- wanadaiwa wanavamia watu usiku hasa wale waliopenda kutembea usiku wa manane au walevi na kunyonya damu zao kwa kutumia vifaa walivyonavyo.
Ikadaiwa watu wanaofanya kazi hii hutumwa na watu wengine kutoka nchi za nje ambao huuza kwa bei kubwa.
Zikawa taarifa za kukutwa kwa miili ya watu wakiwa wamekufa huku ikiwa imegongwa mihuri kuonyesha kuwa marehemu kanyonywa damu.Na ikawa inasemekana kuwa hata askari polisi wakiikuta maiti imepigwa mhuri basi hapo tena hakuna kesi, wanajua kuwa mtu huyo amenyonywa damu, hivyo wanawapa tu ndugu wakazike na kesi inaishia hapo.
Na wengi wa watu ambao walikuwa akisemwa kuwa ni wanyonya damu walikuwa ni watu wenye kipato. Hivyo kipato chao kuhusishwa na unyonyaji wa damu.
Pia wakawa wanahusisha kuwa wana mahusiano ya serikali kwa sababu damu inayopatikana nyingine pamoja na kuuzwa, iliyobaki inapeleka hospitalini kwenye akiba ya damu.
Ukikaa na watu wa zamani wana historia na hadithi nyingi za aina hiyo, kila mmoja atakusimulia kivyake lakini huwezi kukuta hata mmoja mwenye uhakika na anachokisema.
Kwenye mikoa au majiji yote nchini zipo hadithi hizo, na Dar es Salaam sehemu ambazo zilikuwa maarufu na uvumi wa wanyonya damu.Sehemu hizo ni kama Buguruni, na Mwananyamala ambapo hata jina lenyewe maana yake ni 'mtoto nyamaza' kwa lugha ya kizaramo, kwani wakati huo ilikuwa ni porini tu na wakazi walikuwa wachache.
Kulikuwa na uhalifu wa kukaba watu, lakini wengi walihusisha na watu hao wanaoitwa 'mumiani'.
Kulikuwa na watu maarufu pande mbalimbali za nchi wakati huo hasa waliokuwa na uwezo mkubwa kipesa walikuwa wakihusishwa na kazi hiyo, wakiogopwa na baadhi ya akinamama na watoto.
Wakati mwingine hata mitaani tu, sokoni na sehemu zingine likionekana gari ambalo wana wasiwasi nalo na hasa lenye rangi nyekundu, basi watu wataanza kutimua mbio bila kuuliza na wakifika majumbani huzusha stori kuwa wamewaona wanyonya damu.
Twende kwenye miaka ya 1970 hadi mwishoni mwa miaka ya 1980, stori za mumiani zilihamia mashuleni.
Nako huko ndiyo balaa kwani ikionekana gari yenye rangi nyekundu, wanafunzi wanatoka madirishani na kukimbilia majumbani. Kinamama nao wakiona hivyo, khanga mkononi wanakwenda mashuleni kuwawashia moto walimu kuwa wanashirikiana na mumiani kutaka kuwanyonya damu wanafunzi.
Wale watoro wakiona hivyo ndiyo hawaendi shuleni hata mwezi kwa madai kuna wanyonya damu.
Je ni kweli kulikuwa na watu wa aina hiyo? Ukweli ni kwamba hadi leo haijathibitika na zimekuwa ni stori za kufikirika kwani hakuna uthibitisho kamili. Kulikuwa na watu fulani kwa sababu zao wanazozijua walitengeneza vitu kama hivyo kwa kuwatia watu hofu.
Ni kama zile zile tu imani za ushirikina. Watu wanaweza kutengenezewa hofu kuwa fulani ni mchawi wakamhofia kijiji kizima na kumchukia.Wakati ule tatizo kubwa lilikuwa ni elimu. Leo hii utakuta matamasha makubwa ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari huku kukiwa na magari ya msalaba mwekundu wamepaki pamoja na wafanyakazi wake tayari kwa kutoa huduma. Ni kwa sababu hivi sasa si wanafunzi tu, bali hata wazazi wanajua kazi za msalaba mwekundu.
Wakati huo ilikuwa si rahisi kwani linapoonekana gari la msalaba mwekundu tu, basi watoto wote wanatimua mbio. Magari yote yaliyokuwa na msalaba mwekundu yalikuwa yanaogopewa na watoto na hata baadhi ya watu wazima yakinasibishwa na vitu kama hivyo.
Hii ni elimu kubwa imefanyika na serikali imefanya kazi kubwa kuelemisha raia wake hadi leo hii kuona hata mtoto mdogo aliona watu wa msalaba mwekundu ni marafiki na watoa huduma ya kwanza.
