Eliena Malisa, akiwa katika mazingira ya bashasha kumkaribisha mgeni wake mwandishi wa habari wa Nipashe aliyefika katika mgahawa wake ambao kwa jicho la kwanza unaendeshwa kidigitali zaidi.
Muda wote oda kupitia simu hazikomi, huduma mahali hapo ni za kupokezana, mlo wa mchana unapatikana tangu alfajiri, lakini kubwa mwendeshaji ni msomi wa sheria, sasa anaonyesha makubwa katika fani mbili tofauti; masoko na upishi.
Kama Waingereza walivyo na usemi ‘mtoto kama mama yake’ ni aina ya unasaba wa kuiga ameupata kutoka kwa mzazi wake (mama), hata ikambadilisha sasa yu katika makubwa zaidi, lakini akinong’oneza sheria bado imebaki kwenye damu yake, kwani haikwepeki.
Anajitambulisha kumaliza Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro mwaka 2016, lakini baada ya kuhitimu taaluma hiyo ya sheria, akaamua kukifungia kabatini cheti chake na kufungua biashara ya chakula kutokana na uhitaji uliopo sokoni.
Tofauti na migahawa mingine, mwanamke huyo ameamua kuja tofauti kwa kupika vyakula vya mchana wakati wa asubuhi, tena kuanzia saa 12 asubuhi, huku eneo lake la biashara likitambulishwa kwa jina ‘Lunch for Breakfast’ eneo la Survey, jirani na Mlimani City mkoani Dar es Salaam.
Anasema jina hilo linatokana na utafiti alioufanya na akabaini uhitaji wa chakula cha mchana wakati wa asubuhi kwa baadhi ya watu, pindi wanapoamka hutaka kula mlo kamili kabla ya kwenda kazini au kwenye shughuli zao.
Mwanamke huyo anayeendesha mradi huo na kinamama wenzake anasema, alibaini watu wengi wanapenda pindi wanapoamka kula mlo kamili kabla ya kuanza shughuli zao za kila siku.
“Ninaposema ‘ishi kama mfalme’ maana yake mtu anaamka asubuhi anakula mlo wake kamili, mchana anakula kidogo na jioni anakula kidogo zaidi au atakula matunda yake, kisha analala. Hapo hata mfumo wa chakula unakaa vizuri,” anasema.
SIMULIZI ALIKOANZIA
Ilikuwaje akafikia hatua hiyo? Eliena anasema, pamoja na kwamba amesomea sheria, lakini biashara ni kitu anachokipenda na imekuwa ikimpa msukumo mkubwa wa kutafuta vitu vipya kila siku ili kuboresha alicho nacho.
Anasimulia kwamba, kabla ya kufikia biashara hiyo, wakati akiwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, akiwa mwaka wa kwanza katika masomo hayo ya miaka mitatu, akajikuta ametumbukia katika uuzaji wa viatu vya mitumba kwa wenzake.
Eliena anasema, akaanza biashara hiyo baada ya kubaini ni moja ya hitaji kubwa kwa wanafunzi wakati huo, akaunda ubunifu wa kufika sokoni na kuanza ‘kusagura’ viatu vya mtumba na kuuza kwa faida.
“Nilianza biashara ya viatu mwaka 2015 nilipoingia chuoni. Kabla ya kuanza biashara, nilianza kujivalisha mwenyewe, wanafunzi wenzangu wakawa wanavutiwa wakawa wananiagiza.
“Biashara yangu niliifanya kwa mtaji mdogo wa Sh. 100,000 na fedha hii niliipata kwa kujiwekea akiba kidogo kidogo, sikuwa mnufaika wa mkopo wa elimu ya juu,” anasimulia katika mazungumzo hayo yaliyotawaliwa na kuhudumia wateja wenzake kwenye mradi, ikiwamo kupitia oda za simu, hata analazimika kusaidiwa aliyo nao kwenye mradi huo.
Anaeleza kwamba katika miaka mitatu chuoni, akatumia fursa ya soko hilo kwa wanafunzi kufanya biashara na wateja wake wakiwa ni wanafunzi na watu wengine nje ya hapo.
Mama huyo kijana, anasema baada ya kumaliza masomo chuoni, ndipo wazo lingine la kufanya biashara ya chakula likamjia. Hapo akatumia tena usomi wake kwa kufanya utafiti na akabaini, baadhi ya watu wamekuwa wakitafuta mlo wa mchana wakati wa asubuhi na wanaukosa.
