Umiliki wa silaha za moto na ugeni wa matumizi yake hapa nchini

30Mar 2016
Hekima Akilimali
Nipashe
Umiliki wa silaha za moto na ugeni wa matumizi yake hapa nchini

KAMA miongo miwili na nusu iliyopita, Bunge la Tanzania lilipitisha sheria iliyoruhusu umiliki wa silaha za moto.
Huu ndio ulikuwa mwanzo wa kukaribisha (labda kuhalalisha ni sahihi zaidi) kampuni binafsi za ulinzi nchini.

Rais Magufuli (kushoto) akikabidhiwa silaha yake baada ya kukaguliwa na ofisa wa jeshi la Polisi.

Kadhalika ilikuwa ndio mwanzo wa kuendeleza utalii wa uwindaji katika viwango tunavyovishuhudia sasa.
Suala la kuhalalisha soko la silaha lilifanywa ni jambo lisiloepukika kwa wakati huo.

Tanzania ikiishi na tishio halisi lililotokana na ‘soko holela’ la silaha ambalo lilileta chagizo katika nchi za jirani za Burindi, Rwanda, Kongo, Uganda na hata Kenya.

Hivyo kupitisha sheria hiyo ilikuwa ni mwendelezo wa kuingizwa silaha za moto nchini ambazo hutumika kufanya uporaji na ujambazi.

Kama leo Tanzania tunashuhudia ujambazi mithili ya uliokuwa ukiwatesa majirani zetu Kenya miaka ya 80 si bahati mbaya bali tuliruhusu hili tena kwa sheria.

Leo rais ana silaha (ingawa analindwa) mawaziri wanatembea na silaha na kuna taasisi lukuki za ulinzi zinamiliki silaha.
Lengo la serikali kuruhusu watu binafsi kumiliki lilikuwa zuri na huenda lililenga kuwapa uwezo wa kujilinda wenyewe na siyo matumizi zaidi ya hayo.

Raia hana budi kuhoji kama kweli Tanzania ni nchi ya amani kulikoni Rais anayelindwa kubeba silaha ya moto?
Miaka ya 70 Tanzania Bara ilipitia kipindi kigumu kiuchimi kutokana na kupanda kwa bei za mafuta na baadaye kutokana na Vita dhidi ya Iddi Amin.

Hali hii ilichangia kuwapo uhaba wa bidhaa muhimu kila siku, hivyo kukaanza biashara za magendo ambazo ziliwawezesha wananchi kupata vitu vya msingi kama vile dawa za meno, sabuni na hata mafuta ya kupikia na ya manukato.

Kutokana na siasa za wakati huo watu hawa wakaitwa ‘wahujumu uchumi’ ila tofauti na sasa wahujumu uchumi waliokuwa wakianikwa enzi hizo walikuwa si ‘mapapa na manyangumi’ bali wengi walikuwa walanguzi wa kubabaisha, hasa maeneo ya mipakani.

Lakini katika kamatakamata hiyo kukazuka tabia ya kukamata walioshukiwa kuwa wapinzani dhidi ya serikali na chama tawala.

Mara nyingi ikitosha kuwashutumu kuwa ni wahujumu uchumi kuwamaliza kisiasa na kimaisha. Mifano imejaa tele ingawa hatupendi kuwatambua.

Hali ya kiuchumi na kimaisha ilizidi kuwa mbaya na Tanzania ikabidi iweke siasa zake upande na kukubali sera za uchumi huria.

Baada ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi maarufu ‘Mzee rukusa’ kushika hatamu ya nchi na sera zake kuashiria kuwa uchumi wa nchi utafunguka basi wananchi walifanya kila jitihada ya ‘kujiendeleza’ iwe kwa jitihada zao wenyewe au kwa kununua nafasi za ‘ufaulu’.

Biashara ya kununua vyeti vya elimu ikashamiri na taathira zake tunaziona mpaka leo.
Utakuta mtu, wakiwamo baadhi ya wabunge na watumishi wakubwa serikalini ana jina la dhehebu au kabila lingine hata hafanani nalo.

Mara nyingi watu wakitafuta vyeti vya ufaulu wa ‘O’ Level au ‘A’ Level ili apate kazi ili baadaye aendelee na masomo ya juu.

Leo mtindo huu wa kununua majina ya watu sasa umegeuka na kuchukua taswira mpya.
Bomu la mwisho liliripuka bungeni na vyombo vya habari vilianika aibu ya wajumbe wanaotuhumiwa kuwa na vyeti vya elimu ya juu vya kugushi.

Wakati wengine walinunua vyeti, baadhi yao waliongopa tu juu ya sifa zao.

