wariLeo ni mwendelezo wa makala hiyo, ikimhusu Swabrina Ghalibu (19), msaidizi pekee wa Iswalala, ambaye katika kipindi kifupi cha mafunzo kazini hospitalini hapo, ameonyesha uwezo mkubwa wa jukumu lake, hata kugeuka mvuto mkubwa kwa uongozi wa hospitali uliodhamiria kumuajiri.
Hilo linaendana bosi wake kazini, Iswalala naye kuvutiwa na utendaji wake na kubatiza jina la utani ‘Jembe.’ Fuatilia mazungumzo yao na mwandishi wa makala hii:
Nipashe: ‘Jembe’ Swabirina hujambo?
Swabrina: Sijambo karibu mwandishi, umerudi tena? Kwanini unaniita jembe? (anaonyesha kujiamini na kufahamu kuna watu wanaomshangaa)
Nipashe: Ni baada ya kuambiwa wiki iliyopita na Andrew (Iswalala) kuwa wewe ni ‘Jembe’ na anakutegemea sana tena katika zile kazi ngumu ambazo wengine wameshindwa, lakini wewe unazimudu.
Swabrina: Mbona kawaida tu!
Nipashe: Ok! Niliahidi ningerudi tena kuongea na wewe baada ya kuambiwa siku ile ulikuwa ‘bize.’ Vipi leo uko tayari kuongea na mimi?
Swabrina: Usijali wewe niulize chochote.
Nipashe: Jina lako kamili unaitwa nani?
Swabrina: Jina langu kamili naitwa Swabrina Ghalibu Khatibu na ninaishi Mlandizi karibu na Bar ya Twiga.
Nipashe: Swabrina wewe ni mtoto wa ngapi katika familia yenu?
Swabrina: Mimi ni mtoto pekee kwa wazazi wangu. Nilizaliwa peke yangu!
Nipashe: Nieleze kwa kifupi historia yako.
Swabrina: Nilizaliwa miaka 19 iliyopita hapa katika hosptali ya Tumbi mjini Kibaha. Nilianza masomo katika ya Shule ya Msingi Jamhuri mwaka 2004 na kuhitimu mwaka 2010. Niliendelea na masomo katika Shule ya Sekondari Kilangalanga mwaka 2011 na kumaliza mwaka 2014.
Nipashe: Baada ya kumaliza kidato cha nne uliendelea na nini?
Swabrina: Nilijiunga na chuo cha afya kilichoko Mafinga. Kinaitwa Neema Uhai na nilichukuwa kozi ya mwaka mmoja ya uhudumu wa Mochuari.
Nipashe: Nieleze kwa kifupi, ilikuwaje hadi ukaamua kusomea kazi, hii binti mrembo kama wewe na wakati imezoeleka kuwa wahudumu wa Mochuari huwa ni wanaume tena wenye ujasiri?
Swabrina: Dada yangu siku hizi hakuna kuchagua kazi. Kazi zote zinafanywa na kila mtu. Ni kweli awali kazi kama hii ilikuwa inafanywa na wanaume pekee, lakini hivi sasa ni wanaume na wanawake. Hata chuo ninachosoma, wanawake ndio wengi zaidi.
Nipashe: Vipi kuhusu wazazi wako walipokeaje suala lako la kutaka kusomea kazi hii?
Swabrina: Kwa mara ya kwanza walikataa, lakini walipoona nina msimamo, waliamua kukubaliana na mimi na kunilipia ada ambayo ni Shilingi milioni 1.5 na nikaenda Mafinga kusoma.
Nipashe: Mlikuwa wangapi mnaotoka Mlandizi na kwenda katika chuo hicho kwa ajili ya kusomea fani hiyo?
Swabrina: Nilikuwa peke yangu niliyetoka Kibaha, lakini kule Mafinga katika darasa letu tulikuwa wanafunzi kumi na kati yao, wanawake tulikuwa wanane na wanaume wawili na idadi kubwa walitoka mikoa ya Kusini.
Hata hivyo, wakati tunakwenda ‘field’ (mafunzo kwa vitendo kazini), wenzangu wote walisema wanaenda kubadilisha fani, hawataki tena, yaani walikuwa mguu ndani mguu nje.
Nipashe: Uliweza kuwadadisi ni kwanini waliamua kubadilisha fani hiyo?
Swabrina: Hakuna kingine ni woga tu, walikuwa wanaogopa.
Nipashe: Unafikiri nini kiliwaogopesha?
Swabrina: (Anatafakari)…Nadhani ni woga wa kuhudumia maiti tu, wameshindwa kuwa wajasiri.
