WAZIRI, RC, DC MOROGORO WAAMUA

14Apr 2016
Ashton Balaigwa
Kilosa
Nipashe
WAZIRI, RC, DC MOROGORO WAAMUA
  • Vijiji kugawanywa upya na wafugaji kutengewa malisho 50 katika mikoa 16

MIGOGORO ya wakulima na wafugaji katika mkoa wa Morogoro imeendelea kuwa tishio kwa muda mrefu na hivi sasa inagharimu maisha ya watu na mali zao.

aliyekuwa mbunge wa Mvomero, Amos Makalla, akimsaidia mmoja wa waathirika wa mapigano ya wakulima na wafugaji jimboni kwake.

Wilaya za Kilosa na Mvomero ndizo kwa sasa zimeshamiri katika migogoro hiyo, licha ya kuwepo jitihada za serikali na asasi binafsi kudhibti.

Kushamiri migogoro hiyo, kunatokana na maeneo hayo kuwa na hali nzuri ya hewa, ardhi yenye rutuba inayowafanya wakulima na wafugaji kushindwa kuvumiliana, inapotokea
wamepishana kauli katika shughuli zao.

Wafugaji na wakulima wanategemeana katika kupata riziki za kila siku. Wakati mfugaji anamtegemea mkulima kuzalisha mazao ya chakula ili apate mahitaji yake kila siku ya mlo, mkulima anamtegemea mfugaji kwa ajili ya lishe kama nyama na maziwa.

Migogoro iliyokithiri katika wilaya za Kilosa na Mvomero kati ya wafugaji na wakulima, inajumuisha makundi ya wafugaji kutoka mikoa ya Manyara, Arusha, Mwanza, Simiyu, Shinyanga na Geita.

Kuna maswali yanayojitokeza kwa umma kwamba shughuli za kilimo na ufugaji ziko katika maeneo hayo kwa kipindi kirefu, lakini hakujawahi kusikika mapigano, mauaji, vurugu na uharibifu wa mali kama hali inayojitokeza sasa. Chanzo ni nini?

MIGOGORO KILOSA

Wilaya ya Kilosa ndio iliyoanza kuwa na migogoro kati ya wakulima na wafugaji kuanzia miaka ya 1990 ulipotokea mgogoro mkubwa katika kijiji cha Rudewa Mbuyuni, hata kusababisha vifo vya watu 29.

Hiyo inadaiwa ilitokana na mfugaji mmoja kuingiza mifugo katika shamba la mkulima ambaye alichukua bunduki na kumpiga. Hapo ndipo wafugaji walipoungana na kulipiza kisasi kwa wakulima.

Hivi Karibuni migogoro hiyo imeendelea na kushika kasi katika wilaya ya Kilosa, huku vijiji vya Parakuyo, Mabwerebwere, Tindiga, Rudewa Mbuyuni, Rudewa Mabatini, Ngaite Ulaya na Mabwegere vikiathirika zaidi.

KILIO CHA WAKULIMA

Migogoro iliyopo dai lake ni kwamba linatokana na kuwepo vijiji vilivyoandikishwa ndani ya mashamba makubwa yenye hatimiliki zilizo hai. Jingine ni wakulima na wafugaji kupakana.

Chanzo cha migogoro ni kwamba, katika maeneo hayo hivi sasa kunadaiwa kuwepo ongezeko la mifugo kutoka nje ya wilaya na kuzalisha wingi usioendana na mahitaji halisi ya ardhi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Rudewa Mbuyuni wanachoishi wakulima, Amos Hilaly, anaelekeza lawama kwa serikali kwamba mara nyingi mgogoro wa wakulima na wafugaji, kesi yao huishia mkulima huwa hapati haki kutokana na kuwepo dhana wanaofanya maamuzi wanawaogopa wafugaji na ndio chanzo cha migogoro.

Msuguano huo kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa kijiji, ni pale mifugo wanapolishiwa katika mashamba ya wakulima.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Rudewa Mbuyuni, Dawood Kufa, anasema chanzo cha migogoro hiuyo ni wafugaji kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima kwa makusudi.

Anasema, kwa sasa hali imekuwa mbaya, licha ya wafugaji kudhibitiwa na makundi ya sungusungu yalioundwa na viongozi wa kijiji na kutakiwa kulipa faini.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Rudewa Mabatini, Juma Mfaume anaungana na mwenzake, akisema hali imekuwa mbaya, licha ya wafugaji wanaotuhumiwa baada ya kuingiza ngombe katika mashamba ya wakulima kukamatwa na shauri sasa liko mahakamani.