Alimradi suala zima la kugushi vyeti vya elimu na sifa za kazi ikazoeleka na baada watu kufanikiwa basi nao wakawa wanawafanyia ndugu zao nao wapate riziki zao na kupunguza mzigo wa utegemezi hata kama wanafanikisha hilo kwa mizengwe.

Likaja suala la kuingilia na hatimaye kudhulumu mali za watu. Leo, Tanzania inakabiliwa na migorgoro ya ardhi lukuki.
Kila kukicha taarifa za habari zinabeba habari kuhusiana na migogoro ya wananchi na ardhi.

Tafiti zilizofanywa na taasisi kama za Haki Ardhi na Kitivo cha Sheria zilibaini kuwa migogoro mengi ilihusu watu kuvamia maeneo ya wengine na kujipatia hati miliki kwa njia za udanganyifu.

Hii ilileta tatizo la ugawaji mara mbili (yaani double allocation). Kadri utendawizi ulivyoenea baada ya Tanzania kuregeza mfumo wake wa uchumi basi wananchi wakazidi kuporwa na maeneo yao ya makazi.

Ardhi hiyo ilichukuliwa kisheria na kupewa wawekezaji wa ndani na wa nje ya nchi ingawa sasa inabainika kwamba waliopewa si wawekezaji bali walitaka kuiweka tu ardhi na kuifanyia biashara kinyume kabisa na itikadi ya ujamaa iliyokataza uhodhi wa rasilimali.

Linalosikitisha ni kuwa hata watumishi wa umma wakiwemo wale waliokuwa na nyadhifa za juu wakawa wanajichukulia maeneo makubwa na baadaye kujimilikisha kisheria wakati wananchi wa kawaida hata wakijaribu kusajili mali zao basi mfumo unawawekea pingamizi kufanikisha haja yao ya kulinda ‘chao’.

Ndio maana leo wananchi wakathubutu kavamia ‘eneo’ la Waziri Mkuu mstaafu eneo alilojipatia wakati yuko katika utumishi kwa madai kuwa si mkaazi wa hapo na halitumii.

Mhe. Sumaye si kiongozi pekee ambaye atashutumiwa na wananchi kwa kuhodhi ardhi ikiwemo ya umma au binafsi.
Zanzibar, wakati wa utawala wa Amani Karume kulizuka usemi wa “hapa pangu!” kukejeli tabia ya jamaa zke kuhodhi ardhi na majumba kwa kudai kuwa ni mali ya familia yao.

Pia tusisahau mgogoro uliovuma mwishoni mwa utawala wake kuhusu ugawaji wa eneo la wazi katika ufukwe wa Mji Mkongwe ambapo leo ipo sehemu ya Park Hyatt.

Wapo marais kadhaa ambao wameshutumiwa kwa kutoa maeneo ya wazi kama viwanja vya mpira wa kikapu pale Gymkhana, iliyokua sinema ya Drive Inn au maeneo yaliyopo Koko Beach kwa wawekezaji bila ya kujali kuwa ni maeneo ya wazi au kuwa ni maeneo yaliyozoeleka kwa matumizi ya umma.

Huko Zanzibar kwa mfano ambapo moja ya matukio makuu ya Mapinduzi ni ni kutwaa ardhi kutoka mikono ya wachache na kuwagawia wananchi imekuwa na matokeo tofauti.

Ayoub Mohamed Mahmoud ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Ardhi, Makazi na Madini katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar amebaini uovu unaondelea kuhusu matumizi ya eka.

Kwa sasa Ayoub ni Mkuu wa wa Wilaya Maghribi B na katika ziara zake wilayani karibuni alibaini kuwa ardhi nyingi za heka zimegawiwa viwanja kinyume na sheria. Viongozi na watumishi wengine wamediriki kugawa au kujigawia ardhi ambazo si zao.

Ni dhahiri kuwa maadili mema husambaratika pale tunaporuhusu ukiukwaji, hasa ukiukwaji huo ukiwa kinyume kabisa na maadili ya msingi. Kila kashfa iliyowahi kuanikwa ilianza na kiongozi (na hata mwananchi) kuregeza msimamo kidogo na hatimaye tabia ikazoeleka.

Waswahili wanasema usipoziba ukuta utajenga ufa. Aidha wana usemi unaosema ‘rahisi, ghali’. Kama mwenendo wetu utakuwa kuruhusu mambo kwa kukidhi haja za muda, tena muda mfupi bila ya kuzingatia taathira ya muda mrefu basi tukubali kuwa kamwe hatutojenga bali tutadumisha bomoa boma katika msingi wa utaifa na uhai wetu.

Aidha kama utaendelea na tabia za ‘funika kombe wanaharamu apite’ tutambue kuwa tutaikosa hapa duniani na kuitengeneza akhera yetu na ya vizazi vyetu.