Nipashe: Wewe mbona huogopi
Swabrina: Ni kazi ambayo ninaipenda. Sikushawishiwa na mtu na hivyo naifanya kwa moyo mmoja bila ya woga.
Nipashe: Marafiki zako wanakuchukuliaje, hasa wale mnaoishi nao Mlandizi na hata wale mliomaliza nao shule ya sekondari Kilangalanga Kibaha?
Swabrina: Ki-ukweli wananiogopa sana! Kuna waliowahi kuja hapa Mochuari walikuwa wamefiwa. Waliponikuta hapa, walishangaa sana. Waliniogopa na kusema mimi sio mtu wa kawaida.
Nipashe: Una rafiki wa kiume au mchumba na kama unaye, anakuchukuliaje?
Swabrina: Ninaye mchumba,lakini sitaki kumzungumzia gazetini.
Nipashe: Ok! lakini mchumba wako anasemaje juu ya fani hii unayoisomea?
Swabrina: Kwa ukweli yeye hapendi kabisa kazi hii, lakini mimi ‘nakomaa’ tu. Kila wakati nimekuwa nikimuelimisha kuwa kazi hii haina ubaya wowote.
Nipashe: Mlifahamianaje na huyo mchumba wako? Wazazi wake wanaishi wapi?
Swabrina: Wanaishi Mlandizi, lakini wao ni Wachagga. Tulifahamiana Mlandizi.
Nipashe: Katika kipindi chote ulichokuwa katika mazoezi ya vitendo katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Tumbi, ulishawahi kukutana na maiti iliyokutisha au kitu chochote ambacho ulikutana nacho na kikakuogopesha?
Swabrina: Sijawahi kukutana na kitu chochote kibaya nikiwa katika mazoezi. Naona kila kitu ni cha kawaida, hakuna cha ajabu.
Nipashe: Vipi siku ya kwanza ilikuwaje ulipohudumia maiti kwa mara ya kwanza, ulijisikiaje? Hukuwa na woga?
Swabrina: Siku ya kwanza nakumbuka ilikuwa kule Mafinga Iringa, nikiwa chuoni. Nilipewa maiti ya mwanamke na alikuwa mzee yaani bibi. Nikaambiwa nimuhudumie.
Kwa ukweli niliogopa sana, nikaanza kulia. Sikuweza kabisa kufanya chochote.
Nipashe: Oooh pole! Nini kilikufanya ulie, maiti ilikuwa inatisha au uliona nini?
Swabrina: Wala hakuwa anatisha. Nilijiwa na huruma na kuona kumbe sisi binadamu ni wa kupita tu. Kumbuka nilikuwa sijawahi kuona maiti tangu nizaliwe.
Nipashe: Enhee! Baada ya kulia ikawaje?
Swabrina: Mwalimu aliniambia natakiwa kuwa mjasiri na mtu akishakufa, hana anachosikia kwa hiyo nisiogope, nimuhudumie.
Nipashe: Unaieleza nini jamii hasa wanawake wanaogopa kusomea fani hii na wale wenye dhana potofu kuhusiana na wahudumu wa Mochuari?
Swabrina: Naitaka jamii iache dhana potofu kuhusiana na fani hii. Ni kazi kama kazi nyingine na ajira ziko nje nje.
Nipo kwenye mazoezi, lakini tayari nimeshapata maombi kutoka hospitali mbalimbali wakinitaka niandike barua za kuomba ajira. Hata katika hopistali (Tumbi), pia wanasema nisiondoke, wataniajiri.
Nipashe: Unafikiri kwanini unagombewa na waajiri wa hospitali mbalimbali?
Swabrina: Zipo sababu nyingi. Mojawapo ni jinsia, wahudumu wanawake ni wachache na wenye umri wangu hakuna kabisa.
Wanasema nitatoa huduma nzuri kwa maiti wa kike, tofauti na awali maiti za kike zilikuwa zikihudumiwa na wahudumu wa kiume.
Nipashe: Kwa hiyo umekuwa ukitoa huduma kwa maiti wa kike tu?
Swabrina: Hapana! Hapa ninahudumia maiti wa aina zote, lakini endapo kuna mhudumu kwa ajili ya wanawake, ni vyema. yeye akafanya kazi hiyo badala ya kufanywa na wanaume.
Nipashe: Nashukuru sana ‘Jembe’ Swabrina kwa ushirikiano wako, pia nakupongeza sana kwa kuwa mwanamke jasiri hasa ukiwa katika umri mdogo. Nakutakia kazi njema na kwaheri!
Swabrina: Asante dada mwandishi, nashukuru, karibu tena.










