Haikuwa rahisi kwa mtu kuamini mara moja kama kweli kocha huyo anaweza kufanya kazi kipindi chote hicho bila kulipwa mshahara na mwajiri wake - Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Malimbikizo hayo sasa yamefikia Sh. milioni 200. Inasikitisha.
Katika maelezo yake, mkwasa mchezaji wa zamani Yanga na Taifa Stars, alisema kwa kipindi chote hicho alikuwa akilindwa na uzalendo.
Kwamba, aliamua kufanya kazi bila kulipwa mishahara yake kutokana na mapenzi na uzalendo mkubwa alionao kwa timu ya taifa.
Kwa kuzingatia, yeye mwenyewe aliwahi kucheza timu ya taifa, kwake ilikuwa rahisi kuweka utaifa mbele kuliko kudai haki yake.
Makocha wachache wanaweza kufanya hivyo. Iko mifano mingi. Tumeshuhudia makocha wazalendo wa nchi kama Nigeria wakitishia kuicha timu kwa sababu tu ya kutolipwa mishahara au haki zao nyingine.
Uzalendo wa Mkwasa ulilenga kuishtua TFF baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu bila kusema lolote kuhusu haki za kocha Mkwasa.
Naamini, kauli ya Mkwasa imekuja baada ya kutoona lolote likifanywa na TFF. Kwa wanaomjua Mkwasa, watakubaliana na mimi kuwa siyo mtu wa kulalamika.
Lakini inapofikia hatua ya kulalamika, basi ni wazi TFF walijisahau kupita kiasi na kuliona suala la kudaiwa ni la kawaida.
Kwanini? TFF ina madeni kila sehemu. Ndani ya shirikisho hilo, fedha ni tatizo kubwa kuweza kulielezea.
Pengine kutokana TFF kuwa wazoefu wa kudaiwa, inawezekana pia ndicho kilichowafanya kuibadilisha haki ya Kocha Mkwasa kuwa deni.
Sasa leo kocha huyo anadai milioni 200, TFF watapata wapi fedha za kumlipa, wakati huohuo ina deni la zaidi ya Sh. bilioni 1 lililotokana na kukwepa kulipa kodi.
Mwishoni mwa mwaka jana, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ilizifungia akaunti za shirikisho hilo kwa madai ya kutolipa malimbikizo ya kodi.
Hadi sasa haieleweki suala hilo limefikia wapi, zaidi ya kuelezwa kuwa kuna mazungumzo yanafanyika na huenda wakafikia muafaka.
Lakini kabla hata ya kufikia muafaka uliodaiwa na TFF, mwanzoni mwa wiki iliyopita, TRA ilikamata mali za shirikisho hilo kwa madai yaleyale ya kukwepa kodi.
Wakati Mkwasa akionyesha uzalendo na kuendelea kufanya kazi bila kulipwa mishahara, kwa TRA ni tofauti. Hawataki uzalendo pamoja na kutambua kuwa shirikisho hilo ni mali ya Watanzania.
TRA wanasimama kwenye kanuni na sheria za ukusanyaji wa kodi kwa maendeleo ya nchi. Lakini Mkwasa, alisimama kwenye uzalendo.
Ni swali la kujiuliza, kama angekuwa kocha wa kigeni angeweza kuvumilia kama alivyofanya Mkwasa? Jibu liko wazi, isingekuwa rahisi.
Hii inatoa picha kwamba, TFF haina tena uwezo wa kuajiri kocha wa kigeni na kumlipa wenyewe bila msaada kutoka nje yao.
Utawala uliotangulia wa Rais Kikwete, haukuwa na shida kuchukua jukumu la kulipa mishahara ya makocha wa Stars.
Lakini sasa mambo yamebadilika. Kila mmoja ale kwa urefu wa kamba yake. TFF kama taasisi lazima isimame yenyewe.
Kama TFF itaendelea kukosa ubinifu wa kusaka vyanzo vingine vya fedha na kuendelea kutegemea asilimia za viingilio vya uwanjani kujiendesha, hakika inakwenda kupotea.
Kwa staili hii, TFF hii chini ya Jamal Malinzi haitapona kutoka kwenye mlolongo wa madeni. Itakuwa taasisi ya madeni na siyo kuongoza soka.
Kwanini viongozi wetu siyo wabunifu? Shirikisho kubwa kama hilo linashindwaje kujisimamia kuendesha soka la Tanzania?
Katika zama hizi ambazo mchezo wa soka siyo tena burudani tu, TFF inaendelea kukumbatia utamaduni wa kizamani wa kuufanya mchezo wa soka kuwa wa burudani peke yake.
Hivi kweli TFF yetu haifahamu kuwa soka ni kiini cha ajira? Haifahamu kuwa mchezo wa soka ni kisima cha kuzalisha mapato?
Kwanini TFF isije na ubunifu wa kuleta ushindani kwenye mchezo wa soka? Wako wapi viongozi wetu? Kila kukicha ni malalamiko tu?
Tukiendelea kuishi kwa kupenda kuota ndoto za mafanikio, ambayo hayapo kimsingi, maana yake tunajitumbukiza kwenye kiza.
Huu siyo wakati wa kufanya mambo kwa mazoea, TFF hii iamke sasa. Ione kero kulalamikiwa ndani na nje ya uwanja. TFF ya Malinzi ione aibu kudaiwa.
Kauli ya Malinzi kwamba wamechanganyikiwa baada ya Chad kujiondoa kwenye mashindano ya kusaka tiketi ya kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika na kuwatia hasara na hatua ya TRA kukamata magari matano mali ya TFF, inaonyesha mwisho wa upeo wa kujikomboa.
Nilidhani, badala Malinzi kusema: 'tumechanganyikiwa', alipaswa kuja na kauli inayolenga kwenda kutatua tatizo lililopo.
'Kuchanganyikiwa' siyo dawa ya kutatua tatizo, bali ni mwendelezo wa tatizo.
Ni kweli TFF ya sasa iko kwenye wakati mgumu kutokana na kuandamwa na malalamiko kila siku na madeni yasiyokuwa na mwisho.
Hata hivyo, wana nafasi na wanaweza kuondoka kwenye hali hiyo kama viongozi wakaonyesha dhamira ya dhati ya kuleta mageuzi ndani yao.










