Aina ya migogoro inayopatikana sehemu hizo, hutegemea mazingira yake, ingawaje zina sura zinazofanana sana. Ni jambo linaloisumbua sana serikali, ushuhuda halisi ni kinachoendelea sasa wilayani Mvomero.
Wakati akiapisha safu mpya ya wakuu wapya wa mikoa hivi karibuni, Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Dk. John Magufuli alieleza sababu za kumuacha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, kwamba ilitokana na kushindwa kudhibiti migogoro hiyo.
Mbali na hali iliyoko Morogoro, wilayani Misenyi katika mkoa wa Kagera, nako kuna vituko vyake. Kumetawaliwa na migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji, ambao kwa asilimia kubwa wanatoka katika nchi jirani.
HALI ILIVYO
Kwa mujibu ripoti ya mkoa, picha halisi ya migogoro ya ardhi inayojitokeza Misenyi, ni wafugaji na wakulima wakigombea maeneo ya kulima; Wafugaji wanagombea ardhi ya kulisha mifugo na wakulima wakililia ardhi ya kilimo.
Kuna sura ya pili kwamba, kuna migogoro ya ardhi inayotokana na ubinafsishaji wa rasilimali za umma na uwekezaji, inayoendana na hitaji la ardhi kwa wawekezaji husika.
Sababu zinazotolewa na wananchi kuhusu kuibuka migogoro hiyo, inajumisha serikali kushindwa kupima na kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji na jamii, huku ubinafsishaji unaofanywa kutokuwa shirikishi.
Pia, kuna athari nyingine ya mgogoro wa ardhi unaotawaliwa na njaa na umaskini. Ni hali inayochangiwa na mazingira kama vile uzalishaji duni wa mazao, uharibifu wa mali, ulemavu wa kudumu na vifo vinavyosababisha kupotea nguvu kazi.
Mkoa wa Kagera unaopakana na nchi nyingi, migogoro yake ya ardhi ina asili ya nchi nyingine, kwa maana raia kutoka nchi jirani huingia na kusababisha kuibuka msuguano na wazawa wa eneo husika.
Mwaka jana, Idara ya Uhamiaji iliwakamata na kuwachukulia hatua mbalimbali, ikiwamo kuwarejesha makwao wahamiaji haramu 794. Hata hivyo, wananchi wanaendelea kulalamika kuwa waliokamatwa ni wachache, ikilinganishwa na hali halisi.
Watendaji wa serikali waliopewa dhamana ya kuwadhibiti wahamiaji haramu na vyombo vyao, wanatajwa na wananchi kwamba utendaji wao si wa kuridhisha, huku lawama zikiwaangukia baadhi ya wananchi wanaowahifadhi wageni katika makazi yao.
Pia kuna wenyeviti wa vitongoji na vijiji wanaodaiwa kutumia madaraka yao kuruhusu wahamiaji haramu kuingia mkoani humo, wakati wakitambua hawana mamlaka ya kufanya hivyo.
ZIARA YA MAJALIWA
Machi 13 mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alizuru mkoani Kagera na katika kauli zake alielekeza kauli zake kwa viongozi wenye dhamana ya kulinda amani nchini.
Dai lake lilikuwa kwamba, wao ndiyo wanaosababisha kuwapo migogoro ya ardhi yenye mzizi kutoa kwa wahamiaji haramu.
Majaliwa aliishutumu Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa na hususan Idara ya Uhamiaji, kwa kushindwa kuwadhibiti raia wa nje wanaoingia kiholela bila ya kufuata taratibu za nchi, akisema umakini wao ni mdogo.
Anawataka Maofisa Uhamiaji kuanzia ngazi za wilaya hadi mkoa wabadilike, kwani wamesahau kuwalinda wananchi wanaowategemea na badala yake ni wepesi wa kutoa vibali kwa raia wa kigeni kutoka nchi zinazopakana na mkoa.
Waziri Mkuu anatahadharisha kuwa Tanzania ina wananchi takriban milioni 45, hivyo kuruhusu watu kuingia nchini kiholela ni hatari na umakini ukikosekana Kagera, udhaifu utavuka kwingineko nchini na kuzua balaa la namna mbalimbali.
