Waziri wa Afya Ummy: Asilimia mbili ya wanafunzi mabwenini wana TB

14Apr 2016
Romana Mallya
Dar
Nipashe
Waziri wa Afya Ummy: Asilimia mbili ya wanafunzi mabwenini wana TB

TANZANIA inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB). Ni athari zake zilizozama mbali katika jamii na inaelezwa kuwa hali si nzuri mabwenini katika shule za sekondari nchini, hususan mkoani Pwani.

waziri wa afya, ummy mwalimu.

Kuna tathmini inayotolewa, inasema kuwa mkoani Pwani kunatawaliwa na TB kwa sababu ya mabweni kuwa na vyumba vidogo na msongamano mkubwa wa wanafunzi.

Tathmini ya hivi karibuni zilizofanywa na Idara za Afya na Elimu katika baadhi ya shule za bweni za mkoa wa Pwani, inaonyesha katika madarasa mawili ya shule moja wanafunzi 16 kati ya 775 wamepatikana na TB ya kuambukiza.

Hiyo ni sawa na asiimia mbiIi ya wanafunzi wote, huku wastani wa kitaifa ukiwa ni asilimia 0.295 ay watu 295 kwa kila watu 100,000.

Uambukizaji TB ugonjwa huo unatokana na vimelea aina ya bakteria wanaojulikana kitaalam kama ‘Mycobacterium Tuberculosis’

Kwa kawaida, mtu anayeugua ugonjwa huo anapokohoa, kuongea au kupiga chafya kabla ya hajaanza matibabu, vimelea hivyo huingia hewani na mtu mwingine atakayekuwa karibu anaweza kuambukizwa.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anasema tathmini hiyo imebaini mabweni mengi yana vyumba vidogo na msongamano mkubwa wa wanafunzi.

Ummy alitangaza tathmini hiyo siku ya Maadhimisho ya Kifua Kikuu, ambayo kila mwaka husherehekewa Machi 24 na kaulimbiu ya mwaka huu inasema, ‘Tuungane Kutokomeza Kifua Kikuu.”

“Tathmini imeonyesha kuingia kwa TB shuleni ni hatarishi na inaweza kuwa chanzo cha maambukizi na kuenea zaidi, ikiwa hatua za makusudi hazitafanyika,” anasema.

Kutokana na changamoto hiyo, Ummy anawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri, wafanye ukaguzi kwenye shule zote za bweni za umma na binafsi, ili kubaini mazingira hatarishi.

“Hiyo iende sambamba na uchunguzi wa ugonjwa huu miongoni mwa wanafunzi katika shule za bweni za msingi na sekondari, kwa kutumia fomu za uchunguzi wa TB ikifuatiwa na upimaji kwa wale watakaoonyesha dalili,” anafafanua.

Waziri huyo anasema kuna fomu maalumu ambazo mwanafunzi kabla ya kujiunga na shule za bweni, wanatakiwa kuzipeleka hospitalini, ili wapimwe magonjwa mbalimbali.

“Baadhi ya wahudumu wa afya wanapopatiwa fomu hizi, wamekuwa hawawafanyii watoto vipimo, wanajaza tu. Huu mchezo naujua na nawaagiza wauache mara moja,”anasema.

Waziri Ummy anasema endapo mwanafunzi atapimwa na kugundulika mapema ana tatizo hilo, ni rahisi kulitibu kabla hajawaambukiza wenzake shuleni.

Kutokana na tatizo hilo, Ummy anasema wizara yake imeanza mashauriano na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ili kuweka mikakati endelevu ya udhibiti wa TB shuleni.

Anaongeza kuwa utaratibu wanaotaka unaotarajiwa kuanzishwa ni kwa mwanafunzi anayejiunga shule apimwe baada ya wiki mbili, licha ya kujaza fomu za awali.

Ummy anasema agizo hilo linaenda hadi kwa wamiliki wa shule binafsi, kuhakikisha wanafanya jitihada kubwa kulinda afya za wanafunzi na wanapaswa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakaguzi wa afya wanapopita shuleni.

TB NCHINI

Anasema takwimu za mwaka jana zinaonyesha ugonjwa bado TB ni tatizo na umelifanya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuendelea kuifanya Tanzania miongoni mwa nchi 22 duniani zenye wagonjwa wengi.

Aidha, anasema kutokana na changamoto za ugonjwa, TB itaendelea kuwa janga la kitaifa kama ilivyoainishwa katika Azimio la Maputo la mwaka 2005.

Anasema takwimu za vituo vya kutoa huduma za afya nchini zinaonyesha ugonjwa huo bado ni tatizo kubwa.

“Hali hii imedhihirishwa na matokeo ya utafiti wa kwanza wa kitaifa wa kutathmini kiwango cha maambukizi uliofanywa mwaka 2012/13, ambayo yanaonyesha pamoja na juhudi zote zinazofanywa na serikali na wadau, ugunduzi wa ugonjwa ndio umefikia wastani wa asilimia 50 tu,” anasema.

“Matokeo haya yanaonyesha pia kiwango cha ukubwa wa tatizo la TB ni zaidi ya wagonjwa 295 kwa kila watu 100,000. Hii inamaanisha kila mwaka, wastani wa watu 112,000 huugua Kifua Kikuu,” anasema.

Anasema ugonjwa kupitia uhalisia wa TB, kunaonyesha Tanzania ina idadi kubwa ya wagonjwa kutoka kwenye jamii ambao wanawakosa kila mwaka, ili kuwaweka katika matibabu.

