Udanganyifu huo, unaofanywa na baadhi ya watu kwa kufanya biashara ya kutengeneza vyeti feki kwa bei ya chini, huku wengine wakidiriki kuwatengenezea ta wanafunzi wa vyuo vikuu kwa gharama ya kuanzia Sh. 120, 000 hadi Sh.700, 000.
Vyeti hivyo vya elimu ya sekondari navyo vinadaiwa kuuzwa kwa Sh. 50,000 na hutumiwa na watu katika kupata ajira hapa nchini.
Wafanyabiashara hao hudiriki hata kujitangaza katika vyombo vya habari, lakini Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, haionekani kuchukua hatua za haraka.
Katika baadhi ya shule za sekondari na msingi, walimu waoke kwa kushirikiana na wakuu wa shule zao, wanadiriki kula njama yakununua mitihani na njama zingine zinazofanana na hizo kama vile kuwafanyia mtihani wanafunzi wao, kwa lengo la kuongeza kiwango cha ufaulu, ili shule husika ipate sifa kubwa.
Madhara ya udanganyifu, hujitokeza pale mwanafunzi anapofaulu kwa alama za juu na kuchaguliwa kwenda shule za vipaji maalum, lakini mwanafunzi huyo anashindwa kufanana katika uwezo wa kitaaluma katika shule hiyo anauojiunga, jambo linalowashangaza walimu wa shule za vipaji maalum.
‘MAJIPU’ YA TCU
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Yunis Mgaya, anakiri kuwepo udanganyifu katika elimu katika ngazi ya vyuo vikuu, hali anayoieleza inatishia uhai wa elimu kitaifa.
Anasema wanafunzi wanaofanya vitendo hivyo, nao wanapaswa kuitwa mafisadi wa elimu.
“Tumeshafahamishwa na tunafuatilia. Wanafunzi hao wanapaswa kuitwa mafisadi, kwa sababu wanapata elimu ambayo hawajaitolea jasho,” anasema Profesa Mgaya.
Anaeleza kuwa suala hilo ni tatizo la dunia nzima na siyo Tanzania peke na inachangiwa na wakufunzi na wahadhiri walioko vyuoni, wanaoletewa andiko (draft) la kwanza hadi la mwisho, bila ya kuwapo na kosa lolote, huku mhadhiri au profesa anayemsimamia mwanafunzi huyo hashituki juu ya walakini huo.
Profesa Mgaya anasema TCU kwa kushirikiana na baadhi ya vyuo vikuu nchini, kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mzumbe na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), wameanzisha programu ya kuzuia wezi wa kitaaluma inayoitwa Turnpin.
Anasema mwongozo huo unamsadia msimamizi wa utafiti kutambua iwapo andiko hilo la utafiti limeshawahi kuchapishwa.
Mkuu huyo wa TCU anasema kazi yote ya mwanafunzi huingizwa katika programu hiyo, ambayo inatafuta kila sehemu na kurudisha majibu kwa asilimia kadhaa ya ukweli wa kazi hiyo.
Anasema endapo programu hiyo itarudisha majibu yanayozidi asilimia 30, ina maana kazi hiyo imenakiliwa kutoka sehemu nyingine, hivyo mwanafunzi atachukuliwa hatua kama vile kufukuzwa chuo au kurudia masomo au andiko lake.
Profesa Mgaya anafafanua kuwa, endapo majibu yakiwa chini ya asilimia 30, mwanafunzi huyo anaruhusiwa kuendelea na kazi yake, kwa kuwa haijafanana na kazi zingine kwa kiwango kikubwa.
Anatoa mfano binafsi kwa kauli; “Niliwahi kumkamata mwanafunzi mmoja wa Masters (shahada ya uzamili) wakati nikiwa UDSM (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam), ambaye alikuwa amenakili kazi na alirudia mwaka wake wa masomo,” anasema Profesa Mgaya.
