Mbunge Kuchauka: Kipaumbele cha kwanza Liwale ni afya

23Mar 2016
Abdul Mitumba
Liwale
Nipashe
Mbunge Kuchauka: Kipaumbele cha kwanza Liwale ni afya

MIEZI minne iliyopita, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vilikuwa vikijipambanua kwa kauli mbili iliyopata ushindi mkubwa ya elimu kwanza kama kipaumbele cha kwanza hadi cha tatu.

Kauli mbiu hiyo ilisikika zaidi wakati wa kampeni na iliibuliwa na aliyekuwa mgombea urais wa umoja huo, Edward Lowassa, alisema kuwa endapo Ukawa ingeingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, nchi ingekwenda na falsafa ya ‘Elimu Kwanza’ na mambo mengine yangefuata baadaye.

Maana yake ni kwamba, kwa wabunge na madiwani walioshinda kupitia Ukawa, inatarajiwa wataongoza maeneo yao kwa kutumia kauli mbiu hiyo jambo ambalo ni tarajiwa la walio wengi.

Kaulimbiu hiyo ilipokelewa vizuri na waliokuwa wagombea wa nafasi mbalimbali za udiwani na ubunge kupitia Ukawa, iliyokuwa ikiundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) NLD na NCCR-Mageuzi.

Hata wakati Lowassa na timu yake walipofika katika jimbo la Liwale lililopo mkoani Lindi kwa kampeni, kaulimbiu ya Elimu Kwanza ndiyo iliyoshika kasi na miongoni mwa walioipokea na kuipigia debe kikamilifu, ni mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Zuberi Kuchauka.

Kuchauka aliyemshinda mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Faith Mitambo, wakati wote wa kampeni alikuwa akihubiri Elimu Kwanza kama kipaumbele cha kwanza cha Ukawa.

Lakini baada ya kuapishwa, mbunge Kuchauka amerejea jimboni akiwa na kipaumbele chake kipya cha ‘Afya Kwanza’ kwa wapiga kura na wananchi wa jimbo la Liwale kwa jumla, akiamini mtu bila ya kuwa na afya bora, hakuna atakayefanya kazi za kuzalisha mali kwa ufanisi, ikiwamo kilimo ambatyo ni shughuli kuu ya wapiga kura wake.

"Nakubaliana na kauli mbiu ya elimu kwanza kwa sababu ilibeba kampeni zetu kitaifa, lakini baada ya kuchaguliwa na kushinda, binafasi nimelazimika kubadili kipaumbele hadi kuwa Afya kwanza kwa sababu ya mahitaji makubwa ya wananchi wangu," anasema.

Mbunge Kuchauka (CUF) anasema, amegudumua mengi juu ya hali ya wananchi wangu kiafya ikiwamo uchache wa vituo vya zahanati, vituo vya afya na hospitali ambapo wilaya nzima ina hospitali moja ya wilaya na kituo cha afya kimoja tu.
"Unaweza kushangaa ukiambiwa kuwa hata hiyo hospitali ya wilaya haina sifa hiyo.

Tangu ipandishwe hadhi kutoka kituo cha afya miaka kadhaa iliyopita, haijawahi kuongezewa jengo hata moja kwa ajili wodi, hivyo kubaki na majengo mawili yenye wodi za watoto, kinamama, kinababa na za wajawazito," anasema.

Anaongeza kuwa, kila eneo ambako ujenzi wa zahanati na vituo vya afya ulianza, umekwama kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kukosa ufuatiliaji wa karibu, hivyo kulazimika kuanza kampeni ya kuendeleza na kuanza upya ujenzi wake.

"Ukifika kata ya Mpigamiti ambako mimi nimezaliwa, pana zahanati ya kizamani na ujenzi wa jengo la kituo cha afya ulianza lakini umekwama kwa sababu ambazo hakuna anayejua kwa sasa. Hali ni mbaya sana, wananchi wanahitaji huduma ya afya na wanalazimikia kutumia hadi zaidi ya kilomita 200 kufuata huduma hiyo Liwale mjini," anasema Kuchauka.

