Shule za Songea zaelimishwa kukabili changamoto za kimwili na maumbile

05Apr 2016
Gideon Mwakanosya
Songea
Nipashe
Shule za Songea zaelimishwa kukabili changamoto za kimwili na maumbile

ELIMU ya afya ya uzazi na magonjwa yanayosababishwa na ngono ni muhimu sana kufundishwa wanafunzi shuleni kwa sababu ukosefu wake umekuwa ukichangia baadhi ya wanafunzi kukatisha masomo kwa sababu ya mimba za utotoni na matatizo mengineyo.

Ukosefu wa elimu ya mahusiano ya kimwili inayoweza kujenga au kuharibu maisha ya wanafunzi shuleni au mitaani.
Tafiti mbalimbali mbalimbali zinaonesha kuwa watoto wenye umri kati ya miaka 14- 25 ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukizwa VVU /Ukimwi

Pia yaonyesha kuwa kati ya asilimia 11 ya watoto wa kike na asilimia 10 ya watoto wa kiume tayari wanashiriki tendo la ndoa kabla ya kufikia umri wa miaka 15.Huo ni umri ambao wanafunzi hao wanasoma shule za msingi na baadhi wanaanza sekondari.

Kwa kutambua hilo, Asasi ya kiraia iitwayo Ruvuma Orphans Association (ROA) imeanzisha mradi uitwao Prevention and Awareness in Schools about HIV/AIDS ( PASHA ) katika shule za msingi tano za Misufini, Lilambo, Mateka, Madizini na Mjimwema zilizopo katika halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma

Lengo ni kuongeza utashi na utayari wa walimu na wanafunzi kuzungumzia masuala ya VVU/Ukimwi na kupiga vita unyanyapaa kupitia klabu za wanafunzi na walimu shuleni na kuongeza ufahamu kwa wanafunzi wa shule za msingi kuhusu uelewa wa VVU/Ukimwi na athari za masuala ya uzazi

Mwenyekiti wa Asasi hiyo Methew Ngarimanayo anasema kuwa mradi huo wa PASHA ni mkakati wa elimu ya kinga na uelewa kuhusu Maambukizi ya Ukimwi kwa shule za msingi.

Katika mkakati wa taifa wa mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, watoto wa kike wametajwa kama kundi la kuangaliwa kipekee (kundi la kipaumbele) katika mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi

Mpango huo umeanza kutekelezwa katika shule tano (5) za msingi zilizopo katika Manispaa ya Songea kwa kuwahusisha walimu na wanafunzi wa shule hizo ili wawe chachu ya mabadiliko shuleni na kwenye jamii zinazowazunguka

Mpango huu, unahusisha kuteua walimu na kuwapa mafunzo yahusuyo VVU/Ukimwi, Unasihi, Malezi ya watoto, na namna ya kuunda na kuendesha klabu za watoto shuleni.

Walimu waliopata mafunzo huteua watoto sita katika kila shule tajwa na kuwapa mafunzo yahusuyo VVU/Ukimwi, elimu ya afya na uzazi, elimu ya kujitambua na kukabiliana na changamoto za kimwili na kimaumbile.

Watoto hao kwa kushirikiana na walimu wao, wanatakiwa kuunda na kuendesha klabu za watoto katika shule zao na kuendesha mijadala kupitia klabu za watoto ili kuwajenga watoto hao kujiamini na kujadili mambo yanayowahusu kwa uhuru na fikra pevu

Mijadala hiyo itahusisha elimu kuhusu VVU/Ukimwi, elimu ya afya na uzazi na ujinsia, stadi za maisha, elimu kuhusu kukabiliana na changamoto za kimwili na kimaumbile na mazingira, michezo na ujasiliamali.

Lengo kuu la mpango huo ni kuwakinga watoto dhidi ya maambukizi mapya ya VVU/Ukimwi na kujitambua ili wawe chachu ya mabadiliko katika shule zao na katika jamii zinazowazunguka

Hadi sasa, tayari walimu wawili kutoka katika kila shule iliyopo katika mpango huu wametambulika na kupata mafunzo ya siku kumi na kwamba, walimu hao wametunukiwa vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo
Licha ya walimu hao, watoto sita kutoka kila shule iliyo katika mpango huu pia wamepata mafunzo ya siku tano na kuhitimu vizuri mafunzo yao

Ofisa Kinga wa Asasi hiyo Onesmo Mbilinyi akizungumzia alisema kuwa, suala la unyanyapaa shuleni au majumbani bado kubwa na kwamba juhudi zaidi zinahitaji ili kukabiliana nalo na kwa kutambua ukubwa wa tatizo la unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU imeanzisha kampeni ya kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi ili waweze kuwa na uelewa mzuri zaidi wa masuala ya VVU/Ukimwi