Anasema wanafunzi kuandikiwa utafiti, chimbuko lake linaanzia nyumbani ambako mzazi au mlezo anamfanyia kazi za kitaaluma) mtoto huyo anaporudi kutoka shule.
NECTA NA KINACHOJIRI SHULENI
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), Dk. Charles Msonde, anasema kuwa wizi katika mitihani na kupata vyeti feki ulikuwapo kabla ya mwaka 2007.
Anasema Necta ilikuwa inatoa vyeti vya wanafunzi bila kuwa na picha ya mwanafunzi husika, hivyo iliwapa mwanya wadanganyifu kuchapisha vyeti visivyo na uhalisia.
Dk. Msonde anasema kuwa, ilipofika mwaka 2008, Necta ilianza kutoa vyeti vyenye picha ya mwanafunzi husika, jambo lililopunguza wimbi la kutengeneza vyeti bandia.
“Ni kweli kuna udanganyifu katika elimu, lakini ilipofika mwaka 2008 udanganyifu huo ukaanza kupungua. Ki – ukweli, tunajitahidi kupambana na udanganyifu,” anasema Dk. Msonde.
Anafafanua kuwa, mwaka 2011 waliwakamata wanafunzi zaidi ya 9,000 waliokuwa wamefanya udanganyifu katika mitihani ya mwisho.
Dk. Msonde anasema uliofuata – 2012. idadi ya wadanganyifu ilipungua hadi kufikia wanafunzi 263. Hiyo ni sawa na asilimia 2.92 ya wadanganyifu wa mwaka uliotangulia -2011.
Anasema kuwa, mwaka 2013 idadi ya wadanganyifu ilipungua zaidi na kufikia 13, wakati mwaka 2014 hakukuwepo kabisa, huku mwka jana akiwepo mmoja pekee.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Rising Bird, Ephraim Solomon, anathibitisha kuwapo udanganyifu huo katika elimu na sasa ni kuna shule nyingi zinazotumia mbinu chafu katika kufaulisha wanafunzi wao.
Anasema elimu sasa imetekwa na mtazamo wa biashara kwa asilimia 75 na katika shule binafsi hasa za sekondari, ufundishaji wake si wa kumuandaa mwanafunzi kujitegemea, bali kutafutiwa ajira.
Solomon anataja sehemu ya kasoro hizo kuwa katika shule nyingi binafsi, mwalimu anamtafutia elimu mwanafunzi kwa asilimia 90, jambo ambalo mwanafunzi anapofaulu na kwenda katika shule za vipaji maalum anashindwa kuendana na mazingira ya shule hiyo.
Mkuu huyo wa shule anaainisha kuwa shule za vipaji maalum, mfumo wake wa ufundishaji ni kwamba walimu wanafundisha kwa asilimia 30 tu na asilimia 70 zilizobaki ni kwa mwanafunzi kijitafutia.
“Hata elimu ya msingi, mitihani yake haimjengi mwanafunzi. Utakuta mtihani wa mwisho unakuwa wa ‘multiple choice’ (mfumo wa kuchagua). Sasa hapo kweli utasema umetunga mtihani wa kumpima mwanafunzi?” anahoji mwalimu Solomon.
Dk. Ayub Rioba, mhadhiri katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anaunga mkono hoja hiyo akikiri uwepo wa hujuma za kitaaluma.
Anafafanua namna nyingi hadaa hizo zinavyofanyika, ikiwamo walimu kushirikiana na wamiliki wa shule kuiba mitihani na kuwapa majibu wanafunzi.
Dk. Rioba anafafanua kuwa hiyo hufanyika kabla ya kuingia katika chumba cha mtihani au wanafunzi wakiwa katika wanafanya mitihani.
WAHADHIRI WANENA YANAYOWAKABILI
Mwanataaluma kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine (Saut), Profesa Mwesiga Baregu, anasema kuwa hivi sasa taifa lipo katika hali mbali ya kutengeneza bomu la vijana kutoka kwenye mfumo wa elimu unaowandaa.