“Ipo kesi moja kwa mkulima amempeleka mfugaji mahakaman, baada ya ng’ombe wake kuingia na kula mazao ya mkulima karibu ekari tatu na ushahidi wa mifugo ulikamatwa na Polisi,” anasema Mfaume.

Anaongeza: “Alipompeleka mahakamani, mkulima alishindwa kesi na kuambiwa alitakiwa kuishitaki mifugo na siyo mwenye mifugo.”

WAFUGAJI WANENA

Mwenyekiti Mstaafu wa Kijiji cha Wafugaji cha Palakuyo, Abdallah Niuyai, anajitetea akisema hawana tatizo na wakulima tangu miaka ya nyuma na walikuwa wakiishi kindugu, kwa shida na raha.

Niuyai anasema kuwa tatizo limeibuika katika miaka ya karibuni, migogoro ikichangiwa na baadhi ya vigogo wanaohodhi mashamba makubwa wilayani Kilosa.

Bila ya kuwataja majina, anasema vigogo hao wanahodhi mashamba makubwa bila ya kuyaendeleza, huku wafugaji wakikosa maeneo ya kulisha na kunyweshea mifugo yao.

Hapo ndipo panapoibua hoja ya wanakijiji kutaka serikali iyagawe mashamba hayo yaliliyotelekezwa kwa wafugaji na kila hoja hiyo inapoibuliwa, huishai katika mgogoro.

“Kuna mashamba makubwa yanamilikiwa na viongozi wa serikali, lakini hayajaendelezwa kwa miaka mingi. Ukiingiza ng’ombe huko, wanauawa kwa risasi.

“Kwa nini wasitupe sisi wafugaji tukafugia mifugo yetu ambayo imekuwa ikiongezeka? Sisi hatufurahiii ugomvi na wakulima,” anasema.

Anatoa mfano wa namna wamiliki wa ardhi wanavyochangia migogoro hiyo, akidai kijiji chao chenye hati miliki ya kuishi wafugaji, hivi karibuni ardhi yake imemegwa na serikali na kupewa kijiji cha Rudewa Mbuyuni.

Niuyai analitaja hilo kuwa jambo lililozua mgogoro mpya, kwani hali iliyoko sasa ni kwamba eneo lililobaki haliwatoshi wafugaji, lakini bado wanapunguziwa.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Parakuyo, Salum Kibugule, anakiri kuwepo mgogoro kijiji kwake, ardhi yao kumegwa na kupewa kijiji cha Rudewa Mbuyuni.

Hata hivyo anasema mgogoro huo umeshamalizwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, John Henjewele.

MSOMI AUCHAMBUA MGOGORO.

Mtafiti kutoka mradi wa Usalama wa chakula (Trans Sec) kwa kushirikiana na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Wadogo (Mviwata), Paul Saidia, anasema kuwab kuendelea kuwepo migogoro hiyo katika Wilaya ya Kilosa, kunahatarisha usalama wa chakula.

Mtafiti huyo ambaye ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu(Ph.d) katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia utafiti wake uliofanyika katika vijiji viwili vya Kilosa, anabainisha kuwepo wa tishio la usalama wa chakula kwa wananchi, hao, endapo migogoro itaendelea.

Saidia anasema wakulima wengi kumiliki mashamba, wanashindwa kuendesha kilimo kutokana na mazao yao kuharibiwa na mifugo kila mara na wanapoingilia kati kuwazuia, wanaambulia vipigo kutoka kwa wafugaji.

“Katika utafiti wetu, tumekutana na kikwazo kikubwa kinachotishia usalama wa chakula ni suala la migogoro baina ya wakulima na wafugaji hili ni tatizo kubwa na lipaswa kushughulikiwa kwa haraka sana,” anasema Saidia

Ushauri wa msomi huo wa kilimo, ni kwamba serikali ihakikishe inamaliza kabisa tatizo la migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

MKUU WA WILAYA

Kwa upande wake, Mkuu Wilaya ya Kilosa, John Henjewele, anaanza kwa kukiri kuwepo migogoro hiyo ya muda mrefu na kusababisha athari kubwa.

Anasema kuwa, hilo linatokana na mazao ya wakulima kuwa na mifugo, tena baadhi ya matukio hiyo hufanywa kwa makusudi.

Henjewele anataja chanzo kingine ni kuwapo watendaji wa vijiji wasio waaminifu, wanaopokea hongo za wafugaji na kuwaruhusu kuingiza mifugo katika maeneo ambayo ardhi yake haitoshi kuchungia mifugo.

