Tangu nikiwa mdogo mwanafunzi wa elimu ya msingi kwa miaka saba yote, eneo la Ilala Sharif Shamba, jijini Dar es Salaam, kila ama nikienda au kurudi shule nilikuwa nakutana na bibi huyo ambaye alikuwa muuguzi ambaye ni mlemavu wa macho.
Kama walivyokuwa watoto wenzangu, nilipenda sana kumshika mkono na kumuongoza kuelekea kazini kwake katika Hospitali ya Amana, ambayo ni jirani na mahali hapo tulikokutana.
Sikumbuki sana ni kipi kilinivutia nikapenda kumsaidia. Ila kuna cha upekee tulifunzwa shuleni, adabu ya kuwasaidia wahitaji wa namna hiyo.
Nakumbuka mara ya kwanza nilipojitolea kumsaidia kumshika mkono, alinidadisi mambo kadhaa kama vile jina, ninakoishi na shule ninayosoma.
Siku inayofuata anaponishika mkono tu alinitambua, daima hakuwahi kunisahau hadi nilipomaliza darasa la saba, ndipo mawasiliano yetu yalipofifia, kwani baadaye nilihama.
Wastani wa wiki mbili zilizopita, nilikuwa katika eneo la Msimbazi Misheni, kufika nyumbani kwa bibi huyo, ambaye kwa jina lakini ni Theopista Kamugisha.
Mchakato wa kumtafuta niliuanzia katika Hospitali ya Rufaa ya Amana ambako baada ya mchakato huo, niliambatana na muuguzi aliyenielekeza alipo.
Safari hii mimi si msichana au mwanafunzi tena, huku Bibi Theopista naye ameshabadilika, si muuguzi tena, bali ni mstaafu na hanikumbuikio tena. Lakini zaidi ya hapo, zile tabasamu alizokuwa nasi watoto zimeisha. Nagundua mara moja amejawa na huzuni. Hiyo ilikuwa majira ya saa 5.00 asubuhi.
Mara baada ya kukaribishwa katika nyumba aliyopanga katiika chumba cha jirani yake ambaye humpatia ushirikiano wa kimaisha, tukaambiwa anakunywa uji chumbani kwake .
“Nimekuja kukusikiliza,” alitamka Bibi Theopista, muda mfupi baada ya kufika chumba niliko, namo nikajitambulisha kwa kauli: “Mimi ndiye Romana Mallya nilikuwa nasoma Shule ya Msingi Msimbazi Mseto.
“Nilikuwa ni miongoni mwa wanafunzi tuliokuwa tunakusaidia kukuongoza kukutoa nyumbani kwenda kazini na wakati mwingine kukupeleka nyumbani. Lakini sasa nimekuwa mkubwa, nafanya kazi ni mwandishi wa habari… lakini nimeguswa na maisha yako!”
Ilikuwa ngumu kwake katika hatua ya kwanza kukubali kuzungumzia historia ya maisha yake na changamoto zake, kabla na baada ya kustaafu, zaidi akilalamikam haina msaada wowote. Baada ya kushawishiwa na jirani yake, alinielewa na tukaanza mazungumzo yetu yaliyichukua wastani wa saa…..
AFUNGUKA
“Namshukuru Mungu, kwa sababu licha ya kuwa na ulemavu wa macho, nimeweza kuitumikia kazi yangu ya uuguzi kwa uadilifu na upendo na sasa nimestaafu lakini bado nafuatwa na kupigiwa simu wananchi, kuombwa ushauri wa mambo ya afya,” anatamka Bibi Theopista, ambaye sasa ana umri wa miaka 66.
Theopista alistaafu akiwa Muuguzi Mkunga Mwandamizi katika Hospitali ya Amana, mara zote akiirejea ni taaluma aliyotumikia kwa upendo mkubwa.
Anasema baada ya kufanya kazi katika hospitali za serikali na Misheni, alistaafu mwaka 2010 na kufanya kazi kwa mkataba kwa miaka mitatu. Baada ya hapo, amekuwa akiishi katika eneo la Msimbazi Centre, Ilala Dar es Salaam ambako amepanga vyumba viwili anakoishi.
