Kipi cha kujivunia Siku ya Wanawake Duniani?

08Mar 2016
Nipashe
Kipi cha kujivunia Siku ya Wanawake Duniani?

NI miaka 71 tangu Umoja wa Mataifa (UN), kupitisha maazimio ya tarehe ya leo kila mwaka kuwa siku ya maadhimisho ya siku ya wanawake kwa lengo la kupaza sauti zao juu ya ukandamizaji na ukatili ambao umewafanya washindwe kushiriki maendeleo endelevu ya familia na taifa kwa ujumla.

Wanawake wakiwa katika maandamano ya sikukuu ya wanawake duniani

Chimbuko la Siku ya Wanawake Duniani lilianza miaka mingi na mwaka 1911, baada ya Wanawake nchini Marekani kuandamana kudai haki zao ambazo walikuwa wakizikosa: kama vile kulipwa ujira mdogo, kufanyishwa kazi ngumu na kwa masaa mengi, kukosekana kwa huduma za jamii na ubaguzi wa kijinsia.

Kila mwaka maadhimisho haya yanafanyika na kubainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake na kuwa kikwazo kikubwa cha kusonga mbele katika kujikwamua kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa.

Miongoni mwa changamoto ambazo wanawake wa Tanzania wanakumbana nazo, ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia na athari za kiafya, wanawake kutopewa haki sawa katika maamuzi na kutoshirikishwa.

Nyigine ni wanawake katika jamii hutoa mchango mkubwa katika kutunza familia, lakini bado wanaathirika zaidi na maradhi kama vile Ukimwi, vifo vinayotokana na uzazi, kupigwa, kutukanwa, kutelekezwa, kubakwa, ukeketaji, mauaji ya vikongwe, mimba za utotoni na kunyimwa haki ya kumiliki mali.

Katika maadhimiso haya, kila mwaka kuna kauli mbiu na tathimini ya pamoja kutafakari namna changamoto zilivyotatuliwa na kupanga namna ya kukabiliana nazo.

Maadhimisho haya ambayo yamefanyika miaka yote kiasi cha kufikia umri wa mtu kuishi duniani kama ulivyotajwa katika vitabu vitakatifu; asilimia 25 ya watoto wako katika ndoa za utotoni na kichocheo kikubwa kikiwa ni mkanganyiko wa sheria ya Ndoa ya mwaka 1977 na Katiba ambavyo vinakizana katika umri.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali InterNews Tanzania na Ubalozi wa Canada, wanatoa elimu ya kuisaidia jamii kuacha na kupinga ndoa za utotoni ambazo ni kinyume cha haki za binadamu kwa kuwa zinaruhusu mtoto wa kike kunyanyaswa na kukosa elimu.

Mashirika hayo na Ubalozi wameyakutanisha mashirika yanayotetea haki za watoto wa kike nchini ili kuunganisha nguvu kwa pamoja kupinga ndoa za utotoni zinazoleta mimba za utotoni, lengi ni kuwa na sauti kubwa ya kuelekeza jamii kuhakikisha mambo mabaya yanayofanyika kwa watoto wa kike hayafanyiki.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga, anasema tatizo la ndoa za utotoni ni kubwa kwa kuwa watoto wananyimwa fursa za kuwa watoto, haki zao zinakiukwa na wale ambao walipaswa kuwa mstari wa mbele kuwatetea, wanashiriki kuwakandamiza kama kupokea mahari ili waoelewe badala ya kusoma.

Anasema mbali na wazazi kama walezi wa kwanza na waamuzi wa maisha ya mtoto wao, lakini walimu na viongozi ni watetezi wengine ambao wanapaswa kuwafunza na kuandaa mazingira rafiki, wanapokuwa shuleni waweze kusoma na kufanya vizuri kama wasichana.

“Lipo tatizo kubwa kwa watoto wa kike waliovunja ungo kushindwa kwenda shule kwa siku zote anapokuwa katika siku zake kwa sababu anaona aibu, hakuna miundombini mizuri ya choo ya kumwezesha kuwa safi muda wote wanapokwenda kujisaidia au kubadili taulo na hajaandaliwa kisaikolojia kuifikia siku hiyo,” anafafanua.

Anasema kutokana na hali hiyo mwanafunzi wa kike hujikuta amekosa shule kwa siku tano ambazo wenzake wameendelea na masomo na ukizijumlisha zote kwa mwaka ni nyingi na kwa namna moja au nyingine zinaathiri taaluma yake.

Sanga anasema utafiti wa Tamwa unaonyesha kuwa wasichana wengi wanaingizwa katika majukumu ambayo hawakutoa ridhaa nayo, kama vile kufanyishwa biashara ya ngono na kuozeshwa kwa lazima jambo ambalo linaonyesha kuwa ubaguzi wa kujinsia bado ni tatizo kubwa.

