Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau wa elimu kwa kushirikiana na serikali ili kuhakikisha watoto wanafanya vizuri katika mitihani yao, bado wanafunzi wengi wanaendelea kufanya vibaya.
Zipo sababu mbalimbali zinatajwa kuwa, zimekuwa zikichangia watoto wengi kushindwa mtihani wa somo hilo. Hata hivyo, sababu kubwa zaidi ya zote ni kutokuwapo kwa msingi imara wa kuwawezesha watoto kushinda somo hilo, kuanzia shule za msingi na uhaba wa walimu wa hisabati.
Maria Kipaka ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Rwazi iliyoko katika manispaa ya Bukoba. Anataja sababu za watoto wengi kushindwa somo hilo katika mitihani ya taifa, kuwa ni uhaba wa walimu wa hisabati kuanzia katika shule za msingi hadi sekondari.
Maria anatoa mfano wa shule yao kwamba ina mwalimu mmoja anayefundisha somo hilo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Hali hiyo, inawapa mashaka wanafunzi kama wataweza kufaulu somo hilo, kutokana na mwalimu kuelemewa na mzigo hata kushindwa kupata muda wa kutosha wa kufundisha.
Sababu nyingine anasema ni wanafunzi hawapendi kusoma hisabati wamekata tamaa kwa sababu ya kusikia ndugu, wazazi na viongozi wanaowategemea wakisema somo hilo ni janga la kitaifa.
“Kama waliotutangulia wanatwambia hili somo ni janga la kitaifa wakimaanisha sio rahisi kushinda, mwanafunzi anaona kwa nini apoteze muda kusoma somo ambalo hawezi kushinda, anaachana nalo na kuendelea kusoma masomo mengine” anasema
Wengi wanaoogopa kusoma somo hilo anasema kuwa ni watoto wa kike wanaoona kuwa ni somo la wanaume. “Tumejenga fikra kuwa kila kitu kinachoonekana ni kigumu inabidi kifanywe na mwanaume, na katika hisabati hali iko hivyo,” anasema.
Maria anayechukua masomo ya sayansi, anaona ili kukabiliana na tatizo la watoto wengi kushindwa mtihani wa hisabati, serikali iwezeshe kuwapo kwa walimu wa kutosha kufundisha somo hilo kuanzia shule za msingi, ili watoto wakue wakilifahamu na kulipenda somo hilo.
Anasema pia wanafunzi wanaofanya vizuri katika somo hilo hata katika mitihani ya kawaida isiyo ya kitaifa wapewe motisha shuleni na nyumbani, ili kuwafanya waongeze bidii kusoma hisabati, maana mtoto atajua asipofanya vizuri hatapata zawadi.
“Walimu wanaofundisha vizuri hisabati nao wapewe motisha ili kuwaongezea moyo wa kuwafundisha watoto somo hili.Pia waboreshewe maslahi yao na kulipwa kwa wakati, ili wanapoingia darasani wawaze kuwafundisha watoto badala ya kuwaza madeni wanayoidai serikali,” anasema.
Maria anaona kwamba kama mwanafunzi wa kike ni tofauti na wanafunzi wengine ambao wamejenga woga wa jumla wa kuogopa somo hilo, ili kuthibitisha hilo anasema sasa amejiwekea utaratibu wa kufanya angalau maswali mawili kila siku ya hisabati. Anasema bila kuweka jitihada binafsi sio rahisi kushinda somo hilo.
“Ili niweze kufaulu masomo yangu ya sayansi, huwa najitahidi kufanya mazoezi ya mara kwa mara hasa kwa masomo ya hisabati na fizikia, nawasumbua sana walimu na wanafunzi wenzangu ambao wana ufahamu mkubwa wa somo hili, ili wanifundishe ambacho sijakielewa” anasema.
Said Kombo ni mwalimu wa taaluma katika shule ya sekondari Hamugembe iliyoko pia katika manispaa ya Bukoba, anataja sababu mbalimbali zinazochangia watoto wengi kushindwa kufanya vizuri mtihani wa hisabati kuwa, ni wanafunzi kulichukulia kama somo gumu kuanzia ngazi za chini.
