Wanahabari tuache uchawa kwa wanasiasa

28Oct 2022
Joseph Kulangwa
Dar es Salaam
Nipashe
Wanahabari tuache uchawa kwa wanasiasa

SASA hivi Mtanzania mwenzangu ukitaka kujua nchi inakwendaje na iko wapi, usikose taarifa ya Kikosi Kazi cha Chifu Hangaya kilichotafiti masuala ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Mimi leo kwa heshima na unyenyekevu, nijikite kwenye hili linalotuhusu la uandishi wa habari, unapofika wakati wa uchaguzi, ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushauriana na vyombo vya habari vya umma, wagombea na vyama vya siasa huandaa mwongozo kwa vyombo vya umma, kwa mujibu wa kifungu cha 53 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

Mwongozo unalenga kutoa fursa sawa kwa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa vyama vyote vya siasa, kuelezea Ilani, sera za vyama vyao na kutangaza habari za mikutano ya kampeni kwa kutumia vyombo vya habari vya umma.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Uangalizi wa Uchaguzi Tanzania (TEMCO) ya mwaka 2015, masuala ya habari husimamiwa na sheria, lakini hakuna chombo kinachosimamia vyombo vya habari kwa ujumla na vyombo binafsi haviwajibiki kisheria kufuata Mwongozo huo.

Hali hiyo imezaa malalamiko kwa wanasiasa, vyama vya siasa (upinzani), watazamaji na waangalizi wa uchaguzi, kuwa baadhi ya vyombo huwa na upendeleo wa wazi, kwa kuchapisha au kufifisha habari za baadhi ya wagombea na vyama.

Kukua kwa teknolojia ya mawasiliano, kumesaidia wanasiasa kuanzisha akaunti za mawasiliano ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram, Telegram na mingine ambayo huitumia kufikia wafuasi wao moja kwa moja na kirahisi, bila kupitia kwa wanahabari wanaowalalamikia.

Ukuaji huo wa teknolojia, umekuja na changamoto zake, mathalani baadhi ya wanasiasa na wadau wamekuwa wakitumia mitandao kusambaza habari za kughushi, kutoa lugha za kuudhi, kejeli, matusi na upotoshaji kwa baadhi ya wagombea.

Hayo sasa, yakasababisha kutungwa kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na Kanuni za Maudhui ya Mtandao za mwaka 2018. Hivi ndivyo tunavyolizwa sasa na sheria hizo zinazokanyaga uhuru wa habari nchini na kilio kinapazwa ili ziboreshwe.

Sasa basi, pamoja na hali hiyo, kilichobainika kwetu wanahabari ni cha kusikitisha, mathalan tunasemwa, kwamba tunakandamiza wapinzani kwa kuwanyima uhuru wa kutumia vyombo vyetu kutokana na vitisho kutoka serikalini; je ni kweli?

Tunatumiwa na wanasiasa kutoa matusi na kejeli kwa wanasiasa wengine badala ya kujadili hoja, lakini pia hatuko huru, kwani tunakuwa na upendeleo wa wazi kwa chama tawala, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi; mnasemaje hapo wananzengo?

Kingine, eti vyombo vya habari vya umma havitoi habari kwa usawa kwa vyama vyote vya siasa nchini; mpo? Halafu tunatuhumiwa kula mlungula mchana kweupe au kujipendekeza tukitarajia kuteuliwa tunapoandika au kutangaza habari katika kipindi cha uchaguzi; mnakataa hilo?

Kumbe watu wamegundua, kuwa sisi na wanasiasa hatuaminiani,kwani baadhi yetu hatutangazi kampeni za wagombea wote kwa usawa na eti ndiyo sababu, uhusiano kati ya vyombo vya habari, vyama vya siasa na wanasiasa huimarika wakati wa uchaguzi na kufifia baada ya uchaguzi; mnaionaje hii, lakini kaukweli kapo.

Lakini kumbe kuna madai, kuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa huelekeza wafuasi wao kushambulia wanahabari au kutotoa ushirikiano kwa baadhi ya vyombo vya habari, wakati wa kampeni; hii si sawa kwa kweli.

Hii sasa ni baba lao, kwamba baadhi ya wanahabari hujinasibisha na vyama vya siasa au kushiriki siasa, huku wakiendelea kufanya kazi ya uandishi wa habari, hali inayoondoa imani ya wananchi kwa vyombo vya habari; nani anabisha hapa, wakati wengine tumewakuta ndani ya magwanda kabisa!

Kwa kweli kuna haja ya kukaa chini na kuangalia nini cha kufanya, ili kuondokana na makandokando haya yanayotuzingira mpaka tuonekane wachafu mbele ya jamii, na hivyo kukosa imani nasi.

Tunashauriwa kuunda chombo cha kusimamia maadili ya wanahabari na vyombo vya habari; ukiwapo pia utaratibu wa kusimamia utekelezaji wa sheria husika, ili vyombo vya habari vya umma vitoe fursa sawa, ya kutangaza habari za wagombea na vyama vya siasa wakati wa uchaguzi bila upendeleo.

Lakini la msingi ni kuandaliwa kanuni zitakazoelekeza vyombo vya habari kuheshimu maadili ya taaluma ya uandishi wa habari, ikiwamo mwanahabari kuhakikisha anahakiki habari kabla ya kuitoa. Tukikosea hapa tumekwisha na tutaendelea kuitwa chawa wa wanasiasa. Alamsiki!