Dk.Shein na mtihani wa kuunda serikali itakayotuliza hasira Wazanzibar

30Mar 2016
Hekima Akilimali
Nipashe
Dk.Shein na mtihani wa kuunda serikali itakayotuliza hasira Wazanzibar

LEO nataka kutumia wasaa huu wa sikukuu adhimu ya Pasaka kujaribu kushawishi mustakabali wa mambo Zanzibar kuhusu mabadiliko baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 20 Machi 2016.

Rais Ali Mohamed Shein akinyanyua cheti cha ushindi alichokabidhiwa na ZEC.

Nimezungumza na watu wengi ambao wanajipambanua kuwa ni Wazanzibari. Watu hawa wanasikitishwa kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) kimewafikisha pahala ambapo siasa za Zanzibar ni sawa na ushabiki wa vyama vya mpira au hata vya beni vya enzi.

Utaifa ama utambulisho wa Uzanzibari umefifia, umewekwa pembeni.

Wazanzibari hawa wanakerwa na hali wanayoishuhudia nchini mwao.

Wakizungumza kwa hamasa kubwa waliibua masuala kadha wa kadha waliyotaka Rais wa Zanzibar ayatambue wakati anaunda serikali yake.

Katika makala haya leo nitawapa nafasi kwa kile wanachotaka kihabarishe uteuzi wa serekali itakayodumu Zanzibar mpaka 2020.

Mchangiaji wa kwanza kaomba afafanuliwe nani ndiye Rais wa Zanzibar? Nilipotaka ajieleze zaidi akajimwaga na kusema, “Tukijikumbusha yaliyojiri wakati wa mkwamo wa siasa tangu kufutwa uchaguzi Oktoba 2015, Rais wetu hatukuwa tunamuona sana wala kumsikia.

Badala yake tunasikia manaibu wa UVCCM na makada wengine ndio wasemaji wakuu wa serikali ingawa serikali ni ya Wazanzibari wote na chama kinabaki na masuala yake ya chama.

Labda kwa vile sasa imekuwa serikali ya chama kimoja mipaka baina serikali na chama itazidi kuwa eneo lenye giza.
Wananchi wanataka uwazi juu ya serikali inayongozwa na nani na nani ndiye msemaji wake mkuu?

Mtu mwingine aliyechangia alitaka wizara zibadilishwe ili zikidhi mwelekeo uliopo katika kuunda serikali.

Alisisitiza, “Kuna sura tunaziona serikalini na katika Baraza la Wawakilishi miaka nenda miaka rudi. Hivyo, tuundiwe wizara ya wenye nchi, ya wano nafasi maalumu na ya viongozi wastahili!”.

Kwa mujibu wa mchangiaji huyu hakuna haja ya kuwa na waziri wasio na wizara maalumu kwa kipindi kizima cha miaka mitano wakati kuteuliwa kwake tayari kunaashiria kuwa anayo nafasi maalumu na ndio maana hajaachwa.

Mchangiaji wa tatu yeye ombi lake halijaenda mbali. Naye kataka wizara zinazoakisi siasa za Zanzibar kwa sasa badala ya kuunda wizara kwa mazoea.

Alidokeza, “Wajifunze kwa Magufuli ambaye hajaona tabu kuunda Wizara ndefu zilizorundika mambo aliyoyaona yanastahili kushughulikiwa mutawaliwa.

Hivyo hapa Zanzibar kuwe na wizara ambazo zitasimamia mambo ambayo watawala wetu wanayaona ni muhimu,”
Nikataka kujua ni wizara kama ipi aliyokuwa anaifikiria?

Mchangiaji wa Tatu alijibu, “Tusipoteze muda kuunda wizara ambazo si vipaumbele vya serikali na wapambe wake.
Wale wazungumzaji wakanikodolea macho kwa kunishangaa na kusema kwa pamoja, “Lini kumekuwa na utawala wa sheria au katiba?”

Nilipoonyesha kutoelewa kauli yao akaendelea mchangiaji wa nne, “Labda kwenye karatasi lakini kiuhalisia kila anayewekwa kinarani basi anaendesha mambo anavyoona yeye.

Kungekuwa na utawala wa sheria hapa kwetu basi tusingevurugana kiasi hiki hata hatujielewi tunakwenda wapi au tunataraji nini
Kuna kijana mmoja wa kike naye akaongeza lake. Akaanza kwa kuwatahadharisha wenzake, “Jamani, tusikome katika wizara tu lakini hata katika mamlaka mbalimbali zilizopo nako kufanywe marekebisho tena ya msingi” alianza na nikapata tumaini kuwa labda sasa tutaanza kuelwana juu ya muundo timamu wa serkali.

Hakika hiki kikosi cha wachangiaji kilinitoa jasho maana sijategemea kabisa maoni yao na wakati ninayatafakari mwingine akarukia, “Hakika tunahitaji mamlaka si ya mambo ya kale lakini ya mambo yaleyale maana ndo hatuoni mabadiliko, si katika kauli si katika matendo ingawa tunajivunia kuwa sasa tumejitawala”

Mzungumzaji wa kwanza alitoa ishara ya kukubaliana na kauli hiyo kwa kichwa akaongeza, “leo urithi wa Zanzibar unaporomoka!

Hata hiyo nyumba ya ajabu inamegeka-megeka na kuporomoka leo paa, kesho kuta ili hali ndo sehemu ya urithi wa mambo ya kale ambao unaiweka Zanzibar katika ramani ya dunia.

Hili haliwashughulishi wasimamiaji mambo ambao wanatumia vitega uchumi vya Mji Mkongwe na urithi mwingine kujineemesha. Hivyo, tutambue tunahitaji kuhimiza mambo yale yale na wala si mambo mapya au yale ya kale!”
Mshiriki mmoja alikuwa kakaa kimya muda mrefu alitabasamu akaanza kujinesanesa nikahisi naye anataka kuchangia. Nikamgeukia na kumuuliza “Naam, una la kuongeza?”

Akacheka na kujibu kwa tafakuru nzito, “Hata sijui niongeze nini maana mtu hupata tumaini kile anachokisema basi alau kiwe kinatiliwa maanani. Lakini kwa utamaduni uliotawala na kuzoeleka hapa ni sawa na bure.
Fikra chanya hazitakiwi. Watu wanaofikiri na kuhoji hawatakiwi.

Uhuru si kupiga kura tu. Uhuru ni kuwa na chaguo na imani kuwa chaguo lako litaheshimiwa na kuzingatiwa kwa usawa na uzito unaostahili.

Hii ni tofauti na kuwasemea watu au kuwaburuza halafu ukatumia kauli za ‘Mapinduzi Daima’ kudhibiti wakosoaji ili hali Katiba inatambua kuwepo uhuru wa kujieleza.

Bora tujijue tu tuko hivi badala ya kujipakaza sifa ambazo hatuziamini si kwa fikra, kauli wala vitendo.

Awamu hii unafiki uwe basi. Tujipambanue namna tulivyo watu wote waelewe na waridhike kuwa hivi ndivyo tulivyo.
Hata hivyo, ningependa kuwakumbusha walio ihodhi nchi kuwa Zanzibar si ya CCM au ya CUF bali ni ya wazanzibari wote, wenye vyama na wasio na vyama.

Kuwashurutisha kujiunga na mitizamo finyu na yasiyo na tija ya kichama ni uhaini wa aina yake”, mchangiaji akamalizia.