“Kwa hiyo watoto wanakua wakijua kuwa hisabati ni somo gumu, kwa hiyo wengi hukimbilia kusoma masomo ya sanaa na kuikimbia sayansi, na kawaida mwanafunzi anayekuwa na mwanzo mzuri wa hisabati ndiye huendelea vizuri tofauti na mwenye mwanzo mbaya” anasema.
Kombo anasema kuwa, mtoto anamaliza elimu ya msingi hafahamu hisabati kabisa kwa hiyo akijiunga na elimu ya sekondari anaacha kulifuatilia somo hilo.
Anasema kuwa siku hizi wanapelekewa wanafunzi ambao uwezo wao kitaaluma ni mdogo, hata wakifundishwa kuelewa kwao ni shida, na kutoa mfano wa mwaka 2014 ambao walipokea wanafunzi wenye alama 67 na kuwa mwanafunzi wa hivyo kumfundisha hasa hisabati inakuwa shida kuelewa.
Bado anaona tatizo la wanafunzi kutumia lugha ya Kiswahili katika shule za msingi na baadaye kulazimika kutumia lugha ya Kiingereza ni changamoto kubwa, na kuwa inaweza kuwa inachangia asilimia 60 ya wanafunzi wanaofeli.
“Lugha ndiyo msingi wa mawasiliano ina maana kama mwalimu na mwanafunzi hawaelewani itakuwa vigumu mwalimu kumfundisha mwanafunzi akaelewa haraka” anasema.
Anasema kuwa hata muda wa majuma sita wa kumfundisha mtoto kumtoa katika lugha ya Kiswahili kuelekea katika matumizi ya Kiingereza ni mfupi, na kuwa ungeongezwa angalau ukafikia miezi sita.
“Tatizo la hisabati hata kama vitabu vipo sio rahisi mwanafunzi kusoma peke yake akaelewa bila kuwapo mtu wa kumwelekeza hasa katika muda wa kujisomea, ni tofauti na masomo mengine mtoto anaweza kujisomea na kuelewa” anasema.
Mwalimu Kombo pia anaona umri mdogo wa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza nao ni changamoto maana kutokana na umri huo anaokuwa nao mtoto, anakuwa hajawa na uwezo wa kuhimili vitu vigumu ambavyo vinahitaji umakini wa hali ya juu, na kutoa mfano kuwa sasa wanapokea wanafunzi wenye umri wa kuanzia miaka 12.
“Hata sisi walimu hatuna mafunzo ya mara kwa mara wakati mbinu za ufundishaji zinabadilika kila mara, lakini pia wingi wa wanafunzi darasani humfanya mwalimu ashindwe kumfikia kila mwanafunzi, na katika ufundishaji wa somo la hisabati bila kumfikia mtoto ili kumpa msaada wa karibu anaweza asielewe” anasema.
Anasema pia uchache wa walimu wa somo la hisabati kuanzia shule za msingi ni tatizo, lakini pia watoto kufanya mtihani wa taifa wa kuhitimu darasa la saba kwa kuchagua hasa wa hisabati, huwafanya kuonekana wanafahamu somo hilo, lakini akiingia kidato cha kwanza anaonekana hata hesabu ndogo zinamshinda.
“Matokeo mabaya ya somo hili ya wanafunzi wenzao waliotangulia nayo huwakatisha tamaa, utasikia mwanafunzi akidai fulani alikuwa akisoma sana hisabati, lakini kashindwa, pia hata uhaba wa vifaa vya kufundishia unaongeza tatizo” anasema Kombo.
Anatoa mfano wa chumba kimoja cha darasa la kidato cha tatu katika shule yake, kuwa kina wanafunzi 96 idadi ambayo ni kubwa, huku akisema pia watoto kukosa chakula shuleni ni tatizo maana ni vigumu kumfundisha mtoto somo gumu kama hisabati huku akiwa na njaa.
“Utakuta kuna siku somo hili lipo mchana, watoto hawajala chochote njaa inauma hata mwalimu akiwafundisha hawamwelewi” anasema.
Anasema kuwa ili kukabiliana na tatizo la watoto kufeli somo hilo iwekwe miundombinu inayoendana na idadi ya wanafunzi, mfano vyumba vya madarasa, madawati, meza na viti, na kutoa mfano kuwa katika shule yake kuna wakati watoto kati ya watatu hadi wanne wanakalia viti viwili kwa wakati mmoja.
