Kuna usemi wa Kiswahili, ‘hayawi hayawi yamekuwa.’ Wiki iliyopita ilitwaliwa na mjadala wa mitaani na kwenye vyombo vya habari, kutathmini kutumia siku 100 za utawala huo mpya na ahadi za Samia kuhusu huduma za wajawazito. Jicho la gazeti lilitua katika Hospitali ya ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Tathmini ya jumla inabainisha kuwepo changamoto kubwa ya nafasi ndogo ya chumba na upungufu wa vitanda vya kupumzikia kinamama wanapotoka kujifungua, huku kukiwepo na ufinyu wa chumba wanachotumia kabla ya kujifungua.
WAZAZI WAFUNGUKA
Baadhi ya wazazi waliojifungua wakisubiri katika mchakati wa kuruhusiwa kutoka hospitalini akiwemo Pili Jumanne (28), mkazi wa Kichanganikatika Manispaa ya Morogoro, anasema wanalazimika kulala kati ya wawili na watatu katika kitanda kimoja, wakisubiri kupimwa na kuruhusiwa muda mfupi baada ya kutoka kujifungua.
Pili anakiri huduma za afya katika hospitali hiyo zimeboreshwa upande wa dawa na mapokezi, pindi wanapofika kusubiri kujifungua, kwani hakutani na mazingira yasityofaa kama vile kunyanyaswa hali iliyokuwepo zamani.
Anasema, hali iliyopo sasa ni kwamba kila mjamzito anazalishwa na mkunga zaidi ya mmoja tofauti na ilivyokuwa zamani alikuwa anapata huduma hiyo kwa daktari zaidi ya mmoja.
Pia anataja kutoweka baadhi ya mambo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakitawala, ikiwa ni pamoja na masimango na lugha chafu.
Aveline Thelasini (29), mkazi wa Mikese wilayani Morogoro, anauanga mkono kuboreshwa huduma ya afya na vifaa tiba na kwa sasa hawalipi hitaji lolote la kujifungua, katika mahitaji kama nyembe na nyuzi kwa wanaojifungua.
Mzazi huyo anataja changamoto kubwa iliyopo ni sehemu ya kupumzikia baada ya kujifungua ndiko wanakokutana na changamoto, wakikosa nafasi ya muda wa kupumzika huku wanalazimika kulaza watoto wao wawili hadi watatu kwenye kitanda kimoja.
Anasema ni hali inayotokea pia wanaposubiri kujifungua, wajawazito hufikia hatua ya kulala wawili katika kitanda, hali inayotokana na upungufu wa vyumba vya kujifungulia.
Wanaelekeza ombi lao kwa Rais Dk. Magufuli, kuangalia uwezekano wa kujenga jengo kubwa na la kisasa litakalokidhi mahitaji ya wazazi hao, kwani ni ahadi ya mtangulizi wake Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Gazeti hili lilishuhudia vitanda tisa pekee katika chumba kidogo cha kujifungulia vikiwa na wagonjwa watatu kila kimoja mwenye watoto wachanga.
WAGANGA WAFAFANUA
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Rita Lyamuya, anasema hospitali ina jumla ya vitanda 30 ambavyo vinatosha kuwahudumia wazazi hao, lakini wanalazimika kujifungua kwenye vitanda tisa pekee, kutokana na udogo wa chumba kwa ajili ya kinamama hao.
Dk. Rita anasema hospitali ina uwezo wa kuzalisha wajawazito kati ya 20 na 30 kwa siku na kwa mwezi inakadiriwa kuzalisha wajawazito kati ya 800 na 900, huku ikikabiliwa na uhaba wa wakunga kuhudumia wazazi.
Anasema wastani unatakiwa mkunga mmoja uzalisha wajawazito watatu kwa siku, lakini uhalisia ulioko katika Hospitali ya Rufaa Morogoro, mkunga mmoja analazimika kuzalisha wajawazito zaidi ya 10.
Dk. Rita anasema pamoja na hospitali kuwa ya Rufaa, lakini inapokea wagonjwa kutoka maeneo yote ya mkoa wa Morogoro wanaofika moja kwa moja kupata huduma bila ya kuwa na rufaa kutoka hospitali yoyote,
Anasema ni hali inayochangia ongezeko la wagonjwa na wajawazito wanaoamini huduma bora zinapatikana hospitalini hapo pekee, jambo ambalo mganga huyo mfawidhi analalamika linasababisha upungufu wa vitanda vya kupumzikia, kabla na baada ya wazazi kujifungua.
Pia anasema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto ya kushindwa kuagiza dawa za kukidhi mahitaji kutika Bohari Kuu ya Dawa za Serikali (MSD), kutokana na deni la Sh. milioni 51 zinazotokana na hospitali kuagiza dawa nyingi kuliko fedha zinazotumwa na wizara husika, kwenda MSD.
Anasema kutokana na changamoto hiyo, wanalazimika kutumia nusu ya makusanyo ya fedha zao hospitali kuilipa MSD, ili kupunguza deni hilo kwa nia ya kulimaliza na wakati huo huo wanaendelea kupokea dawa hizo.