“Ndoa za utotoni ni tatizo kubwa na suluhisho lake ni lazima liwe la kitaifa, wasichana waachwe waingie kwenye mahusiano na watu wanaowapenda na kuchagua wenyewe na siyo kubanwa katika utumwa ambao unawaathiri kisaikolojia kwa kuingizwa kwneye majukumu mazito ya kifamilia na ndoa asiyoyaweza na kuathiriwa kibaolojia wakati wa uzazi,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa InterNews Tanzania, Valeria Msoka, anasema kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwaka jana ulifanyika mkutano wa kupinga ndoa za utotoni nchini Zambia na kuwaleta pamoja marais na wake wa marais, mawaziri na viongozi wa kimila ambao walitoa tamko la kukataa ndoa hizo na kwenda kusimamia katika nchi zao.

Anasema yote yalifanyika chini ya siku ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike Novemba 11, Canada, Zambia na UN wote wakiwa na lengo la kuelimisha jamii na kuwezesha mtoto anayezaliwa kujua anapendwa, analindwa na anawezeshwa kutimzia ndoto yake.

Mkurugenzi huyo anasema kwa mujibu wa utafiti waliowahi kufanya vinavyochangia ni mfumo dume, usiri, baadhi ya viongozi wa dini, kukosekana kwa miundombinu rafiki kwenye shule nyingi, umbali wa shule na kutoa nafasi kwa wanafunzi kurubuniwa.

Nyingine ni wanaoishia darasa la saba katika umri mdogo wanashindwa kujiamualia na wenye jukumu la kuwalinda hushiriki uharamia huo na kukosekana kwa utashi wa kisiasa kwa baadhi ya viongozi.

Mathalani, mkoani Shinyanga mtoto anapoonekana anafanya vizuri shuleni na wazazi wanataka afeli huamishwa shule kwa kisingizo cha wazazi kuhama eneo lakini huishia kuolewa.

“Kila mtu anatakiwa kuhakikisha mtoto wa kike anabaki kuwa mtoto wa kike na siyo mke wa mtu,” alisema Msoka.
Anasema kuendelea kupoteza watoto wa kike kwa ndoa za utotoni kuna hatari kubwa ya kuwa na watoto wa kike wasiojitambua, haki zao zilizopo katika misingi ya UN zinafinywagwa.

“Tuwe na ubunifu katika mbinu mpya ili kuhamasisha viongozi kupitia nafasi walizonazo watoto wapate haki zote hasa ya elimu, mkanganyiko uondolewe ili kupeleka sauti moja serikalini kwa kushirikiana na vyombo vya habari,” anabainisha.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), nchini umebaini mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa ndoa za utotoni kwa asilimia 59 ukifuatiwa na Tabora asilimia 58.

Mikoa mingine na asilimia zake kwenye mabano ni Mara (55), Dodoma (51), Lindi (48), Mbeya (45), Morogoro (42) na Singida (42).

Aidha, Unicef imekadiria kuwa ifikapo mwaka 2050 watoto milioni 310 wana uwezekano wa kuwa katika ndoa za utotoni; na kila wasichana watano kati yake wawili wameingia kwenye ndao za utotoni.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Agape Aids Control Program mkoani Shinyanga, John Myola, anasema changamoto kubwa kwa mkoa huo ni mila na desturi zilizopitwa na wakati zinazosema mtoto wa kike hana haki ya kusoma bali kusubiri kuolewa kwa kuitajirisha familia kupata mahari ambayo ni ng’ombe.

Nyingine ni mgogoro ndani ya familia kwa mtoto kukosa ulinzi kwa walezi wake na mahitaji ya msingi na kuingia katika vishawishi katika umri mdogo na wakati mwingine wazazi kumtengenezea mazingira hayo.

Myola anasema nyingine ni vyombo vya dola kama polisi na vya maamuzi kama Mahakama na madaktari kushindwa kutoa haki kwa haraka na wakati mwingine kukubali rushwa ili kuharibu ushahidi na kesi kwa ujumla.

“Ipo mifano katika eneo letu kesi ambayo imeharibiwa na Daktari kuandika ripoti isiyo ya kweli ya mtoto aliyebakwa, Polisi kushindwa kufanya upelelezi unaotakiwa na Mahakama kutoamua kesi kwa haki, ukifuatilia kwa undani sababu kubwa ni rushwa,” anasema.

Anatoa mfano wa tukio la binti wa miaka nane aliyebakwa na kijana wa kiume na kila mwenendo ulionyesha binti ameingiliwa kimwili, lakini ripoti ya daktari ilisema haionyeshi kama binti huyo ameingiliwa kimwili.

Anasema mazingira kama hayo na hukumu za namna hiyo, zinachochea watendaji wa makosa hayo kuona ni haki na sahihi kuendelea kufanya hivyo.