“Wanachukua viti viwili wanaunganisha, wanabanana watatu au wanne, mtoto anayekaa katika mazingira ya namna hiyo ni vigumu kuwa makini kumsikiliza mwalimu, na somo hili usipokuwa makini huwezi kuambulia chochote utaishia kufeli” anafafanua.
Anaitaka jamii kuona hisabati ni sawa na masomo mengine ili kuwaondolea hofu watoto maana kila mara ndugu, wazazi, walimu na hata viongozi wa siasa husikika wakilipa majina yanayowakatisha tamaa watoto mfano kusema ni janga la kitaifa.
Anasema pia mitihani ya taifa ya kuhitimu darasa la saba hasa wa hisabati, ifanyike kwa ubora ili kuwezesha shule za sekondari kupokea watoto wenye uelewa, huku akiomba walimu kupatiwa mafunzo yatakayowawezesha kupata mbinu mpya za kufundishia.
Anasema kwa kawaida inabidi mwalimu wa hisabati kwa wiki afundishe vipindi sita, lakini katika shule nyingi inashindikana kutokana na uhaba wa walimu hivyo anaiomba serikali kuweka mikakati itakayowezesha kupatikana kwa wingi walimu wa hisabati.
“Walimu wa hisabati ni wachache, unaweza kukuta shule haina mwalimu hata mmoja au nyingine ina mwalimu mmoja tu wa somo hili, kwa hiyo kufundisha kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne ni mtihani mkubwa kwake, serikali iliangalie hili” anasema.
Anasema mfumo unavyoanzia chini wa kuogopa hisabati unakwenda hadi vyuoni, na kuwa ndiyo maana utakuta wanavyuo wanaojiandaa kwa ajili ya kufundisha somo hilo ni wachache, huku akiiomba serikali kuwezesha kupatikana kwa wanachuo wa kwenda kufundisha hisabati, ili kupunguza uhaba wa walimu wa somo hilo.
“Lakini hawa walimu inabidi waandaliwe vizuri ili watakapokuja kwenye kazi, waonekane wana uwezo mzuri wa kufundisha, wakiletwa walimu wasio na uwezo, tatizo la watoto kufeli hisabati litabaki pale pale,” anasema.
Ili kuthibitisha kuwa, watoto wengi wanafanya vibaya katika somo la hisabati, katika mtihani wa taifa wa kuhitimu kidato cha nne uliofanyika mwaka 2015, shule ya sekondari Hamugembe waliofanya mtihani ni wanafunzi 64 lakini waliofaulu somo hilo ni saba tu mbao ni sawa na asilimia 10.9.
OFISA ELIMU ATOBOA
Wandere Lwakatare ni Ofisa Elimu Sekondari katika manispaa ya Bukoba, anakiri watoto wengi kufeli somo hilo na kuwa pamoja na sababu nyingine kubwa zaidi ya zote ni msingi mbaya ambao wanafunzi wanatoka nao chini katika shule za msingi kwenda sekondari.
“Utaratibu wa elimu ya msingi mara nyingi ni wa kukaririsha sio wa kumwongezea mwanafunzi uelewa, kwa hiyo mtoto anapoingia sekondari anajikuta hana msingi mzuri katika ufahamu wa hisabati na kusababisha kupata ugumu” anasema.
Lwakatare ambaye pia ni mwalimu wa somo hilo, anasema hisabati katika sekondari hutegemea sana somo hilo lilivyofundishwa ngazi ya msingi maana yaliyopatikana ngazi za chini ndiyo hutegemewa ngazi za juu.
“Hisabati yahitaji mtu kufanya kazi, kusoma na kuelewa na kufanya mazoezi ya kutosha. Hilo, wanafunzi wengi hawapendi labda apewe zoezi na mwalimu kwamba lazima afanye, ni wachache wanaoweza kuchukua vitabu na kujisomea,” anasema na kuongeza
“Wakati nasoma mwalimu wangu aliniambia nikitaka kufahamu hisabati vizuri lazima nifanye maswali angalau matatu kila siku, maana ili kushinda somo hili lazima ufanye ukokotoaji kila mara,” anasema.