Theopista ambaye anaongea taratibu na kwa hatua, ikichangiwa na umri wake, anasema akiwa kazini hakuwahi kujutia taaaluma na majukumu yake, kwa sababu aliipenda mno kutoka moyoni, tangu angali mtoto.
Anasema alipokuwa katika shule ya msingi, alijikuta akipenda kufanya kazi hospitali, hivyo baada ya kumaliza masomo katika miaka ya 1970, alikwenda kusomea taaluma hiyo ili kutimiza ndoto yake.
SAFARI YA AJIRA NA
KUPOTEZA MACHO
Bila ya kueleza shule na chuo alichopitia, Theopista anasema baada kuhitimu mafunzo ya uuguzi, aliajiriwa na hospitali za Misheni huko huko kwao Bukoba.
Anahimiza kwamba, alifanya kazi katika kile anachokieleza “kwa bidii, unyenyekevu na uadilifu ili kutowakwaza wagonjwa na watumishi wenzake.”
Theopista anasema hakukaa sana Bukoba, kwani aliamua kuhamia jijini Dar es Salaam ambako aliajiriwa katika Hospitali ya Mwananyamala na ndiko janga la macho na kupoteza uwezo wa kuona.
“Nilizaliwa naona. Hata wakati nataka kutimiza ndoto zangu, nilikuwa naona, nikasoma nikamaliza. Lakini wakati nikitumikia kazi niliyokuwa naipenda kutoka moyoni,” anasimulia na kuongeza:
“Ghafla macho yakaanza kuwa na uono hafifu na baadaye kutoona kabisa. Wakati huo nilikuwa ningali binti mdogo, ilikuwa ni miaka ya 1980.”
Matatizo yaliyomfika Theopista hata akapoteza macho ni maradhi ya Trachoma ambayo tiba yake ilikuwa vigumu kupatikana nchini na uwezo wake kiuchumi haukumruhusu kwenda nje ya nchi kutibiwa.
Wakati anapata maradhi hayo yaliambatana na presha ya macho na alishangaa kuona macho yake yanapoteza uwezo wa kuona na hata kufifia kabisa na ndio ukawa mwisho wake kuona.
Anasema kabla ya kupatwa na tatizo hilo, alipenda kufanya shughuli zinazohusu uuguzi.
“Unajua ukifanya kazi unayoipenda kutoka moyoni, lazima uifanye kwa nguvu na ari kubwa, ili hata mwajiri wako ajisikie yupo na mfanyakazi mahiri. Niliipenda kazi yangu na nitaendelea kuipenda,” anasema na kuongeza:
“Baada ya tatizo hili la kutoona zile kazi nilizokuwa nazifanya awali zilibadilika, nikawa mshauri naongea na wagonjwa wodini kuhusu mambo ya afya kwa ujumla, nikawa mshauri kwa wajawazito, wenye watoto lishe gani inafaa kwao lakini pia nilikuwa naongea na wanaume,” anasema.
Theopista anasema baada ya kupata tatizo hilo ndoto zake alihisi zimefifia kwa sababu hakuweza kufanya shughuli zote alizokuwa akizifanya awali.
Anasema hakuweza kuchoma sindano, kutoa dawa wala kuzalisha kinamama. Shughuli yake kuu ikawa ni kuelimisha wagonjwa mambo mbalimbali, kama vile kujikinga na maradhi na kwenye kliniki waliko wajawazito, wazazi na watoto.
Pia alikuwa anawaelimisha masuala ya usafi ili wawapo majumbani mwao wahakikishe yale mazalia yote ya mbu wanayatokomeza.
Anasema kwa kipindi chote akiwa kazini, hadi anastaafu Hospitali ya Rufaa Amana, kazi yake kubwa ilikuwa hiyo ya uelimishaji.
Theopista anasema maisha mapya ya kutoona, hayakumfanya achelewe katika eneo lake la kazi. Aliendelea kama kawaida kuamka saa 10.00 alfajiri na kila alipomaliza kufanya shughuli zake za nyumbani, alihudhuria kazini kwa wakati, kama ilivyo kwa watumishi wengine.