Anaungana na malaamiko yaliyopo kuwa, mkoa wa Kagera una wahamiaji haramu wengi na anataja sehemu kubwa ya udhaifu unajionyesha katika wilaya za Missenyi, Kyerwa na Ngara, huku Biharamulo na Karagwe zikiwa na kiwango kidogo.
Anasema hata idadi kubwa ya mifugo inayoletwa mkoani Kagera haiwanufaishi wazawa baada ya kunenepeshwa kwa rasilimali za Tanzania, kwani wanarejeshwa walikotoka.
Majaliwa anasema kuwa Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa wingi wa mifugo mingi, ikitanguliwa na Ethiopia, lakini haijamudu kuuza nje nyama na mazao mengine ya mifugo.
Anasema sababu kuu ya kushindwa kusafurisha nje nyama, kwamba nyama husika haina ubora na kuwa kinachotakiwa sasa ni kufuga kisasa ili wananchi wapate tija.
RANCHI YA MISENYI
Miongoni mwa maeneo aliyoyatembelea waziri mkuu huyo, ni Ranchi ya Taifa ya Missenyi. Takriban miaka 14 imekuwa katika mgogoro wa ardhi na wananchi wa Kata Kakunyu, uliotokana na baadhi ya maeneo ya ranchi kutengewa vitalu vidogo na kubinafsishwa, kwa lengo la kufanya ufugaji wa kibiashara.
Vitalu vinavyolalamikiwa na wananchi kuchukua maeneo yao ya vijiji anayataja kuwa: Namba Moja, Tatu, Sita, Saba, 10 na 11.
VIONGOZI WA KIJIJI NA KILIO WAKAZI
Kutokana na kuwepo mgogoro wa muda mrefu, wananchi wa vijiji vya Kakunyu, Bubale, Bugango na Bwenkoma waliunda kamati ya kutafuta suluhu, chini ya Mwenyekiti Abdallah Hassan.
Mwenyekiti huyo anawalekezea kidole watendaji wa serikali kuwa ndio chanzo cha mgogoro, kwani wanashindwa kuheshimu haki za binadamu kwa kuwaondoa wenyeji kwa nguvu, licha kuwepo hapo kwa miaka 60 sasa.
Anasema badala ya vitalu hivyo kutumiwa na wawekezaji waliobinafsishwa na serikali, vinakodishwa kwa wafugaji wa kigeni, hatua inayosababisha wananchi kunyanyaswa.
“Hivi vitalu vingekuwa vinatumiwa na Watanzania, tungekuwa tayari tumeelewana na mgogoro ungekuwa umekwisha. Tatizo ni vitalu vinatumiwa…wanatudharau kwa sababu wamekwishaongea na wakubwa,” anasema.
Hassan analalamika namna mgogoro ulivyorudisha nyuma maendeleo yao kwa kuzuia kuendesha shughuli za kilimo na mifugo, ambayo imekuwa ikikamatwa mara kwa mara na kutozwa faini.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bugango, chenye wakazi 3,600, Sprian Tindika anasema ugawaji wa vitalu hivyo ulivuka mipaka ya ranchi na kuingia vijijini.
“Ranchi irudi katika mipaka yake ya mwaka 1963, migogoro itakwisha. Mfano katika kijiji Change wameweka Jeshi - Suma JKT (Kikosi cha Uzalishaji cha Jeshi la Kujenga Taifa) wakati kuna wakazi 567. Serikali inasema hakuna wananchi, eti waliomo waondoke wamevamia,” analalamika Tindika.
Anasema wakati wananchi wako tayari kulinda mipaka ya nchi kuwadhibiti wahamiaji na mifugo yao, nao wanaomba hatua ichukuliwe kuihamisha Suma JKT iwe jirani na mpaka, ili kuimarisha ulinzi wake.
Kwa mujibu wa Tindika, wageni wanaoshi na mifugo mingi katika kata ya Kakunyu wanalazimika kutafuta malisho kwa gharama yoyote ile, hali inayojenga mazingira ya kutokea uhasama na migogoro ya ardhi ndani ya jamii.
Ernest Rwamashonga ni Mwenyekiti Kijiji cha Bubale, chenye wakazi 8,891 na ng’ombe 15,991. Anaomba wawekezaji wanyang’anywe vitalu vya ardhi walivyopewa, akiamini wakazi wa kata hiyo wana uwezo wa kusimamia miradi yao ya mifugo kisasa na kibiashara.