MIKOA INAYOONGOZA

Waziri anaitaja mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mara, Manyara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Pwani, Shinyanga, Tabora na Tanga kuwa ndio imeelemewa na kasi ya maambukizi.

Mwalimu anasema, takwimu za mwaka 2015 zinaonyesha mikoa hiyo inachangia zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wote wa kifua kikuu waliogundulika Tanzania Bara na Visiwani.

Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, anasema wastani wa wagonjwa wapya 63,000 wamekuwa wakigundulika na kuanzishiwa matibabu kila mwaka.

Anasema utafiti na tathmini nyingine za hivi karibuni, zimeonyesha wazee na watu wanaoishi vijijini na maeneo hatarishi yenye misongamano kama vile kwenye mabweni, Magereza na migodini wako hatarini, tofauti na ilivyodhaniwa awali.

Anataja takwimu za wizara yake za mwaka 2014, ambazo nazo zinaonyesha kuna ushiriki mdogo wa vituo vya afya binafsi na asasi zisizo za kiserikali katika kutoa huduma za TB.

“Ni asilimia 10 tu ya vituo vyote vya binafsi vinatoa huduma za kifua kikuu na ni asasi chache tu zinazojihusisha na harakati za mapambano ya kifua kikuu katika mikoa na halmashauri zetu,” anasema.

Waziri anatoa rai kwa wamiliki wa vituo binafsi vya afya, kupanua wigo wa huduma za TB katika taasisi zao.
Waziri Ummy anasema wizara yake imeanza mchakato wa kuhakikisha utoaji huduma za TB. ni lazima kwa vituo vyote vya serikali na binafsi.

Anaeleza dhamira ya serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo katika maeneo wanakoishi, bila ya kikwazo chochote.

“Serikali itaendelea kushirikiana na watoa huduma wote pamoja na kusimamia ubora wa huduma kwa upande wa kifua kikuu, tutaendelea kuvipatia vituo binafsi dawa za kutibu TB, vifaa vya upimaji na vitendaji bila gharama yoyote kama ilivyo kwa vituo vya umma,” anabainisha.

Waziri anaongeza kuwa ameshawaagiza watumishi walioko kwenye vituo vya afya, wahakikishe wanatoa huduma bora kwa wagonjwa wote wanaogunduliwa kuwa na TB, kwa kuwasajili na kuanza kuwatibu bila ya kuchelewa.

KIFUA KIKUU SUGU

Waziri Ummy anasema usimamizi duni na ufuatiliaji wake unasababisha kuongezeka usugu wa dawa, tatizo linalochangia kuwepo TB sugu.

“Niwakumbushe kuwa tatizo la TB sugu ni ghali sana na huchukua takribani miaka miwili mgonjwa kuweza kupona,” anasema Ummy.

“Nahimiza kila mtu katika nafasi yake zikiwemo asasi za kiraia, idara za serikali, mashirika binafsi, wanahabari na wadau wa maendeleo, kuunganisha nguvu kwa pamoja kuongeza kasi na kuchochea mapambano dhidi ya kifua ikuu,” anafafanua.

WANAOPONA

Anasema kiwango cha wagonjwa wanaopata matibabu na kupona kimevuka lengo la kimataifa ambalo ni asilimia 85, huku Tanzania ililifikia asilimia 91 mwaka juzi.

Anasema vifo miongoni mwa wagonjwa, vimepunguzwa kwa asilimia 50, kutoka asilimia 11 za mwaka 2000 hadi kufikia asilimia 5.6 mwaka juzi.

Waziri anasema takwimu za mwaka jana zinaonyesha asilimia 91 ya wagonjwa wote wenye maambukizi ya TB, walipima maambukizi ya VVU na kupata ushauri nasaha.

Anasema, wenye magonjwa mseto TB na Ukimwi wanapata dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV).
Pia anasema wizara imefanikiwa kupeleka huduma za matibabu hadi ngazi za kaya na zaidi ya asilimia 78 ya wagonjwa wamekuwa wakipata dawa nyumbani chini ya usimamizi wa ndugu na jamaa zao wanaowachagua wenyewe.

ZANA ZA UCHUNGUZI ZAIMARISHWA

Mwalimu anasema zana hizo za uchunguzi na ugunduzi zimeboreshwa na sasa matokeo ya katika hospitali nyingi za mkoa na wilaya yanapatikana ndani ya saa mbili badala ya siku tatu kama ilivyokuwa awali.

“Mpaka sasa zaidi ya wagonjwa 495 wa TB sugu tayari wameanzishiwa matibabu katika taasisi ya magonjwa ya kuambukiza ya Kibong’oto mkoani Kilimanjaro kutoka kuanzishwa kwa huduma hizo mwaka 2009 na silimia 80 kati ya hao wamepona,” anasema.

Mkurugenzi wa Huduma na Tiba wizarani hapo, Dk. Margaret Mgando, amekiri hali ya Kibong’oto ambayo ndiyo tegemeo kwa wagonjwa hao kuwa mbaya na kueleza kuwa mchakato wa kuiboresha umeanza.

Anaeleza kwa sasa kuna upanuzi wa hospitali hiyo unaoendelea na wataongeza vifaa pamoja na kuifanya iwe na bodi ya kuiendesha.

Meneja Mpango wa Taifa wa Programu ya Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, Dk. Beatrice Mutayoba, anasema mkakati wa WHO ni ifikapo mwaka 2035 ugonjwa huo uwe umetokomea.