Mbilinyi alisema kuwa, suala la unyanyapaa ni mtambuka hivyo lengo ni kuhakikisha kuwa linapigwa vita na ili kulipa uzito suala hilo, vilabu vya watoto walio shuleni vimeazishwa ili visaidie jamii katika kueneza elimu ya VVU/Ukimwi na kupiga vita unyanyapaa na kujenga jamii jumuishi isiyo na ubaguzi wa aina yoyote ile kwani makundi yote ya jamii yana haki ya kulindwa

“Tumeamua kutoa elimu kwa wanafunzi hao, kutokana na umri wao kuwa mdogo, kwani watakuwa mabalozi wazuri wa kutoa elimu husika shuleni, michezoni na wanaporudi majumbani kwao, hivyo kusaidia jamii kupunguza athari za unyanyasaji na mimba za utotoni kwa kiasi kikubwa tofauti na ilivyo sasa,” alisema Mbilinyi

Naye Dadiely Chanachayo wa asasi ya ROA alisema kuwa, katika klabu hizo, zilizoanzishwa licha ya kujifunza mambo mbalimbali pia zimegawiwa mipira na vifaa vya michezo ili wanapomaliza kujifunza wanakwenda uwanjani kujenga afya kupitia timu zao

Chanachayo alisema kuwa, klabu hizo zitawaleta pamoja walimu na wanafunzi wao ambao watakuwa marafiki hali inayotarajiwa kupunguza utoro mashuleni, mimba za utotoni, magonjwa yatokanayo na ngono, vikundi vya matumizi ya dawa za kulevya na kamari na kufanya afya zao ziwe bora na kukuza ufaulu wa wanafunzi na kujenga jamii bora na inayothaminiana

Alisema mafunzo hayo yanayotolewa kwa walimu na wanafunzi ni endelevu na siyo ya kupita hivyo walimu na wanafunzi kwa awamu ya kwanza wamefaidika na mafunzo hayo na kwamba wataendelea kuzifikia shule nyingine, kwa mujibu wa bajeti ya mradi na kwamba Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo na wizara yenye dhamana ya afya kuziongezea nguvu asasi za kiraia zina uwezo wa kuendesha miradi kama hiyo

Walimu na wanafunzi waliopatiwa mafunzo ambao ni waelimishaji rika wanaendelea kutoa mafunzo hayo kwa wanafunzi wenzao kupitia klabu za afya mashuleni na katika shule zao za jirani lengo ni kuzifikia shule nyingi na jamii kwa ujumla
Walimu walionufaika na Mradi huo Asumta Haule na Irene Kayombo wanasema kuwa katika Idara ya Elimu kuna changamoto nyingi za unyanyapaa, lakini baada ya kupata mafunzo hayo wamepata ujasiri wa kupambana na suala hilo pamoja na kuwafariji walimu na wanafunzi ambao wameathirika na unyanyapaa wa aina yoyote ili kutibu athari za kisaikolojia katika akili zao ili waweze kujenga jamii yenye upendo na kuthaminiana

Naye Mwanafunzi Elizabeth Tindwa akizungumza kwenye mafunzo hayo alisema kuwa, licha ya kupata mafunzo bora ya namna ya kujilinda na mimba za utotoni na Ukimwi kuna kila sababu ya jamii kuwa na maadili stahiki na kuwalinda wanafunzi

Tindwa alisema kuwa, tumefaidika sana na mafunzo hayo ambayo yametujengea ujasiri mkubwa wa kupambana na vikwazo vyovyote katika afya zao pia watakuwa mabalozi wazuri wa kushauri na kutoa elimu mitaani, nyumbani, mashuleni na kwenye kaya zinazowazunguka ili ziweze kujenga jamii salama kwa mustakabali wa vizazi vijavyo

Naye Ofisa Elimu ya Watu wazima Nathaniel Yonas alisema kuwa mimba za utotoni ni tatizo nchini na Takwimu za Wizara ya Elimu na

Mafunzo ya Ufundi zaonyesha wasichana 8,000 kila mwaka huacha shule kutokana na ujauzito na kati yao 3,000 ni wanafunzi wa shule za msingi.

Yonas alisema, kila siku wanawake 24 hufariki dunia kutokana na mimba au wakati wa kujifungua na kwamba wanawake watano hadi sita wanaofariki kati ya hao ni watoto wadogo.

“Ni ukweli usiopingika kuwa, watoto hao hufariki dunia kwa kuwa miili yao haijakomaa vya kutosha kwa ajili ya kujifungua ,ingawa pia wanapopata mimba wasizozitarajia huzitoa kwa njia zisizo salama hivyo mradi wa PASHA unafaa kwa wanafunzi kwani unawasaidia kujitambua,”alisema Yonas