Kwa mujibu wa Dk. Rita, sehemu kubwa ya dawa wanazoagiza kutoka MSD ni za kuhudumia kuhudumia wajawazito na watoto, ambao hawatakiwi kisheria kutozwa gharama yoyote.
Anasema hospitali imeweka utaratibu wa kusghulikia malalamiko yanayotolewa na wagonjwa, kwa kuweka vikao kuyajadili na kutatua changamoto wanapozipata. Miongoni mwa vyanzo vya kupata taarifa, ni kutoka masanduku ya maoni.
Dk. Rita anasema kuwa malalamiko mengi wanyapata kutoka kwenye huduma za upasuaji, ambako wagonjwa wanalazimika kusubiri kwa muda mrefu, kutokana na kuwepo dharura za kila mara.
Mganga huyo anasema wameweka azimio la kupeana taarifa mapema, iwapo kuna upasuji wa dharura, kabla ya kufikia hatua ya kuwapanga wagonjwa wengine wasio wa dharura.
Ombi lake kwa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, ni kwamba waboreshe huduma zilizopo katika Vituo vya Afya, viwe na uwezo wa kuzalisha wajawazito, jambo litakaloipunguzia Hospitali ya Rufaa mzigo wa kuhudumia wajawazito wengi.
MSAADA KWA WAJAWAZITO
Dk. Rita anasema wamewekea utaratibu ulioanza Januari Mosi mwaka huu wa kupokea taarifa za kila mjamzito anayeingia hospitalini hapo hadi anapotoka.
Anasema lengo la kufanya hivyo ni kuwasaidia kwa karibu kutatua kwa haraka changamoto zinazojitokeza katika mwenendo wa afya yao, hali anayoamini utapunguza malalamiko.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Samson Tarimo, anataja takwimu kuwa, mkoa una jumla ya vituo vya afya na hospitali 14 zenye uwezo wa kuhudumia kinamama wajawazito na watoto katika huduma za upasuaji.
Anasema kuwa, kati ya vituo ya zahanati 382 zilizopo mkoani, ni 49 pekee ndizo zinazotoa huduma za kliniki kwa mama na mtoto.
Dk. Tarimo anasema hospitali inasaidia kusimamia huduma za afya ya ngazi ya jamii katika wilaya zote za mkoa na ina inawafikia wajawazito wanaonyonyesha wakiwa majumbani, ili kuwapa msisitizo na kanuni za afya kwa mama anayenyonyesha, uangalizi na lishe kwa mtoto.
Anasema katika kukabiliana na changamoto ya uchache wa watoa huduma, wajawazito na watoto wameanzisha vituo vya kutoa elimu hiyo kwa muda wa mwaka mmoja, ili kupata wataalam zaidi.
Dk. Tarimo anavitaja moja ya vituo hivyo ni Chuo cha Elimu Lugala kilichopo wilayani Malinyi na Chuo cha Afya ya Jamii kilichopo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
MITISHAMBA
Naye Mratibu wa Afya ya Uzazi ya; Mama, Baba na Mtoto wa hospitali hiyo, Santieli Kinyongo, anaeleza masikitiko yake kwa tabia ya wajawazito kunywa dawa za miti shamba, ili kuongeza uchungu unaowawezesha kujifungua haraka.
Anasema kunywa dawa hizo ni hatari kwa afya ya mama na mwanawe hata ksababisha kifo cha mtoto, baada ya kunywa maji machafu iwapo atachelewa kuzaliwa au mama kuchanika mfuko wa kizazi, hali inayolazimisha mfuko huo utolewe kabisa.
Kinyongo anawadokeza siri kinamama, kwamba mjamzito anapofikia hatua ya kusikia uchungu unakuja na kuacha, mantiki yake kibaiolojia ni kwamba njia ya kujifungua inafunguka na ikifika hatua ya uchungu kuwa mkali, kutamfanya ajifungue salama.
Anasema unywaji dawa za miti shamba unasababisha uchungu kuuma mfululizo na mama kukosa nafasi ya njia kufunguka na matokeo yake ni mfuko kuchanika na mzazi kupata ugonjwa wa fistula.
Mratibu huyo wa uzazi anasema kiwa, ni hali inayiomnyima hewa, ambalo ni janga linguine linaloweza kimpotezea uhai au kupatwa kuanzia umri mdogo, akitaja baadhi ya maradhi hayo ni kuwa na mtindio wa ubongo.
Kinyongo anawataka wazazi waamini kuwa, kuna uchungu wa asili unaoanza wenyewe na kuendelea hadi hatua za kujifungua, kwani kumpa mjamzito dawa bila kujua ukubwa wa mtoto na mlalo wake ni kigezo kingine cha kusababisha kifo wakati wa kujifungua.
Anasema kuwa janga hilo klina uwezi wa kufika mbali kwa kusababisha mama kukosa uwezo wa kuzaa tena.










