Wanaposhinda wanatoka kifua mbele kwenda kuwashukuru wapigakura wao kwa kuwachagua na mara nyingi hapo ndipo wanaposimama na kuelezea mikakati yao ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Kinyume cha hapo wanasiasa hawa hukimbia na kuwaacha wapigakura wao bila ya kurudi na kutaka washirikiane kutatua kero mbalimbali na kuendelea mambo anayokuwa ameaayadi katika kampeni zake.
Huu ni utamaduni mbaya kwa sababu unaonyesha wazi kwamba huyu mwanasiasa shida ilikuwa ni kuchaguliwa na siyo kuwatumikia wananchi akiwa nje ya uongozi.
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyegombea ubunge katika jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, Innocent Melleck Shirima ni moja wa wanasiasa aliyevunja mwiko huo.
Shirima aligombea ubunge katika jimbo la Vunjo mwaka jana na kufanikiwa kupata kura 16,000, ingawa hakushinda na sasa amerudi na kuwashukuru wapiga kura wake na kutaka aanze kushirikiana nao.
Shirima anasema anayo dhamira ya kweli katika kulijenga jimbo hilo na kwamba yupo tayari kufanya hivyo akiwa nje ya ubunge..
Mwanasia huyo chipikizi anasema siasa siyo uadui na kwamba kikubwa kinachotakiwa ni dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi kama mwakilishi wao.
Anasema jimbo la Vunjo lina kero nyingi licha ya kuwa katika sehemu nzuri ya utalii na kilimo lakini bado wananchi wake wanakabiliwa na matatizo mengi.
Kwa mfano, anasema vijana wengi hawana ajira jambo ambalo linawafanya kuishia kunywa pombe na kushindwa kuzalisha mali na kwamba zao la Ndizi ni raslimali muhimu ambayo ikitumiwa vizuri ianweza kubadilisha maisha ya wananchi wa Vunjo.
Shirima anasema lengo lake la kugombea ubunge lilikuwa ni kutaka kushirikiana na wapiga kura wake kuinua uchumi pamoja na kuondoa kero mbalimbali ikiwamo kusimamia mapato yatokanyo na mlima Kilimanjaro.
Hata hivyo, kada huyo wa CCM ambaye ni Naibu Kamanda wa Umoja wa Vijana wa chama hicho UVCCM wilaya ya Moshi vijijini, anasema ingawa hakubahatika kushinda katika uchaguzi wa mwaka jana, lakini hilo haliwezi kumkatisha tamaa ya kushirikiana na wapigakura wake ambao ni ndugu zake.
Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalum, Shirima anasema, jimbo la Vunjo lina matatizo mengi yakiwamo ya kukosa mapato ya mlima Kilimanjaro, tatizo la ajira kwa vijana, ukosefu wa mitaji kwa wanawake pamoja na kuboresha sekta ya afya, elimu na mkundombinu.
Anasema hayo anayajua na kwamba atahakikisha anashirikiana na wananchi ili kuona namna bora ya kutatua kero za wananchi wa Vunjo.
Shirima ambaye aligombea ubunge kwa mara ya kwanza mwaka jana, anasema wananchi hususani wanachama wa CCM jimbo la Vunjo walimuamini na kumpitisha katika kura za maoni.
Anasema kitendo hicho pekee kinatosha kumfanya ajione kama analo deni la kuwalipa wapigakura 16,000 pamoja na wanachama wa CCM waliomchagua
Ahadi zingine alizokuwa amehidi kama kwa wapigakura ilikuwa na kuhakikisha kunapatikana soko la kimataifa eneo la Himo amnbalo litawanufaisha wananchi wote.
Anasema mawazo aliyokuwa nayo awali bado yapo ingawa kura hazikutosha kumfanya awe Mbunge wa Vunjo ingawa bado anajiona analo deni kubwa.
Anasema alichaguliwa na wananchi wengi ambao pia anaamini hawakuwa wana CCM bali kutoka vyama vingine vya upinzani.
Licha ya kuwa hakushinda mwaka jana, Shirima anasema anajiandaa kwa ajili ya kipindi kijacho.
"Mwaka 2020 siyo mbali nitaendelea kufanya kazi kwa karibu na wapiga kura wangu ili kuona namna gani naweza kutekeleza yale niliyokuwa nimepanga kuyafanya kama ningekuwa Mbunge wa Vunjo," anasema
Kada huyo wa CCM ambaye ni kijana alikishukuru chama chake wilaya ya Moshi vijijini pamoja na Kamati Kuu ya chama hicho chini ya uenyekiti wake, Jakaya Kikwete kwa kumuani na kupitisha jina lake bila mizengwe.
"Unajua kitendo cha CCM kukuamini upeperushe bendera yao katika nafasi ya ubunge siyo jambo dogo, hilo peke yake linatosha kunipa moyo kwamba bado ninayo nafasi uchaguzi mkuu ujao 2020," anasema Shirima
Aidha, anawashukuru wanachama wa CCM ngazi ya shina, tawi na kata kwa kuwa walifanya jitihada mbalimbali katika jimbo la Vunjo.
Katika uchaguzi huo, Shirima alipambana na James Mbatia kutoka Chama cha NCCR-Mageuzi, aliyekuwa anaungwa mkono na Ukawa na Augustino Mrema (TLP).
Mbatia ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa jimbo hilo mwaka 1995 kupitia NCCR-Mageuzi aliibuka mshindi kwa mara ya pili katika uchaguzi wa mwaka jana.










