Msimu huu wa 2015/16 beki wa kulia Shomari Kapombe ameweka rekodi ya pekee ya kufunga magoli manane mpaka sasa.
Beki hiyo wa zamani wa Polisi Morogoro na Simba, anatajwa kuwa ni mmoja wa wachezaji wanaoweza kuibuka kuwa mchezaji bora wa mwaka msimu huu.
Kwa kile kinachoonyesha kuwa amekuwa mahiri kwenye ufungaji, amekuwa akiisaidia Azam FC kufunga magoli kwenye michuano mingine, ikiwemo ya kimataifa.
Magoli yake ya Ligi Kuu aliyofunga kwenye mechi dhidi ya Coastal, Azam ikipata ushindi wa mabao 2-0, lingine likiipa ushindi wa bao 1-0 timu yake dhidi ya Ndanda, akafunga mawili Azam ikiibwaga Toto Africans mabao 5-0, moja likiipa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.
Mechi nyingine ilikuwa dhidi ya Mgambo Shooting alipofunga mabao yote mawili, Azam ikishinda 2-1 na bao pekee ikishinda 1-0 dhidi ya Stand United.
Na kwa hali inayoendelea, inawezekana kabisa akaweka rekodi ya aina yake ya kufunga zaidi ya magoli 10 kwenye Ligi Kuu, ikawa ni rekodi ya aina yake tangu ligi ya Tanzania ianzishwe mwaka 1965.
Mwandishi wa habari hizi anakusanya majina ya mabeki waliowahi kupachika magoli mengi kwenye Ligi Kuu kwa msimu tofauti.
1. Said Swedi-Coastal (magoli sita) 2011/12
Wakati Kapombe akiwa na magoli manane hadi sasa, kulikuwa na beki mmoja anayecheza namba kama yake anaitwa Said Swedi.
Yeye msimu wa 2011/12 alimaliza ligi akiwa amepachika mabao sita, akiichezea Coastal Union.
Alikuwa ndiyo kwanza ameihama Simba na kuwa beki aliyefunga magoli mengi msimu huo.
2. Juma Abdul-Toto Africans (magoli sita) 2009/10
Ni Juma Abdul huyu anayeichezea Yanga kwa sasa.
Siyo kama anabahatisha kufunga mabao, kwani ameanzi mbali. Akiwa Toto Africans msimu wa 2009/10 kabla ya kwenda Mtibwa Sugar alimaliza msimu akiwa na magoli sita.
Idadi hiyo ilimfanya kuwa beki aliyefunga magoli mengi msimu huo
3. Tumba Swedi-Ashanti (magoli matano) 2013/14
Ni ndugu na Said Swedi. Kwa sasa anaichezea Mbeya City. Msimu wa 2013/14 alimaliza kinara kwa upachikaji magoli upande wa mabeki. Alimaliza msimu huo akiwa na magoli matano.
4. Mbuyu Twite-Yanga (magoli manne) 2012/13
Msimu wa 2012/13 beki Mbuyu Twite wa Yanga alimaliza msimu akiwa na magoli manne.
Idadi hiyo ndiyo ilikuwa ya juu zaidi kufungwa na mabeki msimu huo.
Raia huyo wa Rwanda kwenye asili wa DR Congo hucheza namba zote za nyuma na alikuwa bado hajaanza kuchezeshwa namba sita, kama ambavyo alivyokuwa akitumika msimu uliopita.
5. Nadir Haroub-Yanga (magoli manne) 2012/13
Ni beki wa kati mkongwe kabisa nchini ambaye msimu wa 2012/13 alikuwa miongoni mwa mabeki waliomaliza ligi msimu huo wakiwa wamefunga magoli matano.
Hiyo ilikuwa ndiyo idadi kubwa ya magoli kufungwa na mabeki msimu huo, Cannavaro akiwa na mwenzake Twite ndiyo walikuwa vinara.
6. Lugano Mwangama-Prisons (magoli manne) 2014/15
Ni beki wa kati wa Prisons ambaye msimu uliopita 2014/15 alikuwa kinara kwa upachikaji wa magoli kwa wachezaji anaocheza nafasi ya ulinzi.
Alifunga jumla ya magoli manne na kuwa beki aliyefunga magoli mengi msimu huo.
7. Jimmy Shoji-AFC (magoli matatu) 2010/11
Alikuwa beki machachari wa AFC ya Arusha iliyocheza Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya kushuka.
Shoji aliibuka kuwa beki aliyefunga magoli mengi msimu wa 2010/11 akipachika magoli matatu ambayo hayakufikiwa mlinzi mwingine kwenye ligi hiyo.
8. Said Koko-Moro United (magoli mawili) 2008/09
Msimu huo wa 2008/09 ulikuwa mbaya kwa mabeki, kwani waliofunga idadi kubwa ya magoli, walifikisha mawili tu.
Wote hawa waliongozwa na Said Kokoo alikuwa ameihama klabu ya Simba na kujiunga na Moro United aliyemaliza ligi akiwa amefunga magoli mawili, pamoja na mabeki wengine toka timu mbalimbali.
Wachezaji hao waliofunga magoli mawili msimu huo ikiwa ndiyo idadi kubwa ya magoli kwa mabeki mbali na Kokoo ni Buji Selemani (JKT Ruvu), Juma Nade (Toto Africans), Martin Lupati (Villa Squad), Henry Mwalugala (Prisons), Davis Naftari (Simba), na Sudi Abdallah (Mtibwa).










