Miongoni mwa chakula bora chenye rutuba kwa mwili ni uyoga ambao una protini zinazohitajika kujenga mwili na kuwezesha viungo vya mfumo mzima wa mwili, vifanye kazi vizuri.
Kimsingi, lishe ya mwandamu inapatikana katika makundi makuu matatu; vyakula vinavyotia nguvu mwilini, kuujenga na kuulinda.
Binadamu anapokula uyoga, basi ananufaika moja kwa moja na wanga mwilini kupitia mafuta yanayotoa nishati katika mifumo mbalimbali ndani ya chembehai za mwili.
Pia, mchaganuo wa kitaalamu unaonyesha kuwa vitamini anazozipata mwanadamu kupitia lishe ya uyoga, zinausaidia mwili kujikinga dhidi ya maradhi kwa nyakati na mazingira tofauti.
Aidha, uyoga una utajiri wa madini yanauyojenga mwili na kuwezesha mifumo mbalimbali ifanye kazi vizuri.
‘NJE NA NDANI’ YA UYOGA
Waziri Mkuu mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, ambaye huwa haonekani hadharani mara kwa mara, naye katika moja ya hadhira za karibnui, amejitokeza ‘kupigia debe’ zao hilo kwa maana ina manufaa mengi kwao.
Ni ushauri alioutoa hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Utafiti cha Kilimo cha Uyoga, kinachomilikiwa na Shirika la Afya na Elimu la Hubert Kairuki (KHEN).
Historia ya kula uyoga inaenda mbali zaidi, kwani wakongwe katika zama zilizopita walitumia kwa namna kama vile chakula na ilihifadhiwa kwa namna tofauti kama vile kuzikausha kwa matumizi ya baadaye.
Kwa mujibu wa Dk. Salim, uyoga uko katika orodha ya mazao yasiyopewa kipaumbele nchini, kutokana na sehemu kubwa ya umma kutojua umuhimu wake mwilini, lakini wakipewa elimu kuhusu faida zake wanaweza kunufaika kupitia chakula na tiba.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Profesa Keto Mshigeni, anasema katika maadhimisho ya 17 tangu kifo cha muasisi huyo, wamebuni mradi wa kisasa utakaobadilisha mfumo wao wa mapato.
Anasema uyoga ukitumiwa vizuri kama chakula, unanufasisha pia katika sura ya pili ya kutibu kwa njia ya kuongeza kuongeza kinga mwilini kwa wagonjwa wa Ukimwi na Saratani.
Anasema kuna aina nyingi za uyoga ambazo hazitumiwi kama chakula, mojawapo ni kama dawa, hatua iliyoanza kutumika tangu miaka 2,000 iliyopita.
“Dawa ya ‘Penicillin Notatum’ inazalishwa na uyoga aina ya kuvu (fungus). Kumekuwapo mwamko wa kufanya utafiti kuhusu uyoga na hasa aina ya uyoga ambazo huko nchini China zimekuwa zikitumiwa katika tiba kwa magonjwa mengi,” anasema Profesa Mshigeni.
Anafafanua hilo kwa kutumia mfano wa utafiti wa uyoga aina anayoitaja kwa jina la Ganoderma Lucidum.’
“Hizi pamoja na aina nyingine nyingi za uyoga, zinaaminiwa kuwa na uwezo wa kupunguza makali ya magonjwa au kuponya kabisa baadhi ya magonjwa kama vile saratani, shinikizo la damu, matatizo ya moyo, figo, ngozi na vidonda visivyopona,” anasema.
Profesa Mshigen, anaeleza katika nchi zilizoendelea ikiwamo China, kuna desturi ya kukithamini kilimo hicho cha uyoga.
“Mwito wangu ni kwamba, Watanzania wajenge desturi ya kulima kilimo cha uyoga kama mazao mengine makuu ya kunyanyua kipato cha taifa na mtu mmoja mmoja, kwa sababu wanaweza kubadilisha mfumo wa kuzalisha na kuuza katika soko la ndani na nje,” anasema Profesa Mshigeni.
UYOGA vs MARADHI
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, kupitia uyoga mwili wa binadamu unanufaika na vitamini C, D na na madini aina ya Potassium, hivyo lishe hiyo ikitumika vizuri, inaunusuru mwili dhidi ya balaa la kupata maradhi ya saratani.
Profesa Mshiheni anasema viini vilivyomo katika uyoga, humuondoa mlaji hatari ya kukabiliwa na viashiria vya magonjwa hayo kwa namna mbalimbali.
Eneo lingine la kumnusuru mgonjwa ni katika maradhi ya kisukari, hata kwa wale ambao tayari wameshaathrika wanapewa nafuu ya kiafya.
Jingine analolitaja la manufaa ya kiafya, ni kuufanya mfumo wa damu kuwa mwepesi, hivyo inarahisisha mzunguko wake mwilini na kumnusuru dhidi ya uchovu na maumivu ya viungo.
Uyoga pia unaiondoa lehemu iliyoko moyoni kupambana na msukumo wa damu, hali kadhalika inatibu ugonjwa wa athma unaoimarisha mfumo wa upumuaji.
Profesa Mshigeni anaongeza kuwa uyoga unatibu tatizo la mwili kuwa na mzio (allergies), matatizo ya figo na kadhalika.
USHAURI
Ili binadamu ajijengee afya njema, anashauri kula uyoga walau mara mbili kwa wiki na aina ya uyoga unaoshauriwa kutumiwa, ni ulio katika uhalisia wake.
Mkuu huyo wa asasi ya Kairuki, anawatahadharisha walaji kuwa makini na uyoga uliochumwa porini, kwamba ni baadhi yake huwa na sumu .
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa anwani ya barua pepe: efraciajoseph@yahoo.com na simu’
+255 753 390772










