Licha ya nafasi hiyo ya kutoa elimu moja kwa moja darasani,kufanya utafiti na ushauri wa kitaaluma, pia amewahi kuwa Ofisa Taaluma Mkuu wa UDSM katika miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000 aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Juu katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Kwa msingi huo,si ajabu sana akajitokeza kwa namna moja au nyingine katika kilio kinachoitikisa taaluma nchini, hususan katika somo la hisabati na ‘binamu’ zake wa karibu masomo ya sayansi.
Na hiyo ndivyo ilivyokuwa hivi karibuni katika maadhimisho ya miaka 20 ya Kitivo cha Sayansi cha chuo hicho na Prof.Massenge alikuwa na maoni yake kuhusu kilio chake cha eneo hilo la taaluma ambako yeye amebobea.
Kimsingi, masomo ya sayansi ni moja kati ya masomo ambayo wanafunzi wengi wamekuwa wakiyakimbia kwa madai ya kwamba ni magumu sana.
Hiyo inadaiwa kuchangia uchache wa wanasayansi wengi nchini na kusababisha nchi kutegemea wataalamu wa masuala ya kisayansi kutoka nje ya nchi.
Prof. Ralph Masenge mwanataalum wa hisabati kutoka Kitivo cha Sayansi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CoANS) anasema kuwa wanafunzi wamekuwa waoga kusoma masomo ya sayansi kutokana na ukosefu wa vifaa vya kujifunzia.
Anasema kuwa, uhaba wa vifaa vya kujifunzia kama maabara za kisasa na uchache wa vifaa mbalimbali vya kujifunzia kama kemikali ndio kikwazo kikubwa kwa wanfunzi kusoma masomo hayo.
“Unajua sayansi ni vitendo, yaani unaonyesha vitu uhalisia na sio kusoma kwa nadharia , kwa hiyo inahitajika wanafunzi kusoma kwa vitendo zaidi.
“Sasa wanafunzi wengi wamekuwa wakiona masomo hayo magumu kutokana na kusoma kwa nadharia na si kwa vitendo hivyo serikali ilione hilo.
Prof. Masenge anasema ,kati ya Machi 29 hadi Aprili Mosi chuo hicho kimeadhimisha miaka 20 ya Kitivo cha Sayansi ambacho kilianzishwa mwaka 1996 kwa ajili ya kuongeza chachu ya wanafunzi kuchukua masomo ya sayansi.
Kwa uzoefu wake anasema tangu ameanza kufundisha masomo ya sayansi, amegundua kuwa Tanzania inaweza kuzalisha wanasayansi wengi nchini kama wataweka mkazo katika kuboresha miundombinu ya masomo hayo.
“Tunafahamu kuwa, bila sayansi na teknolojia hakuna maisha duniani, hivyo tunahitaji kuongeza chachu kwa wanafunzi tangu wakiwa shule za msingi na sekondari kupenda masomo haya ili tuweze kupata wataalamu wengi nchini,”alisema Prof. Masenge
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Idara ya Elimu Mimea, Dk.Amelia Buriyo anasema kuwa, masomo ya sayansi yanahitaji utulivu wa hali ya juu na kubwa zaidi ni kuwa na vifaa ya kutosha.
“Ujenzi wa maabara nyingi pekee haitoshi , kwenye hizo maabara inatakiwa kuwepo vifaa vyote ikiwemo kemikali na vitu vyingine vitakavyowawezesha wanafunzi kusoma kwa vitendo,”anasema Dk Buriyo
Mhadhiri huyo anaongeza kuwa, kwa sasa katika idara yao ya sayansi kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi jambo ambalo haliendani mazingira yaliyopo.
Anabainisha kuwa, wanafurahia ongezeko kubwa la wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi nchini, lakini tatizo ni mazingira ambayo si rafiki kwa wanfunzi hao.
“Kwa mfano sasa hivi chuoni kwetu, kumekuwa na ongezeko kubwa jambo ambalo linasababisha kuchukua wanafunzi mia tatu kwa mwaka na ukiangalia maabara zetu haziwezi kukidhi idadi ya wanafunzi hao,” alibainisha
“Utakuta wanafunzi 10 wanatumia kifaa kimoja, jambo ambalo linachangia kuzalishwa wanasayansi ambao hawana viwango vile vya kimataifa,”anaendelea kusema
Dk. Buriyo anawatoa hofu wanafunzi kuwa, masomo hayo si magumu ila yanahitaji umakini wa hali ya juu na mazoezi ya kutosha mara kwa mara, hivyo wajitokeze wengi kusoma masomo hayo.
Hata hivyo, anaiomba serikali na wadau mbalimbali wa elimu nchini kusaidia sekta ya elimu hasa katika upande wa sayansi kwani una changamoto nyingi’
“Pia ifahamike kuwa, uwezo wetu wa kufundisha masomo haya ni mzuri sana na unaweza kutoa wanafunzi wenye viwango vya kimataifa kabisa, kama miundombinu ya kufundishia itaboreshwa,” alifafanua Dk. Buriyo
Mbali na hayo, Mkuu wa CoNAS, Thomas Lymo anasema katika kuelekea sherehe za miaka 50 ya kitivo hicho wana mambo mengi ya kujivunia licha ya kuwepo kwa changamoto nyingi.
“Katika miaka 50 chuo kimeweza kutoa wanafunzi 3,900 ambao kwa sasa wanafanya kazi katika taasisi na mashirika mbalimbali ya binafsi na serikali,” anasem Prof. Lymo
“Kwanza Rais ni mmoja wa aliyekuwa mwanafunzi wa masomo ya sayans katika chuo hiki, hivyo tunaamini anafahamu changamoto zilizopo hivyo na tuna imani atazishughulikia,”alisema
Aidha anasema sayansi ni majaribio hivyo inahitajika bajeti kubwa, kwani kuna mambo mengi ya kufanya ili wanafunzi wanaozalishwa wawe na viwango vinavyohitajika.
Vilevile anasema kwa sehemu kubwa, wamekuwa wakitegemea msaada wa serikali na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi katika kutoa ufadhili wa wanafunzi kusoma nje kwa ajili ya kupata wanafunzi wenye kiwango cha kimataifa.
Anasisitiza kuwa, serikali inatakiwa kutenga kiasi cha fedha kitakachowezesha kuendeshea shughuli mbalimbali za chuo hicho kwa ajili ya kupata watalaamu wa masuala mbalimbali hapa nchini.