Kutokana na hali hiyo, mbunge huyo analazaimika kuanza na kupeleka jimboni dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya sh.Milioni 6.3 na kukabidhi uongozi wa Hospitali ya Wilaya ua Liwale na sehemu ya vifaa hivyo akavielekeza katika zahanati ya Mpigamiti, ikiwa ni njia ya kujaribu kupunguza pengo la mahitaji.

Anasema anatambua kipaumbele ya kitaifa cha Ukawa ni elimu, lakini kulingana na mahitaji ya jimbo lake ameona aanze na afya na kwamba anaamini watu wake wakiwa na afya bora hata wanafunzi watasoma kwa bidii na kufaulu kwa alama za juu.

"Pia nimesaidia kulipia kaya 100 huduma ya afya kupitia mpango wa CHF kwa mwaka mmoja kama moja ya mikakati ya kuhakikisha kila mwana Liwale anapata huduma ya afya iliyo bora na nitaendelea na jitihada hizo ikiwa pamoja na kuhamasisha ujenzi wa wodi za wagonjwa angalau moja kila mwaka katika hospitali ya wilaya," anasema.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Augustino Mnape, anasema baada ya kupokea vifaa na dawa hizo, ni jambo la kutia moyo kuona mbunge anaguswa na mahitaji ya wagonjwa muda mfupi tangu aingie madarakani.

Mganga huyo aliahidi kuvitumia vifaa na dawa hizo kama ilivyoelekezwa na kwamba anaamini hautakuwa msaada wa mwisho kutoka katika ofisi ya mbunge kwa hospitali hiyo,.

Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Wilson Nyamanga, anayemwakilisha Mkuu wa Wilaya, Ephraim Mbaga, anasema serikali inatambua na kuheshimu misaada ya aina hiyo na mingine inayofanana nayo.

"Kila mwenye uwezo au kuguswa na hali ilivyo katika hospitali yetu, ana haki ya kutoa msaada. Hatuna sababu ya kuweka vikwazo kwa wanaojitoa kusaidia, isipokuwa kila atakayeleta msaada hautakabidhiwa kwanza hadi watalaam wetu wajiridhishe kama ni salama," anasema.

Kauli hiyo ya katibu tawala ilikuja, kufuatia Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mohamed Mtesa anawaonya watumishi wa serikali watakawazuia wanasiasa kukabidhi misaada hospitalini hapo kwa sababu za kisiasa.

Mtesa ambaye pia ni diwani wa Kata ya Liwale B (CUF), moja kati ya kata 14 zilichukuliwa na CUF miongoni mwa kata 20 zinazounda halmashauri hiyo, amwsema, watumishi wa halmashauri hiyo wameanza kuonyesha kubagua misaada inayotolewa na wapinzani bila kujali kuwa ndiyo washindi halali wa uchaguzi uliopita.

“Tangu mbunge alete vifaa na dawa hizi zimepita siku nne kabla hajakubali kuvipokea bila sababuza msingi. Hapo kabla pia mlimzuia kwa muda mtaalam wa kutengeneza mashine ya X-ray kwa visingizio visivyo na maana, acheni tabia hiyo” alisema Mtesa mbele ya watumishi wa hospitali na viongozi wa serikali.

Anasema tabia hiyo, ni ubaguzi na inapingana na matakwa ya wana Liwale walioamua kuchagua upinzani kuongoza halmashauri, hivyo akawataka wakubali matokeo washirikiane kuwaletea maendeleo wananchi.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Wilson Nyamanga anasema serikali haina kinyongo na ushindi wa CUF jimboni humo, isipokuwa kuchelewa kupokea vifaa hivyo kulitokana na watalaam kuchelewa kuvikagua na kuvithibitisha.

“Nawaondolea shaka kwamba huenda serikali imejiegemeza upande fulani wa kisiasa, hapana. Tunaheshimu na kuamini kilichofanywa na wananchi na sisi kama serikali tutashirikiana kikamilifu na vingozi wapya ili kufikia malengo, muhiku ni kuvumiliana tu,” anasema.