Anasema sababu nyingine ni imani ambayo watu wamejijengea kwamba somo hilo ni gumu kitu ambacho sio kweli, mfano utakuta baba au mwalimu anamwambia mtoto kwamba hisabati ni ngumu, kwa hiyo mtoto anaelewa ndiyo ukweli na anakata tamaa.
“Kuna walimu hawana msingi mzuri wa somo hili, kwa hiyo utakuta hata ufundishaji wake hautakuwa mzuri, na hii inajitokeza hasa kwa walimu wa shule za msingi kutokana na siku za nyuma walimu hawakujikita katika kujifunza masomo fulani na badala yake kutakiwa kujifunza na kufundisha masomo yote,” anasema.
Anasema pia kuna tatizo la walimu wa shule za msingi na sekondari kufundisha kwa mazoea na kutotumia zana za kufundishia somo hilo, ambalo ndiyo msingi mkubwa wa kumfanya mtoto kuelewa na kuwa na kumbukumbu.
“Maandalio duni kwa walimu walio wengi wa somo hili ni tatizo pia, mwalimu ananyanyuka na kitabu chake anakwenda darasani, anafunua ukurasa anaotaka kufundisha, akimaliza anatoa mfano ulioko kwenye kitabu wakati mwalimu mwenye maandalio mazuri anapaswa atengeneze mifano yake mwenyewe” anasema.
Anasema zamani katika shule za msingi karatasi moja katika daftali ilitengwa mara tatu, sehemu ya kwanza ilikuwa ya swali, ya pili kazi na ya tatu jibu. Anasema, mwalimu hata alipokuwa akisahihisha aliangalia njia iliyotumika na kuwa hiyo ilijenga uelewa kwa watoto tofauti, lakini sasa watoto wanakaririshwa kushinda mtihani.
“Suala la watoto kufanya mtihani wa hisabati kwa kuchagua sijalikubali sana, kwa maana lazima mtoto aonyeshe amefikaje kwenye jibu, kama ilivyo kwa shule za sekondari lakini pia kuna alama ambayo anaweza kupewa mtoto kutokana na namna alivyokokotoa hata kama jibu kalikosea,” anasema.
Anasema kuwa pia matumizi ya lugha tofauti nalo ni tatizo na kuwa kama lugha inayotumika ingekuwa moja kuanzia chekechea hadi elimu ya juu, bila kujali ni ya Kiswahili au Kiingereza, ufahamu ungekuwa mkubwa.
“Mtoto anapotoka katika shule za msingi ambazo sio zile zinazofundisha kwa mchepuo wa Kiingereza, anapokwenda kidato cha kwanza anapata shida kujifunza lugha na wakati huo akijifunza masomo ya kawaida,” anasema.
Lwakatare anasema kuwa, pia suala la uhaba wa walimu wa somo hilo ni chanzo cha watoto kufanya vibaya.
Kutokana na changamoto hizo anaona ili kupata watoto wanaoshinda vizuri somo hilo inabidi mwanafunzi kuandaliwa na kupata msingi mzuri wa hisabati kwa kumjengea uelewa badala ya kukaririshwa.
Kwa upande wa serikali anasema imejitahidi kuhakikisha vipo vitabu vya kutosha shuleni hasa vya hisabati, na kuwa kwa kupitia ruzuru inayotolewa na serikali asilimia 50 ya ruzuku hiyo inatumika kununua vitabu vya sayansi ikiwamo hisabati na vitabu vya lugha.
“Serikali inaendesha mafunzo kazini kwa walimu katika masomo ya sayansi na hisabati, na sasa kwa walimu wa masomo ya lugha ambayo ni Kiingereza na Kiswahili,” anasema.
Lwakatare anasema kuwa, pia serikali imeanzisha mafunzo ya walimu wa sayansi ngazi ya stashahada kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne, katika Chuo Kikuu cha Dodoma, ili kuongeza idadi ya walimu wa masomo hayo na kupunguza tatizo.
Kwa mujibu wa Ofisa elimu huyo, manispaa ya Bukoba ina shule za sekondari 33, zikiwamo za serikali 19 na binafsi 14.










