al Ahly.
Kikosi cha sasa ambacho kinaaminiwa na Kocha Pluijm kina wachezaji wa tofauti wengi na wale wa mwaka 2014. Mara nyingi Pluijm huwa ana panga kikosi chake hivi; Mustafa Ali ‘Barthez’, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Vicent Bosou, Kelvin Yondani, Pato Ngonyani/ Mbuyu Twite, Deus Kaseke/ Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Donald Ngoma, Haruna Niyonzima/ Godfrey Mwashiuya.
Wakati awali kikosi chake kilikuwa hivi wakati huo wakicheza dhidi ya Al Ahly 2014: Deogratius Munishi ‘Dida’ (benchi), Mbuyu Twite (benchi), Oscar Joshua (benchi), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (majeruhi), Kelvin Yondani (kikosi cha kwanza sasa), Frank Domayo (amehama), Simon Msuva (benchi), Mrisho Ngasa/Athumani Idd 'Chuji' (wamehama), Didier Kavumbagu (amehama), Emmanuel Okwi (amehama) na Hamis Kiiza/ Said Bahanuzi (wamehama).
Kocha Pluijm alisema, “Tunaenda kucheza na timu nzuri ya Al Ahly, maandalizi ndiyo kila kitu kwetu. Kama tuliweza kwa APR ambao hatukuwafahamu vizuri kwanini nishindwe dhidi ya Al Ahly ambao nimekuwa nikicheza dhidi yao mara nyingi wakati nazifundisha timu za Afrika.
“Nilipokuwa na Chelsea ya Ghana niliwahi kucheza dhidi ya Al Ahly, Pia nikiwa hpa Yanga nimewahi. Nitatumia ujuzi wangu kuona jinsi gani ninautumia kwa wachezaji ili tuweze kushinda. Nina Imani kuwa Ah Ahly wamebadili wachezaji wengi kama tulivyofanya sisi kwa miaka ya hivi karibuni,” alisema.
Katika hatua nyingine, Yondani alisema, “Tutapambana mpaka dakika ya mwisho, tutahakikisha tunapata matokeo na kuiwezesha Yanga kwenda kwenye hatua inayofuata.
Naamini ushirikiano miongoni mwetu utatubeba. Mara ya mwisho Yanga ilipoondolewa na Al Ahly kjwenye kombe la mabingwa wa Afrika in mwaka juzi ambapo Yanga ilikubali kipigo cha penalti 4-3 baada ya timu hizo kuwa zimemaliza mechi mbili kwa sare ya 1-1. Hii ni baada ya kushinda 1-0 jijini Dar es Salaam na kisha kufungwa 1-0 na Al Ahly kule Misri.