“Sikupenda kuchelewa, Kwa sababu nafahamu nilikuwa nahudumia watu wa aina gani, hivyo nilikuwa najitahidi kila siku kuwahi, ili nitimize lengo la mwajiri wangu,” anasema Theopista ambaye daima hisia zake bado zimezama katika uuguzi.
MAISHA YA KUSTAAFU
Theopista katika maisha yake ya kustaafu ambayo sasa imemchukua miaka mine, ni wazi kama mwwenyewe anavyokiri inakabiliwa na changamoto nyingi huku akiongozwa na kauli ya majuto kila anapoainisha ukweli unaomhusu .
Katika maisha yake ya sasa anaishi peke yake na katika historia yake, hakuwahi kuwa na ama mume au mtoto, tegemeo kuuu la kipato chake ni kiasi cha pensheni ya Sh. 200,000 kila mwezi anayopata kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii.
“Katika fedha hizo ninazopokea kodi kila mwezi ni Sh. 44,000, umeme Sh. 10,000 na maji Sh. 10,000. Inategemea na matumizi, kwa sababu hapa tupo wapangaji wengi,” anasema Theopista.
Anasema, shughuli nyingine ambazo anayofanya kwa sasa, ni uuzaji wa sabuni na ufugaji kuku na bata, ambao hawako wengi, kwa sababu anakoishi ni nyumba ya kupanga.
“Shughuli hizi zinafanywa na mpangaji mwenzangu Abela Gregory, ambaye amekuwa akinisaidia kutokana na hali yangu,” anatamka.
Theopista anasema kuwa mbali na ulemavu wa macho, pia anasumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu, vidonda vya tumbo na kisukari kilichompata katika siku za mwisho alipokuwa akimaliza mkataba wa ajira yake, miaka minne iliyopita.
Anasema kingine kinachomkimu ni biashara ya sabuni anayoeleza yupo katika ubia jirani yake Abela, anayezifunga kwenye mifuko midogo na kuuza mtaani.
Theopista anamsifu Abela kuwa ndiye anayemsimamia kwa karibu kumtunza na kuhakikisha anakula na kutumia dawa anazoandikiwa hospitalini.
Huduma zinginezo anazosaidiwa na Abela ni kumfulia nguo na shughuli zingine za usafi, huku Theopitsa akitamka:
“Ndoto niliyo nayo na uwezo wa kuitimiza ni kuwa na nyumba yangu ambayo ingenisaidia kufanya shughuli za ufugaji, ili ziniingizie kipato nisukume kurudumu la maisha yangu yaliyobaki duniani. Napenda Watanzania wenzangu wanisaidie kuitimiza.”
Theopista anasema jambo analojivunia ni kwamba, licha ya kustaafu, kila mara amekuwa akipokea simu kutoka kwa watu mbalimbali aliyowahi kuwahudumia, wakitaka msaada wake wac maelekezo.
“Elimu niliyotoa kwa makundi mbalimbali, imemfanya hadi leo kukumbukwa licha ya kustaafu. Wale niliowaelimisha, hunipigia simu na wengine huja hapa kutaka kujua wafanye nini, ili kuboresha afya za watoto wao au wao wenyewe. Najisikia faraja sana kwenye hili,” anasema Theopista.
Kutokana na hilo, anawaasa wauguzi wengine kuwa waadilifu na wavumilivu kazini na wakumbuke wakati wote kuwa, wanaowahudumia wagonjwa ambao ni wahitaji wa upendo.
Muda mwingi anapokuwa mapumzikoni, Theopista anautuimia katika kumcha Mungu na kama ilivyokuwa zama zilizopita, ni rafiki wa karibu wa watoto na hutumia muda mwingi kukaa nao karibu na kuwafunza.
Yeyote anayetaka kuwasiliana na Theopista Kamugisha, simu yake ni: (+255) 0718 57 77 34.









