Umaskini wabadili itikadi za maisha yao, wazazi wao

22Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Umaskini wabadili itikadi za maisha yao, wazazi wao

HALI ni mbaya kutokana na mkanganyiko wa vita na umaskini nchini hapa, mabinti wadogo wanabakwa pia wao wenyewe wako mstari wa mbele ama kujiuza au kuuzwa na wazazi wao.

Jambo baya zaidi katika hilo ni kwamba kwa wale wanaojiuza, baadhi bei yao ni ama mkate mmoja au walau wenye bei ya juu ni sawa na fedha za Kitanzania Sh. 3,000.

Kwa kifupi, umaskini unawaingiza katika maisha wasiyoyapenda, wasiyotarajia na hata mazingira ambayo wazazi wao wangeota wala kupenda kuyasikia.

Ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Kimataifa linalohusika na kutetea Haki za Binadamu (Human Rights Watch), limesema licha ya kuwapo ubakaji, kuna wasichana wanaojihusisha wenyewe na biashara ya ngono ili kujikimu kimaisha.

Taarifa hiyo imesema, baadhi ya wasichana wanaoishi katika kambi ya watu waliopoteza makazi yao katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, wanakubali kujihusisha katika biashara ya ngono ili kujikimu kimaisha.

Wamelambia Human Rights Watch kwamba wanajeshi wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo (Minusca), wanawadhulumu kimapenzi.

Wakati akitafuta chakula au fedha kidogo katika kambi ya Minusca, msichana mmoja mwenye umri wa miaka 18 alidai kubakwa na wanaume watatu.

"Walinichukua kichakani, walikuwa na silaha wakasema wataniua iwapo nitakataa," alisema msichana huyo alipozungumza na Human Rights Watch.

Mkusanyiko wa wanajeshi, vita na umasikini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati umesababisha hali ya kutisha na kuwapo vituko vya udhalilishaji wa kingono.

Tangu kuanza kwa operesheni ya wanajeshi wa kulinda amani nchini humo Septemba mwaka wa 2014, matukio 42 vya udhalilishaji wa kingono yameripotiwa huku wachunguzi kutoka Ufaransa wakifuatilia madai ya ubakaji dhidi ya wanajeshi waliopelekwa katika koloni lake la zamani.

Aidha, mwaka jana theluthi tatu ya kesi zilizoripotiwa miongoni mwa vikosi takriban 16 vya kulinda amani vya Umoja wa mataifa duniani viliwahusisha wanajeshi wa Minusca.

Mjumbe wa Umoja huo mjini Bangui, Onanga-Anyanga, amesema madai hayo ni ya kusikitisha na yasivyokubalika.
Tukio la hivi karibuni lilitokea Februari lililowahusisha watoto wanne katika kambi ya watu waliopoteza makazi waliodaiwa kudhulumiwa na wanajeshi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Licha ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, kumfuta kazi Mkuu wa Kikosi cha Wanajeshi 10,000 cha Minusca Agosti, mwaka jana baada ya kuwapo matukio mengi ya udhalilishaji wa wasichana.

Wanajeshi wanaohusishwa na udhalilishaji huo, wengi wanatokea katika nchi za Congo, Morocco, Niger, Bangladesh na Senegal.

Katika kila tukio lililotokea katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, inadaiwa lilitokea katika kambi ya watu waliopoteza makazi karibu na kambi ya Minusca.

Kambi moja ya wakimbizi ya M'poko iliyoko karibu na mji wa Bangui, imegeuka kuwa makazi duni iliyojaa wakimbizi na umasikini, huku wasichana wadogo wakikubali kuwa na mahusiano ya kingono na wanaume wakiwemo wanajeshi wa kulinda amani ili weweze kupata chakula kama mkate au fedha ambayo ni chini ya euro moja.

"Wanawake wana miili yao tu ya kuuza ili kulisha familia zao iwapo itakuwa waume zao waliuwawa au kupotea," alisema Irene Ngogui, anayefanya kazi katika shirika moja lisilokuwa la kiserikali.

Irene anasema wakati mwingine wazazi wenyewe ndio wanageuka kuwa wakala wa kuuza mabinti zao.