Anasema tayari wameshaanza kuchukua hatua mbalimbali, zikiwemo kuwatambua wamiliki wa mashamba pori na yale yenye hati, ili kufutiwa umiliki na kupewa kiasi anachotumia.

“Wapo watu wanamiliki mashamba makubwa, lakini wanatumia kiasi kidogo kama ekari tano au kumi na mengine wanakodisha kwa watu.

“Sasa hao tunawafutia hati zao pamoja na wale waliochukua mashamba katika vijiji kinyume na utaratibu. Tutagawa upya mashamba hayo na kipaumbele ni wakazi wa eneo husika ili kumaliza migogoro,” anasema Henjewele.

Mkuu huyo wa wilaya anasema serikali imepiga marufuku kuanzishwa vijiji vipya vya jamii ya wafugaji wa kabila moja, akidai vinachangia kuzuka migogoro baina yao na wakulima.

Anasema wanakusudia kuruhusu uanzishwaji vijiji vipya vitakavyochanganya jamii ya wafugaji wa makabila tofauti na wakulima.

Henjewele anafafanua kuanzishwa vijiji vya kabila moja hakutapewa nafasi tena, kwani kumechangia kuwepo migogoro inayodumu kwa muda mrefu wilayani Kilosa.

MKUU WA MKOA

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe, anasema kazi kubwa aliyopewa mara baada ya kuapishwa, ni kuhakikisha anamaliza migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa sugu.

Anaeleza kushangazwa na sababu ya kuwepo migogoro mkoani Morogoro na haipo katika mikoa mingine.

Dk. Kebwe anasema kwa kuanzia, atashirikisha wazee wa mkoa huo kutafuta ufumbuzi wa migogoro iliyodumu kwa muda mrefu wilayani Kilosa na Mvomero na imeletea jamii madhara.

“Mbona kuna mikoa ya wafugaji na wakulima kama mimi nilikotoka kuna migogoro ya ardhi, lakini, huwezi kusikia maafa kama kama ilivyo kwa M0koa wa Morogoro.

“Hivyo, wazee kwa kushirikiana na serikali, lazima tufanye jitahada za pekee kuhakikisha sakata hilo linamalizika na watu wanaishi kwa amani,” anatamka mkuu huyo wa mkoa.

Anadokeza kuwa tayari kuna mikakati imeshaanza kutekelezwa, ikiwapo upimaji upya ya maeneo ya vijiji, ili kuhakikisha wananchi na wafugaji wanakuwa na maeneo yao.

Anaeleza nafasi ya wazee katika kila jamii wana wana nafasi kubwa na muhimu katika ujenzi wa taifa na ndiyo hazina ya busara, hekima, amani na utulivu wa jamii, hivyo abna sababu zote za kuwatumia kumaliza msuguano.

“Wazee wangu nawaombeni sana mshirikiane na serikali katika kumaliza migogoro hii ya ardhi. Naamini mnaheshimika sana katika jamii zenu,hivyo tunahitaji busara zenu kuhakikisha mkoa wetu unakuwa wa amani na utulivu muda wote,” anasema Dk.Kebwe.

WAZIRI WA KILIMO

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Gabriel ole Nasha, anasema wanakusudia kutenga maeneo 50 katika mikoa 16 nchini yatakayotumiwa na wafugaji kwa ajili ya malisho ya mifugo.

Waziri ole Nasha anaeleza imani yake kwamba, huenda maamuzi hayo yatapunguza au kumaliza kabisa migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.

Anasema kuwepo kwa maeneo machache ya malisho ndio sababu kuu ya baadhi ya wafugaji kuvamia maeneo wakulima na kusababisha migogoro.

Anasema katika ijayo, serikali itatangaza malisho 50 ya mifugo katika mikoa 16 nchini, ambayo ni: Morogoro, Tanga, Pwani, Mbeya, Arusha, Mwanza, Manyara, Singida, Mara, Dodoma, Kilimanjaro, Kagera, Tabora, Iringa na Simiyu.

Naibu Waziri anasema mbali na kutenga maeneo hayo, serikali bado inaangalia mfumo mzuri wa malisho, ikiwemo kutunga sera mpya itakayoshirikisha wadau wote wa malisho.

Anawataka wafugaji nchini kuomba maeneo ya malisho yatakayotengwa na serikali, badala ya kuvamia maeneo wasiyoyamiliki.

Mwenyekiti wa Nyanda za Malisho Tanzania (RST) Efraimu Joseph, anasema kwa sasa chama hicho kimejipanga kuhakikisha kila wilaya kinakuwa na wakala wa malisho ili kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.