Hivi leo tunaweza kujiuliza swali moja tu. Hivi kama wale waliokuwa wakiendesha magari ya msalaba mwekundu wangekuwa wana mpango kweli wa kufanya shughuli hiyo walikuwa na ulazima gani wa kuwa na aina ya gari ambalo linawafahamisha na watu wanakimbia?
Si ingekuwa rahisi kwao kuwa na gari hata la rangi ya bluu wakafanya kazi yao vizuri kwa sababu hawatokimbiwa na mwindo wanayoyataka hivyo kuwapata kirahisi.
Kwa nini wanyonya damu watumie gari jekundu ambalo likionekana kwa watu wanakimbia na wanapata shinda kuwakamata? Kwa nini wasiwe na gari ambalo watu hawatokuwa na wasiwasi nalo ili kazi iwe rahisi kwao?Hapa unaona kabisa kuwa ilikuwa ni uvumi uliokuwa unavumishwa na watu kwa sababu wao binafsi wanazozijua wao kwa ajili ya kuitia hofu jamii, lakini hakukuwa na uweli wowote.Kama kawaida kuna meseji za wadau kutoka kwenye mtandao ya kijamii baada ya mada hii kutambulishwa.
"Mimi nadhani zilikuwa ni propaganda tu za watu, hivi kweli inakuwaje utoe uhai wa mtu kwa ajili ya kuokoa uhai wa mti?" Aliandika mdau mmoja.
Mwingine akakumbushia kuwa kuna watu hasa watoro walikuwa wana tabia ya kulianzisha ili kuzua taharuki na kusababisha wanafunzi kukimbilia majumbani."Hadi hatuendi shule kisa gari jekundu, jamani, halafu saa ingine mmekaa darasani mnashangaa tu ka mtu kanawashtua, 'gari jekundu hilo', hizo mbio zake sio za nchi hii."
Wachangiaji mada hii kwenye mtandao walizidi kufunguka.
"Zilikuwa imani za kijinga tu sisi Mbeya kuna dokta mmoja miaka ya 1990 alikuwa anamiliki hospitali yake, watoto wa miaka hiyo tukimuona tunatimua mbio, eti ananyonya damu ili atengenezee vidonge. Ulikuwa ni ushamba tu na kukosa elimu, si unajua tatizo letu kubwa ni elimu, hata sasa kuna vitu ambavyo bado havijakaa sawa, mawazo ya wengi wetu yamejaa ushirikina shirikina mtu akifanikiwa tunamwita mchawi, hatuamini katika uwezo na matumizi sahihi ya akili na utashi kuleta mabadiliko." Mchangiaji huyo aliandika kwa hisisa kali.
Mama mmoja akaandika, akikumbuka mbali kwani ameshawahi kutimua mbio kwa sababu ya mumiani
"Nimekumbuka mbali, walikuwa wanatudanganya jamani, acha kabisa wanyonya damu hahahaha, aliyeanzisha fikra hizi hakika alikuwa mtu mbaya sana. Ilifika wakati tukawa tunaambiwa kuwa Ubongo wa watu ulitumika kutengeneza dawa za kutuliza maumivu." Baada ya kuanduika haya, mwanamke mwenzake ambaye naye alikuwa mtoto kipindi hicho akamjibu.
"Lakini huwa napata hisia kuwa baadhi ilikuwa wanasumbuliwa na wivu hadi kuibua uzushi kuchafua wenzao, ila walikuwa wakiwatuhumu watu ambao baadhi utajiri wao ulikuwa ni ule unaoleta mashaka." Hapo kuna mwingine akaongeza.
"Nadhani kuna watu walikuwa wanapata utajiri kwa sababu ya kula rushwa, pembe za ndovu, na kwa njia zisizo halali, halafu ukaletwa mpango tu wa kutengeneza mazingira waonekane mumiani ili waogopwe na jamii wasifuatiliwe mambo yao."
Kuna stori ya waumini kutokea dirishani na kutimua mbio baada ya mchungaji wao kuteremka kwenye gari lenye rangi jekundu.
"Kule Rukwa kuna Mchungaji mmoja miaka hiyo alipewa lifti na gari lenye rangi nyekundu baada ya gari lake kupata hitilafu njiani, alipofikishwa kwenye kanisa alikokuwa anakwenda kutoa mahubiri, waumini wote walitokea dirishani kutokana na yeye kuteremka toka gari waliloamini ni la mumiani."
Mada hii inamaliziwa na mmoja wa waliokuwa anapenda sana tukio hili litokee ili wasiende shule."Binafsi nilikuwa napenda hizi habari za za wanyonya damu, maana nilikuwaga napata sababu ya kutoroka shule kihalali.