Anasema udanganyifu hivi sasa ni mkubwa vyuoni na kuna haja ya serikali kuandaa tume ya wataalam watakaotafuta ufumbuzi wa tatizo hilo na kutoa mapendekezo mahsusi juu ya nini kifanyike katika kujinusuru na janga hilo.
Profesa Baregu anashauri serikali irudi nyuma na kufanya tathmini kama ilivyowahi kufanyika nchini Marekani mwaka 1980, walipowaita wajuzi na kufanya utafiti wa kupata uhalisia wa ‘jipu’ lililomo ndani ya mfumo wa elimu.
Anafafanua kuwa, ripoti hiyo iliyopewa jina la ‘a nation at risk’ (taifa liko hatarini) lilitoa mapendekezo ya nini kifanyike katika kuboresha elimu na ikawa na manufaa mengi.
Mtaaluma huyo mwandamizi katika fani ya sayansi ya siasa, anasema mfumo wa elimu nchini umekosa mtu maalum anayeuongoza, kwani inaonekana imegawanyika katika maeneo tofauti.
Profesa Baregu anasema hivi sasa elimu inasimamiwa na mamlaka tofauti, ambazo ni Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.
Naye Dk. Rioba, analaumu kuwa mfumo wa elimu nchini umeingiliwa na watu wanaopenda mambo ya mkato na sasa kuna utamaduni anaouita wa “uongo uongo” uliojengeka katika sekta ya elimu.
Anatoa mfano wa katika vyuo vikuu, kwamba wahadhiri hawasimamii vyema utafiti wa wanafunzi wao kutokna na kuwepo ama mazingira yasiyo rafiki kutekeleza majukumu au wao kurahissha mambo.
Dk. Rioba aliyewahi kuwa mwanahabari katika baadhi ya taasisi nchini, anasema kuna wahadhiri wanaowasiliana na wanafunzi kwa njia ya mtandao wakati wanaposimamia utafiti wao, jambo analosema si sahihi.
Anasema ni jambo linalotokana na wasomi kutingwa na majukumu ya kikazi, hivyo wanakosa muda wa kusimamia na kupitia kwa umakini maandiko ya utafiti husika.
Dk. Rioba anasema kuna wakati mtaaluma husika anamamia maandiko ya utafiti wa wanafunzi kati ya 20 na 30, jambo linalomfanya aelemewe na kuwepo usimamizi duni unaoishia katika ubabaishaji wa kazi hiyo.
Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (Duce), Profesa William Anangisye, analalamika kwamba hivi sasa taifa linapotoka kutaaluma.
Anasema kuna wanafunzi wa vyuo vikuu wanaopata daraja nzuri katika maandiko ya utafiti wao, kumbe katika uhalisia kuna ubabaishaji na kuifanya taifa litengenezea wasomi mbumbumbu.
“Sina uhakika na wala sijawahi kuona au kumkamata mwanafunzi aliyeiba research (utafiti) wa mtu au ameandikiwa, ila nimewahi kusikia. Ki -ukweli kama hayo mambo yanafanyika kweli, tutakuwa na wakati mgumu wa kutengeneza wasomi,” anasema Profesa Anangisye.
Anashauri taifa liimarishe mfumo bora wa elimu kuanzia Chekechea ambako ndiko mwanafunzi anaanza kupikwa hadi ngazi za juu.
Profesa Anangisye anasema kuwa, katika maadili ya elimu, mwalimu kuiba mtihani, kusaidia kufanya mtihani au kutoa majibu ni kosa kubwa.
Wasomi hao wanasema kuwa, changamoto hizo ndizo zinajaa jipu la vijana kutoajiriwa baada ya masomo, huku kukiwepo walakini wa kukosa sifa ya kuingia katika soko la ajira.