Rwamashonga anasema mbali na migogoro anayodai inawarudisha nyuma kimaendelea, pia imesababisha wananchi kujeruhiwa kwa mapanga na risasi. Miongoni mwa waliodhurika ni yeye mwenye ambaye ana ulemavu wa kudumu.
Kijana Slivester John (35), mkazi wa kijiji hicho ni miongoni mwa walioacha kumbukumbu mbaya kutokana na mgogoro huo, baada ya kuuawa na watu wasiojulikana, huku lawama za mauaji hayo zikiwaegemea walinzi wa wawekezaji katika vitalu hivyo.
Kijiji cha Kakunyu kilichoko mpakani na Uganda, kina wakazi 7,579 na mifugo 5,432. Mwenyekiti wa kijiji hicho, Grace Byabato, alitajwa na Waziri Mkuu Majaliwa kuwa miongoni mwa waliotajwa katika mkutano wa hadhara, kwa madai ya kutoa vibali kwa raia wa nje kuingia na mifugo yao.
Grace anajitetea kwamba hajawahi kuingiza wahamiaji haramu nchini, huku akidai wageni wakiishi kijijini hapo tayari wanakuwa na vyeti vya uraia.
Anafafanua:“Nilikwenda katika kijiji hicho mwaka 1993 nikiwa Mtendaji wa Kijiji mwaka 2000, nilistaafu wadhifa huo na kugombea nafasi ya uenyekiti tangu mwaka 2003 hadi sasa mimi ni mwenyekiti.”
Anasema inawezekana lengo la serikali kutenga na kubinafsisha vitalu hivyo halikuwa baya, lakini kilicholitia dosari ni vitalu vingi kudaiwa kuchukuliwa na raia wa nje na hasa kutoka Rwanda na Uganda, kupitia migongo ya Watanzania.
Kelele hizo kwa waziri mkuu zilifik mbali, baada ya kuonekana ni mtandao mpana kwa viongozi wengi wa serikali katika ngazi mbalimbali kuwa wanufaika wake, hivyo kuwadhibiti wageni hao walikuwa wanufaika wa miradi hiyo.
MBUNGE KAMALA
Balozi Dk. Diodorus Kamala, ni mbunge wa jimbo la Nkenge, anaeleza uzoefu wake wa ubunge kwa zaidi ya miaka 10, akihoji sababu ya kuendelea migogoro hiyo, wakati hatua zilishachukuliwa.
Mbunge huyo anaeleza kushangaza namna viongozi wa mkoani Kagera kushindwa kutatua migogoro hiyo, huku kuna maagizo mazitio yalishatolewa ya kumaliza migogoro hiyo, akiwamo Rais aliyetangulia, Jakaya Kikwete.
MOTO WAWAKA
Siku chache baada ya waziri mkuu kukamilisha ziara yake mkoani Kagera, baadhi ya viongozi akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Festo Kiswaga, walikunjua makucha yao kwa kuwasimamisha kazi watumishi watano wilayani washikiliwe, hadi uchunguzi utakapokamilika.
Katika orodha hiyo, watumishi wawili ni wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi; Ofisa Mifugo wa Kata ya Kakunyu na Ofisa Mifugo wa Wilaya, Erick Kagolo.
Pia kuna watumishi watatu wa Ranchi ya Taifa ya Missenyi ambao; Meneja wa Ranchi - Martine Ladslaus na wasaidizi wake, Kedimund Magule na Nickson Kashalankoro.
Sababu ya kusimamishwa na kuwakabidhi kwa Polisi kwa ajili ya kuchunguzwa ni kwamba wamekuwa wapatia fedha kwa njia zisizo halali za kuingiza mifugo nchini na kulisha katika ardhi ya Tanzania.
Kiswaga anasema watumishi hao tangu Desemba mwaka jana hadi mwanzoni mwa mwezi huu, wanadaiwa kuchukua zaidi ya Sh. milioni 17 kutoka kwa wafugaji kwa ajili ya kujinufaisha.
Wakati akifanya majumuisho ya ziara yake wilayani Ngara, alitangaza kufuta vitalu saba katika Ranchi ya Missenyi, ikiwa moja ya hatua za kumaliza mgogoro huo.
Pia alisistiza kuwa mchakato wa kuwamilikisha wafugaji utafanyika upya, lakini wazawa ndiyo watakaopewa kipaumbele.










