Tumeshuhudia miaka kadhaa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF) kikisimamia na kuendesha Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Pili na Tatu bila ya kuwa na mdhamini na zote zilikuwa na ushindani.
Hata sasa wakati FDL imelamba udhamini, bado klabu zimeendelea kucheza kwa 'mkopo' mithili ya michuano ya FAT wakati ule.
Klabu zilizoshiriki FDL msimu huu, zinaidai TFF fedha za udhamini kutokana na kile kinachodaiwa kuwa shirikisho hilo limetumia 'mpunga' huo katika masuala mengine.
Ni lini TFF itakuwa tayari kuendesha Ligi Kuu ya Wanawake au Ligi ya Taifa kwa ajili ya kutoa nafasi kwa wachezaji wasichana kuonyesha vipaji vyao?
Shirikisho hilo lenye mamlaka ya soka nchini limekuwa mara kwa mara likiibuka na mipango ya kuanzisha ligi hiyo, lakini utekelezaji wake hauonekani.
Timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars) imekuwa itolewa hatua za awali katika michuano ya kimataifa, lakini wahusika wanaonekana kutoshtushwa na mwenendo huo mbovu.
Kutokana na desturi hiyo ya kutotekeleza programu za maendeleo ya soka la wanawake, aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Rogasian Kaijage, aliamua kuachia ngazi.
Kaijage katika maelezo yake alisema anaamini anaweza kuisaidia Twiga Stars akiwa nje ya timu na anaumizwa kuona shirikisho haliipi matunzo na kipaumbele timu hiyo na ile ya umri chini ya miaka 20 (Tanzanite) kama huduma wanazopata wenzao Taifa Stars.
"Wanangu na wajukuu zangu wa Twiga na Tanzanite, nasikitina sana kuwaacha njiani, lakini imebidi iwe hivyo kwa sababu mazingira hayanipi mwanya wa kuwasaidia kuwapa maendeleo niliyokusudia.
"Nawaomba msikate tamaa, muongeze bidii Mungu atawasaidia, nami nitakuwa nanyi muda wote. Bora nitafute njia nyingine za kuwasaidia nikiwa nje ya timu. Kumbuka ilibidi Yesu afe ili watu wakombolewe, hivyo nami inabidi nitoke ili kuamsha ukombozi wenu, bado niko nanyi. Nawapenda sana," aliandika Kaijage katika ukurasa wake wa Facebook hivi karibuni.
TFF YANENA
Baada ya Twiga Stars kupoteza mechi ya kwanza katika kampeni ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Zimbabwe mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine, alisema shirikisho hilo mwaka huu limepanga kuchezesha ligi katika mazingira ya aina yoyote.
Mwesigwa alisema anaamini ligi ndiyo njia pekee ya kuzalisha wachezaji wapya na waliopo kupata nafasi ya kucheza zaidi na kujiimarisha.
"Hakuna njia ya mkato, Zimbabwe ni timu kubwa na ili na sisi tufike huko, hakuna namna, ni lazima tucheze ligi, kama shirikisho tunaahidi mwaka huu ligi itachezwa, tuna wachezaji wazuri lakini wanahitaji kupata mechi nyingi zaidi kabla ya kuingia kwenye mashindano," alisema.
NASRA: TUTASONGA MBELE
Wakati timu yake haijawahi kuifunga Zimbabwe katika mechi zote walizokutana, kocha mkuu wa Twiga Stars, Nasra Juma, anasema bado kikosi chake kina nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo lakini kinahitaji maandalizi zaidi.
Nasra aansema ni vigumu timu kupata matokeo mazuri bila ya kuiona ikicheza mechi ya kujipima nguvu na kinachowasaidia kwa sasa ni uzoefu wa wachezaji wa timu hiyo ambao wengi wamecheza pamoja kwa zaidi ya miaka mitano.
"Tuna changamoto nyingi za kiufundi, ila baada ya kuwajua wapinzani wetu, tuna nafasi nzuri ya kuwafunga katika mechi ya marudiano, wachezaji wawili waliopata majeruhi (Sophia Mwasikili na Shelder Boniface) mapema ndiyo waliharibu mipango yangu, tuombe uzima, hakuna lisilowezekana," Nasra anasema.
"Mchezo wa marudiano (Zimbabwe) hautakuwa mgumu kwetu licha ya kwamba tutacheza ugenini kwa sababu tayari tumeshajua ubora na udhaifu wa wapinzani wetu."
Twiga Stars ililala 2-1 nyumbani kwenye Uwanja wa Azam jijini Dar es Salaam. Timu hizo zitarudiana mjini Harare kati ya Machi 18-20 na mshindi atakutana na Zambia au Namibia katika hatua inayofuata.










