Wanaume wanavyotelekeza familia kisa ukosefu wa samaki

30Oct 2022
Augusta Njoji
Mtera
Nipashe Jumapili
Wanaume wanavyotelekeza familia kisa ukosefu wa samaki

KATIKA sehemu ya kwanza ya ripoti hii jana, kulikuwa na ufafanuzi kuhusu shida zinazoikabili jamii ya Mtera wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma kutokana na kuadimika kwa samaki kwenye Bwawa la Mtera. Endelea kufuatilia kinachowasibu na mustakabali wake.

Wauzaji wa samaki katika geti la Mtera wakisubiri wateja kwenye barabara ya Iringa-Dodoma eneo la Mtera. Samaki wanaouzwa eneo hilo kwa sasa wanatoka Tabora baada ya Bwawa la Mtera kukumbwa na uhaba wa samaki. PICHA: AUGUSTA NJOJI

WAVUVI WABAKI 10

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Chungu, Andrew Kiparamoto, anasema ni mwaka wa nne sasa hali ya bwawa hilo sio nzuri na kuathiri uchumi wa wananchi wake.

“Wengi wamehama na kutelekeza familia na kufunga biashara, kinababa wametelekeza wake zao na watoto,”anasema.

Kiongozi huyo anasema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa kinamama kuwa hata wakiwapigia simu waume zao kuwajulisha kuhusu hali za familia, nao wanawapa mrejesho kwamba huko waliko nako hali sio njema kiuchumi.

"Wanawake wanasema hata kinachotumwa wakati mwingine hakikidhi mahitaji kwa sababu mtu ameacha mke na watoto, tena wanasoma na wana mahitaji ya shule, chakula lakini anatuma Sh. 10,000, anafika kwa wakala anapata Sh. 8,000 halafu unasema atumie kwa makini baada ya mwezi wakati hata mahitaji ya siku moja haitoshi," analalamika kiongozi huyo.

Anasema wanawake waliotelekezwa na waume zao wanaishi kwenye mazingira magumu.

“Hakuna mzunguko wa fedha, nilikuwa na maduka sita lakini yanayotoa huduma kwa sasa ni mawili, mengine yamefungwa. Hakuna kipato kabisa, nilikuwa na wavuvi zaidi ya 300, sasa hawazidi 10," anabainisha.

Kiparamoto anasema serikali iangalie namna ya kutoa mikopo yenye riba nafuu ili wanawake wafanye ujasiriamali utakaosaidia wajikwamue kiuchumi na kutoa huduma kwa familia zao.

UONGOZI KIJIJINI

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mtera, Angela Minja anasema pamoja na mabadiliko ya tabianchi kuathiri upatikanaji wa samaki kwenye bwawa hilo, pia kuna shida nyingine ya nyavu zinazoitwa 'timba' zilizotumika kwenye uvuvi haramu na kusababisha uhaba huo.

Anasema kwa sasa hali ni mbaya kwenye eneo hilo kutokana na watu kuhama na kibaya zaidi kuna anachokiita kinababa kuacha kinamama na watoto.

"Katika suala la kuacha shule, tumeshaletewa majina ya wanafunzi hapa ofisini ambao walifaulu kuingia kidato cha kwanza, tukaita wazazi ambao wa kike ndio wanapatikana wanasema fedha za kununua sare za shule na madaftari hawana na baba zao hawapatikani, kwamba wanapoondoka hata mawasiliano yanakuwa magumu.

"Hali ya kiuchumi sio nzuri, ninaletewa malalamiko mengi hapa ofisini kinamama uchumi umeyumba, wanalazimika kuingia kwenye mikopo.

"Mama anashindwa kuhimili familia, anaingia kwenye mkopo, mwisho wa siku anashindwa kulipa mikopo na kufunguliwa mashtaka, mpaka sasa malalamiko ya namna hii tumepokea zaidi ya 20.

"Wakiulizwa, wanasema ni hali ya kiuchumi na waume zao wameondoka na hawapatikani, kwamba ameenda kwa shughuli za kiuvuvi Tabora, Singida au Bahi," anafafanua.

Ofisa huyo anasema halmashauri ilikuwa inategemea mapato mengi kwenye shughuli za uvuvi, akibainisha kuwa kata nzima kwa mwezi ilikuwa inapata kati ya Sh. milioni nne na sita lakini kwa sasa hata kwa siku wanaweza wasikusanye mapato yoyote na kwa mwezi mapato ya samaki hata Sh. 100,000 hazifiki.

"Hali imekuwa mbaya wilayani wanakuja wanaangalia hadi bwawani lakini hamna kitu. Kila siku wavuvi wanakuja kuchukua barua za kusafirisha mitumbwi yao kupeleka maeneo mengine, wanasema hali ya hapa ni mbaya.

"Mwenyekiti wetu wa kijiji sisi ni mvuvi, hayupo kwa sasa, kaondoka. Hata wajumbe wa serikali ya kijiji wamebaki 10 kati ya 25 wanaotakiwa. Kuna wakati hata shughuli za kiserikali zinazohitaji uamuzi wao inakuwa tatizo kwa sababu akidi ya vikao haitimii," anasema.

Hoja ya uvuvi haramu kuwa sehemu ya uhaba wa samaki kwenye Bwawa la Mtera, inaungwa mkono na mvuvi Kodi anayesema bwawa hilo lina aina mbalimbali za samaki lakini wanaoongoza na kukuza uchumi kwa haraka ni perege  ambao sasa hawapatikani huko.

"Uvuvi haramu umechangia hali hii. Miaka ya nyuma wakati samaki wanatoka kulikuwa na uvuvi haramu uliokithiri, kuna nyavu za sumu aina ya timba zimechangia sana, wataalamu wanasema nyavu hizo hutumika kwa ajili ya utafiti na zinatoka Kigoma, Tunduma na Zambia," anasema Kodi.

MAHUDHURIO SHULENI

Mwalimu wa Taaluma katika Shule ya Msingi Mtera Dam, Fadhilahi Mkulungu anasema mahudhurio ya watoto yameathirika kutokana na wakazi wengi wa eneo hilo kuwa wavuvi.

"Kuna utoro wa rejareja, yaani kuna kundi ambalo wamehama na watoto lakini kuna ambao wamehama lakini wameacha watoto, unakuta ndio tatizo kubwa. Kuna watoto sasa wamegeuka kuwa wazazi, ni tatizo ambao linatuathiri kwa sasa," anasema.

Anatolea mfano kuwa darasa la saba shuleni kwake mwaka huu lilikuwa na wanafunzi wasiopungua 15 ambao walikuwa na mahudhurio ya kulegalega na kati yao, sita wameshindwa kufanya mtihani wa kuhihitimu elimu ya msingi.

"Kwa darasa la nne pia kuna watoto zaidi ya 15 ambao hadi sasa huenda wasifanye mtihani kabisa kutokana na utoro kutohudhuria shuleni zaidi ya miezi miwili, dakika za mwisho hizi tunawatafuta," anasema.