“Nikaona ni kitu cha tofauti na sehemu nyingi hakuna huduma hii na binafsi ni mdau wa kula mlo wa mchana wakati wa asubuhi, lakini kila nilipohitaji chakula hiki maeneo mbalimbali, nilikuwa sipati,” anaeleza.
Anasema kutokana na hitaji hilo, ndipo alipoamua kufungua eneo lake la kuuza vyakula vya aina hiyo ili kukidhi mahitaji ndani ya jamii.
Eliena anasema baada ya nafsi ya kibiashara kuidhinisha, akaipa jina la ‘Lunch for Breakfast’ ambayo ameianzisha mwishoni mwa mwezi Agosti, mwaka huu akijinasibu kila siku zinavyoenda , wateja wake wamekuwa wakiongezeka.
Anasema biashara yake imelenga wateja wa kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa sita mchana, ambao anawaandalia vyakula vya aina mbalimbali kama, wali maharage, nyama, maini, pilau, chipsi, mayai na aina nyinginezo za mlo tofauti.
Kwanini biashara ya chakula, anasema anaamini hiyo imetokana na maisha yake tangu utotoni? Ni ufafanuzi kwa Nipashe, kwamba mama yake alikuwa akijishughulisha na upikaji keki, hivyo muda mrefu alitumia kukaa naye, hata ikamsaidia kujifunza mapishi ya aina mbalimbali.
Hivyo, anaeleza utashi uliomhamishia kwenye biashara ya viatu, ambayo imemvusha kwa miaka mitatu, sasa imemuwezesha kufungua eneo la chakula ambalo wateja wake wapo wanaokwenda hapo na wengine akiwapelekea walipo, akifafanua soko linapanuka maradufu .
TAALUMA YAKE
Swali la Nipashe likamrejesha darasani, kwa maana ya cheti chake cha shahada ya sheria, kakihamishia kabatini? Hapo Eliena anarejea katika kilichompeleka Mzumbe hajatekeleza unasaba nao.
Anasema, dhamira ya kusaidia Watanzania wanaohitaji msaada wa kisheria haijafutika kichwani mwake, ingawa bado hajafika katika Shule ya Sheria, kusaka idhini ya kusimama mahakami kitaaluma.
“Mpango wa kurudi kwenye kile nilichokisomea bado upo, nikishaweza kusimamia kitu kimoja kikasimama, ninaweza kuendelea na taaluma yangu ya sheria, kwa sababu ni kitu ninachokipenda,” anasimulia.
Anasema amejikita zaidi kwenye biashara kwa sababu ya mazoea na kitu ambacho tayari ameshakifanya kwa muda mrefu na alipohitimu, akajikuta ameegemea zaidi biashara na siyo kutafuta ajira ya alichosomea.
Anasema licha ya kusomea taaluma hiyo hajawahi kuifanyia kazi zaidi ya mafunzo kwa vitendo wakati alipokuwa chuoni.
Hata hivyo, anabainisha kuwa suala la kila Mtanzania kujua sheria ni jambo la umuhimu na halipingiki.
“Kujua sheria ni muhimu, ukiachana na somo kila mtu anatakiwa kuhakikisha anajua sheria ili imsaidie katika maisha ya kila siku. Sijawahi kuomba kazi kupitia taaluma yangu, lakini mtu akitaka ushauri wa kisheria ninautoa,” anabainisha.
USHAURI WAHITIMU
Mwanamke huyo anawageukia wahitimu wenzake na kuwaeleza kuwa wakijisikia kufanya jambo tofauti na taaluma yao wasisite wafanye.
“Ukianza kufikiria sana mtaji utakuaje, anza na ulichonacho, anza bila kujali makosa wakati ukiendelea yasahihishe makosa utakayokutana nayo katika biashara, uwe na uhusiano mzuri na wateja kwa sababu hao ndiyo wanaokwenda kukuletea wateja wapya,” anasema.
Pia, anaeleza kuwa, wakati wakitaka kufanya kitu wasiogope kuomba ushauri kwa watu wengine ili kuweza kupata mawazo mapya.
“Siyo lazima ufanye biashara zipo kazi ambazo hazihitaji taaluma yako unaweza kuzifanya wakati unasubiri kutimiza ndoto yako, tusikae tu kwa kusubiri lazima kujichanganya,” anasema.